Saturday, 16 July 2016

USHAURI WA BURE KWA RC. PAUL MAKONDA!


Na. Mtatiro J.
Mkuu wetu wa mkoa na kijana mwenzetu, huna haja ya kuzungusha Polisi mitaani kukamata Raia wasio na hatia kwa kutumia mamlaka yoyote unayodhani unayo. Common Sense peke yake haikubaliani na jambo hilo;
1. Zoezi lenyewe haliwezekani na halitekelezeki hata kidogo. Halina BASIS za kisheria wala KIMAADILI, kwa hiyo ni NULL and VOID tangu tu ulipolitangaza.
2. Litazua vurugu, balaa na machafuko mitaani na litashindwa kwa asilimia 100 na ni aibu sana kwa kijana mwenzetu ku attempt vitu visivyowezekana.
3. Nakupa ushauri wa bure ndugu yangu, kwamba kama anataka kuwabaini na kuwakamata wakazi wa DSM wasiofanya kazi na wasio na ajira, hebu pitia daftari la Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2012. Takwimu za sensa zimeeleza vizuri sana, mtaa gani una vijana wangapi na hali zao zikoje. Usiwahangaishe polisi.
4. Kisha, toa maelekezo kuwa vijana hao na wananchi wasio na shughuli za kufanya waje wenyewe ofisini kwako, taja tarehe na muda. Mimi kwangu ninao kama 7 hivi, ntawaleta mimi mwenyewe kisha ntakuachia uchukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria kwa makosa yao ya kutokuwa na shughuli za kufanya.
5. Wewe ni kijana mwenzetu na kila unapotoa matamko dhaifu na yasiyo na tija kwa taifa unafanya wananchi wote waamini kuwa VIJANA wa taifa hili hawajakomaa na hawako tayari kuongoza nchi. Ikiwa viongozi vijana tunashindwa kupigania ajenda muhimu za kijamii pindi tunapokabidhiwa mamlaka ya uongozi wa nchi, tunaiandaa jamii itupe hukumu gani mbeleni?
6. Comrade Paul, wewe ni kiongozi mwenye utashi na kwa tunaokufahamu tunajua unayo talanta bora ya uongozi, lakini umeiweka kando. Hivi sasa unaendeshwa na ukuu na kutikisa watu bila sababu. Yuko wapi yule Makonda ambaye aliendesha kampeni ya usafi jijini DSM? Iliishia wapi kampeni ile? Mbona wananchi walikuunga mkono brother? Usafi uliona hautoshi sasa unataka kuwasaka wasio na kazi? Ili iweje? Na unadhani nani atakubali kusakwa na kukamatwa kwa sababu hana kazi, kazi ambayo hajawekewa mazingira ya kuipata kwa kuajiriwa au kujiajiri?
7. Ndugu Paul, unakumbuka ulitangaza kuendesha msako wa ombaomba? Unakumbuka tulivyokuunga mkono? Jamii nzima ya DSM. Ombaomba ni kero kubwa sana na hawapaswi kuchekewa, ukifanya zoezi la kuwarudisha vijijini kila mtu atakuunga mkono. Unakumbuka zoezi la kukamata SHISHA na watumiaji wake? Unakumbuka tulikupongeza na tulikuusia kuwa ungelianza na wasambazaji wa madawa ya kulevya kwanza? Maana COCAINE na HEROIN zinauzwa kama njugu hapa jijini tena huenda unawajua wauzaji hadi majumbani mwao, tulikushauri tu.
8. Kaka Paul, kwa mtizamo wangu, anza kujifunza kujenga DAR yenye utulivu, yenye mipango inayotekelezeka na yenye maelewano. Kamwe usijifunze kuanzisha mazoezi yasiyotekelezeka au ambayo yakitekelezeka yanaweza kuleta balaa kubwa. Unaikumbuka ARAB UPRISING? Ilianzaje? Kijana hana ajira, anajiuzia mbogamboga askari wakaenda kulivunja na kulichoma banda lake na mboga zake, kijana yule akaamua kujitia PETROLI, akaungua hadharani, video zake zikasambazwa, jamii ikashikwa na ghadhabu, maandamano yakaanza mataifa ya Uarabuni, watawala wakang'olewa. Chanzo cha maafa ya Uarabuni ni watawala kushindwa kuweka mazingira rafiki ya ajira kwa jamii zao na kisha watawala hao hao wakaanza kuwanyanyasa watu wasio na ajira.
9. Kiongozi wangu Makonda, UKOSEFU WA AJIRA au SHUGHULI ZA KUFANYA ni bomu lililotulia mahali na aliyelilea anafahamika, ni chama chako, CCM. Chama ambacho kimekupa ukuu wa mkoa ndicho kimeongoza taifa hili kwa miaka 50 sasa, kimeshindwa kuitumia nguvu kazi ya taifa na leo tuongeapo, mamilioni ya vijana hawajui nini wafanye. Hata ajira za kuuza pipi zinafanywa na WACHINA. Hawa vijana unaotaka kuwasaka majumbani watafanya nini? Kwa nini unataka kulitegua BOMU lililojituliza huku hauna utaalamu huo? Likilipuka kwa vyovyote vile hautabaki salama! Utapata madhara. Bomu hili linahitaji PATIENCE na CALMNESS, linahitaji wataalamu waliobobea waje na vifaa vyao. Huwezi tu kubeba ndugu zetu POLISI na kuwabambikizia oparesheni isiyo na nguvu ya kisheria na inayoweza kuleta vurugu na matatizo mitaani.
10. Mdogo wangu Paul Makonda, wanasiasa wengi huwa hawapebdi kushauriwa hadharani, hukasirika na kuwaona washauri wa namna hiyo kama watu wanaowachukia. Mimi ni mwanasiasa kijana kama wewe na huwenda nimewahi kushika majukumu makubwa sana. Huwa nafurahi sana kila nionapo watu wananishauri hadharani, hasa kwa lugha ya heshima kama niliyotumia hapa. Mara kadhaa umewahi kuwa na hofu nami hasa nilipowahi kukukosoa sana kwa hatua ya kumkamata mbunge Kubenea na kumuweka ndani, niliwahi kukukosia pia ulipowaweka ndani watumishi wa halmashauri kwa kuchelewa kazini. Sijawahi kufanta hivyo kwa nia mbaya ,mara zote dhamira yangu inanisuta napoona kijana mwenzangu anaharibu kwenye uongozi. Huwa natoa ushauri huo kwa kijana yeyote yule bila kujali anatoka chama gani. Ni kama mimi mwenyewe navyopenda kupokea ushauri kutoka kokote, ilimradi utumie lugha inayokubalika. Mimi ni kati ya watu ambao wataendelea kukushauri na kukukosoa, bila kujali kuwa unaweza kuchukia na kukasirika kama wanavyoogopa wanasiasa wazee, wanapokosolewa hadharani. Sitajali, ntaendelea na kazi. Kumbuka, anayekukosoa ANAKUPENDA NA KUKUTAKIA MEMA, anayekusifia wakati unakwenda kutegua mabomu bila wataalamu, ANAKUTAKIA MABAYA.
Julius Sunday Mtatiro,
+255787536759 (Whatsup and Text only) juliusmtatiro@yahoo.com
Dar Es Salaam.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search