Tuesday, 5 July 2016

KITWANGA AKANA KULEWA BUNGENI AZUNGUMZA HAYA KUHUSU LUGUMI

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amemshukuru Rais John Magufuli kwa kipindi kifupi alichofanya naye kazi.

Amesema kwamba hawezi kuhoji juu ya uamuzi uliofikiwa na Rais kutengua uteuzi wake.
“Kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Rais, ni mtu ninayemfahamu, ni mwadilifu na mchapakazi, mimi binafsi siwezi kuhoji juu ya kile alichoamua dhidi yangu maana anayetoa ndiye anayeamua,” alisema Kitwanga.
“Tuache mambo ya longolongo, mimi ni mtu mweledi, nachukia ujinga,” alisema na kuwataka Watanzania wamshukuru Rais Magufuli kwa jinsi ambavyo anatekeleza majukumu yake kwenye mazingira magumu.
Kitwanga alisema hayo jana mjini hapa wakati akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Mwanza nyumbani kwake kuhusu hoja mbalimbali zilizomhusu, ikiwemo ya kutimuliwa kazi ya Uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Rais Magufuli kwa sababu ya kulewa akiwa kwenye vikao vya Bunge mjini Dodoma.
Akizungumzia tuhuma hiyo, alisema hakuwahi kufanya kazi serikalini akiwa amelewa tangu alipoajiriwa miaka ya 1990.
“Miaka hiyo yote nilishindwaje kunywa pombe, na wakati nikiwa Naibu Waziri nimekuwa nikijibu maswali wakati mwingine zaidi ya matatu kwa siku, na wakati mwingine kwa zaidi ya wizara tatu kwa siku, hivi huyo anayesema nimekunywa pombe mmemuuliza?” Alihoji Kitwanga.
Kuhusu sakata la Lugumi, alisema hamfahamu mmiliki wa kampuni hiyo na wakati wote akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, hajawahi kuona nyaraka zozote zinazoihusu kampuni hiyo ofisini kwake.
Alivitaka vyombo vya habari kupata taarifa sahihi juu ya suala hilo, ikiwamo kwenda kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela).
Alipoulizwa na waandishi wa habari ni kwa nini anakana kuifahamu Kampuni ya Lugumi wakati alikuwa Waziri mwenye dhamana, ambayo ndiyo ilimpatia Lugumi mkataba wa ufungaji wa mitambo (mashine) za utambuzi wa alama za vidole kwa vituo vya Polisi nchini, alisema kwa wakati huo hakuwepo ofisini na kwamba hakuwahi kuziona nyaraka za kampuni hiyo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search