Wednesday, 22 March 2017

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YALLAANI KITENDO CHA MAKONDA KUVAMIA OFISI ZA CLUODS MEDIA

Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz

Machi 22, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

THBUB yalaani uvamizi wa studio za Clouds Media

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepata taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu uvamizi wa kituo cha Luninga na Radio cha Clouds Media Group, uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda, usiku wa tarehe 17, Machi mwaka huu, akiwa na askari wenye silaha.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, inadaiwa kuwa Mhe. Mkuu wa Mkoa alifika katika studio hizo kwa lengo la kushinikiza kutangazwa kwa taarifa iliyokuwa na maslahi yake binafsi.

Kitendo cha Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam kuvamia kituo cha Clouds Media Group ni kitendo kinachopingana na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayolinda uhuru wa maoni na mawasiliano, jambo ambalo pia linalindwa na Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (1966), na Ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (1986).

Tume imepitia Sheria kadhaa, ikiwemo Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura ya 97 ya Sheria za Tanzania, na imebaini kwamba hakuna Sheria inayomruhusu Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za uvamizi, kama alivyofanya Mhe. Makonda.

Hivyo, hatua ya kuvamia kituo cha habari cha Clouds, akiambatana na askari wenye silaha ni kitendo kisichojali, wala kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu. Ni kitendo cha kujichukulia sheria mkononi na kisichokubalika katika jamii au nchi ya kidemokrasia.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapenda kuungana na Watanzania wengine kulaani kitendo hicho.

Hivyo, Tume inashauri:

  1. Mhe. Paul Makonda akiri kuwa kitendo alichofanya ni uvunjifu wa haki za msingi za waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari.
  1. Kitendo cha kuvamia kituo cha Luninga na Radio cha Clouds Media Group kwa kutumia askari wa Jeshi la Polisi kwa maslahi binafsi ni kitendo kisichoendana na utawala wa Sheria, Mhe. Makonda amelidhalilisha Jeshi la Polisi, kwa hiyo ni budi awaombe radhi Watanzania.
Imetolewa na:

(SIGNED)

Mhe. Bahame Tom Nyanduga

Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Machi 22, 2017

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search