Monday, 4 July 2016

MAMBO MATANO AMBAYO YANAWEZA KUHARIBU NDOA YA MWANAMKE -MWANAMKE USIYAFANYE HAYA KAMWE

  July 04/07/2016 at 10:10 am
Bila shaka utakuwa umeshangazwa na kichwa cha habari cha mada yangu ya leo, na umekuwa na hamasa ya kutaka kujua leo tunashauriana jambo gani.

Naam, leo nataka tushauriane kuhusu mambo matano ambayo unafurahia kuyafanya, lakini unaiangamiza ndoa yako na kumharibu mumeo bila wewe mwenyewe kujua.

Tanbihi: japokuwa makala haya yameelekezwa kwa wanawake, lakini yanawahusu pia wanaume.

KUISHI TOFAUTI NA UWEZO WAKO

Mwanamke mmoja katika memba wa jukwaa hili la makala za Mapenzi aliwahi kuandika: “Kitu bora kabisa unachoweza kufanya kama mke ni kuishi ndani ya mipaka ya uwezo wa mume wako.”

Mthamini na umheshimu mume wako kwa kuwa makini katika kufuata bajeti yenu na kutumia vizuri kile mlichonacho. Tumia busara katika matumizi ya fedha zenu.

Kuendelea kulalamika kuwa huna pesa za kutosha kukidhi matamanio yako ya ubadhirifu ni njia dhaifu kabisa ya kusema “ahsante” kwa mume wako mwema ambaye anafanya kazi kwa bidii na anajituma kwa nguvu kubwa kila siku kuhakikisha familia yenu inapata riziki.

Naam, unaweza usiwe na pesa ya kununua mkoba fulani mzuri ambao uliuona duka fulani wiki kadhaa zilizopita, lakini mume wako atapenda na kukuthamini kwa sababu anaona kwamba unamheshimu na kumshukuru kwa kile kidogo anachokupatia.

KUENDELEZA MTAZAMO HASI

Unaweza ukawa unazichukia nywele zako, unachukizwa na mtu fulani au kitu chochote. Mume wako anapokanyaga mguu nyumbani, unamsukumizia kila baya na hasi ambalo umekutana nalo kwa siku nzima.

Fikiria kama ni wewe unasukumiwa mzigo huo ungejisikiaje? Siku zote kuwa na mtazamo hasi sio jambo zuri. Wanaume wanapenda kutatua mambo, na kuwatwisha mzigo wa malalamiko yasiyohesabika humfanya mumeo apate ugumu katika kukusaidia kuondokana na maumivu uliyonayo.

Kama kuna kitu ambacho tunajifunza katika maisha ya ndoa ni kwamba mwanaume mzuri na mwema anapenda uwe na furaha, na akishindwa kukusaidia katika hilo, naye hukosa furaha. Ni kweli siku hazilingani, unaweza kuwa umechefuka siku moja, hilo linaeleweka, lakini usilifanye kuwa ndio mtindo wa maisha yako.

KITU KINGINE KWANZA

Unapowaweka watoto, marafiki, kazi na mambo mengine kuwa kitu cha kwanza mbele ya mumeo, unakuwa unamtumia ujumbe wa wazi kwamba yeye sio muhimu. Fikiria kama wewe ndio ungekuwa unatumiwa ujumbe huo kila siku na kwa miaka mingi ungejisikiaje?
Muweke mumeo mbele, mumeo kwanza.

Ingawa wakati fulani unaweza kuona kama ni jambo gumu, lakini utashangaa kuona kuwa jambo hilo ni ufunguo kuelekea kwenye furaha kuu katika ndoa. Wanandoa wengi huchokana na kuingia katika migogoro, kwa sababu wanapuuza suala la kuhudumiana, kupendana na kumuweka mwenzako mbele ya kitu kingine chochote. Kumbuka hili: mumeo kwanza, mkeo kwanza.

Ukimuweka mwenzako mbele, utagundua hazina kubwa ya furaha inayopatikana katika jambo hilo.

KUMKATALIA TENDO LA NDOA

Katika makala ijayo tutazungumzia mambo nane ya kumuweka sawa mume” tutaelezea kuhusu umuhimu wa tendo la ndoa kwa wanaume na tofauti ya kibiolojia iliyopo baina ya mwanaume na mwanamke. Wanaume wanahitajia sana tendo la ndoa kutoka kwa wake zao. Unapoendelea kumkatalia tendo la ndoa unakuwa unauchosha moyo wake na kuufanya kuwa wenye kutu na usugu. Kiujumla unakuwa unamhribu.

Tendo la ndoa lisitumike kama nyenzo ya kumdhibiti mwenza wako; bali litazamwe kama nyenzo tukufu ya kuzidi kuwaweka karibu.

Ni baraka kubwa unapohitajiwa na mume  anayetaka kushirikiana nawe peke yako jambo zuri na muhimu. Wakati fulani unaweza usiwe katika hamasa ya kufanya hivyo, lakini ni jambo zuri kuonesha kuwa nawe unamhitaji na kutumia muda pamoja.

KUTOZUNGUMZA LUGHA YAKE

Wanawake hawapendi kuwa wawazi. Nadhani hiyo ni sehemu ya maumbile yao. Lakini, wanaume hawawaelewi. Na nadhani hilo pia ni sehemu ya maumbile ya wanaume. Wanapata shida kuwaelewa wanawake.

Usipoteze muda wako kwa kueleza mafumbo ambayo hayaelewi: zungumza naye kwa uwazi. Zitendee haki hisia zako, na usifunike vitu ambavyo vitajazana na baadaye kupasuka. Akikuuliza una tatizo gani, usisema “hakuna kitu” halafu ukatarajia kwamba atayasoma mawazo na hisia zako. Kuwa muwazi kuhusu hisia zako.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search