Tuesday, 16 May 2017

AGIZO LA WAZIRI KWA WAKUU WA MIKOA KUHUSU SUALA LA MADAWATI

Na Silvia Hyera.
 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI)  Mhe. George  Simbachawene amewataka  Wakuu wa Mikoa nchini   kufanya  tathmini  ya madawati  katika Mikoa yao  ili kupata taarifa  kamili  ya  madawati  yaliyopungua, kuhakikisha wanatawanya madawati yaliyokwisha tengenezwa pamoja na kutengeneza  madawati yaliopungua.
Mhe. Waziri ametoa agizo hilo  leo alipozungumza na waandishi wa habari  ofisini kwake  Mjini Dodoma katika mkutano na vyombo vya habari  ambapo aliwataka Wakuu wa Mikoa kusimamia  zoezi hili kikamilifu  na kuhakikisha  madawati yaliyotengenezwa yameingizwa kwenye vyumba vya madarasa  na sio kutoa taarifa ya kuwapo kwa madawati hayo kwa mafundi.
 “Wakuu wa Mikoa wanatakiwa kuja na taarifa sahihi ya idadi ya madawati iliyopo ukilinganisha na mahitaji  vinginevyo tutadanganyana kwamba madawati yapo mengi lakini kumbe baadhi ya watoto wanakaa chini” alisisitiza Mhe. Simbachawene
Alisema  kuwa kuna baadhi ya Mikoa wana madawati mengi  lakini hayajafika kwenye shule zenye upungufu hivyo ni jukumu la wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa madawati hayo yanafika mashuleni kwa wakati.
Mhe. Waziri alisema  kuanzia Disemba 2015 Serikali ilianza kutekeleza sera ya Elimu Msingi  bila malipo na kutokana na utekelezaji huo,mwitikio wa wananchi kupeleka watoto shuleni umekuwa mkubwa na  kuleta changamoto ya upungufu wa miundombinu muhimu kama vile vyumba vya wadarasa na matundu ya vyoo.
 Aidha,  Mhe. Simbachawene  ametoa   rai  kwa wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kutochoka kuendelea  kushirikiana na Serikali  katika kuboresha miundombinu hiyo muhimu kwenye shule kama walivyotoa ushirikiano wa dhati kukabiliana na upungufu wa madarasa.
Mnamo tarehe 16 Machi, 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Mgaufuli aliagiza kuwa kusiwepo na mtoto anayekaa chini kwa kukosa dawati. Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Elimu nchini wametekeleza agizo hilo kwa kiwango kikubwa.
 Kabla ya agizo hilo mahitaji ya madawati kwa shule za Msingi yalikuwa  3,252,313 na katika shule za Sekondari 1,495,610.  Hadi sasa madawati yaliyopo ni 3,319,355 kwa shule ya Msingi  na kufanya kuwa na ziada ya madawati 66,042 na kwa upande wa Sekondari madawati yaliyopo ni 1,540,625 na kufanya  kuwa na ziada ya madawati 45,015.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake Mjini Dodoma katika mkutano na vyombo vya habari na kutoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kutatua changamoto ya upungufu wa madawati kikamilifu kwa kuhakikisha madawati yaliyotengenezwa yameingizwa kwenye vyumba vya madarasa na kutengeneza madawati yaliyopungua

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search