Wednesday, 22 March 2017

Mke wa Rais na Vibweka Vyake

Mke wa Rais alipojua udhaifu wa mume wake, kwamba anampenda sana acha afanye vituko. Nchi ikasimama. Vurugu zote yeye. Nani wa kumzuia na ndiye usingizi wa Mkuu wa Nchi?

Watu waliufahamu ukali wa Rais lakini wakawa wanastaajabu ukimya wake juu ya vitendo vya mkewe. Wengine wakasema Rais ni Bushoke, wapo waliodai Rais huchimbwa mkwara wa kunyimwa unyumba ndiyo maana alikuwa mpole.

Lucy Kibaki, Mungu amrehemu, aliitikisa Kenya miaka 10 ya Urais wa mume wake, Mwai Kibaki, kati ya mwaka 2002 mpaka 2012.

Lucy hakuwa wa mchezo, alivamia chombo cha habari na kushambulia wahariri. Aliwahi kumpa makofi mpiga picha wa gazeti la Nation kwenye kadamnasi. Watu wakashangaa. Mume wake akawa kimya.

Mwaka 2007, katika sherehe ya Siku ya Jamhuri, iliyofanyika Ikulu, MC alimtambulisha Lucy Kibaki kwa majina ya Lucy Wamboi Kibaki badala ya Lucy Muthoni Kibaki, basi MC mbele za watu akachezea makofi.

Kibaki alishuhudia lakini afanye nini? Lucy ndiye usingizi wake. Mama akazidi kutamba, akamtwanga makofi mtumishi wa Ikulu, Matere Keriri. Halafu akatamba: “Nikisema mimi ndiyo sauti ya mwisho.” Usimchezee mama Prezidaa!

Bunge la Kenya likachachamaa na kumsema Kibaki kwa kushindwa kumdhibiti mkewe. Lucy akamwambia mwanasheria Gitobu Imanyara, afungue kesi dhidi ya wabunge. Imanyara aliposema mashitaka yasingekuwa na nguvu, alichezea makofi.

Kibaki alikuwa na kawaida ya kuwaalika marafiki zake na kupata mvinyo kwenye baa ya Ikulu. Lucy akatimua marafiki wa Kibaki halafu akaagiza baa ifungwe.

Kipindi fulani vyombo vya habari viliripoti Kibaki alikuwa na mke mwingine tofauti na Lucy, basi mama akachachamaa, akamwagiza mumewe afanye mkutano na waandishi wa habari ili akanushe. Kibaki alikanusha huku Lucy akimsimamia.

HATA MAREKANI

Rais wa 19 wa Marekani, Warren Harding naye alikuwa mnyonge kwa mkewe, Florence Harding. Wakati huo, mpaka magazeti yaliandika kuwa nchi ilikuwa na inaongozwa na First Lady.

Florence aliagiza intelijensia kufanya kazi, alimwandikia Rais Harding cha kuzungumza kwa waandishi wa habari. Florence ndiye alikuwa kila kitu kwa Serikali ya Marekani. Florence aliwahi kusema yeye ndiye sauti ya Rais. Ni kama mtu mzima Robert Mugabe alivyo mpole kwa Grace.

Unajua jeuri yote ya nini? Ni mke kujua anapendwa. Mke wa Rais asiye na busara akishajua mume wake amependa mpaka ameoza kwake, basi hufanya vituko mpaka kumdhalilisha Rais mwenyewe na nchi yote

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search