Saturday, 6 May 2017

ASILIMIA 90 YA WAANDISHI NA WATANGAZAJI WA HABARI HAWANA SIFA

Dodoma. Ukaguzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwenye vituo vya utangazaji ili kuhakiki vitendea kazi na ubora wa huduma umebaini kuwa asilimia 90 ya wafanyakazi hawana sifa stahiki katika taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2017/18.

Alisema suala hilo ni changamoto kubwa katika tasnia ya habari na utangazaji.

Maeneo yaliyohakikiwa katika ukaguzi huo ni studio, vyumba vya habari, maktaba, utaratibu wa ndani wa kuandaa na kutangaza vipindi, sifa za watangazaji na waandishi wa habari pamoja na mikataba ya ajira.

Hata hivyo, alisema vituo vyote vilivyokaguliwa vimeonyesha ubora katika kutoa huduma kwa wasikilizaji  wake katika maeneo husika ikiwa ni pamoja na ubora wa usikivu ambao hauna miingiliano ya sauti, ubora wa vitendea kazi katika vituo, uelewa wa taratibu na sheria za utangazaji pamoja na ubora wa kutoa na kutimiza haki na masilahi ya wafanyakazi wake.

Akizungumzia Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC), Dk Mwakyembe alisema liliendelea kuboresha usikivu katika maeneo ya mipakani ambayo ni Kakonko, Kibondo, Nyasa, Longido, Rombo na Tarime.

Alisema hatua zilizofikiwa ni wataalamu kufanya upembuzi yakinifu kubainisha maeneo itakapofungwa mitambo na kuandaliwa hadidu za rejea na shirika limekwishaomba masafa TCRA kwa ajili ya maeneo hayo.

“Zabuni kwa ajili ya kununua mitambo ilitangazwa Februari 4, 2007 na kazi ya kufunga mitambo inatarajiwa kukamilika mwaka huu wa fedha,” alisema Dk Mwakyembe.

Aliomba Bunge liidhinishe Sh28.2 bilioni, kati ya hizo Sh17.3 bilioni kwa ajili ya mishahara, Sh4.6 bilioni za matumizi mengineyo na Sh6.3 bilioni za miradi ya maendeleo.

Waziri huyo alisema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, mwaka 2016/17 wizara hiyo ilikuwa na changamoto saba ilizokabiliana nazo kama sera na sheria za sekta za sanaa, utamaduni na michezo kutokidhi mahitaji ya sasa.

Changamoto nyingine ni kutozingatiwa kwa maadili ya uandishi wa habari uchakavu wa mitambo ya TBC na kuwapo mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Nyingine ni wadau wa tasnia ya sanaa kutozingatia sheria, kanuni na taratibu za kuendesha shughuli za sanaa nchini, eneo la Taasisi ya Sanaa Bagamoyo kumegwa na bahari pamoja na mwamko na uelewa mdogo wa umuhimu wa jamii kushiriki michezo.

Maoni ya Kamati

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alisema pamoja na kwamba TBC ndilo shirika pekee la Taifa lakini lina hali mbaya ya miundombinu na teknolojia kwa maana ya mitambo duni na kompyuta zilizochakaa.

Alisema vyumba vya kurushia matangazo ni vidogo na visivyovutia na ukumbi mdogo wa mikutano ukilinganisha na ukubwa wa shirika.

Mbunge huyo alishauri TBC iwezeshwe kifedha na kuwa ilikwishaandika andilo lenye kuonyesha mahitaji yanayofikia Sh80 bilioni kwa ajili ya kunusuru hali yake.

“Sekta ya habari inahitaji uwekezaji kama ambavyo Azam TV imefanya kwani imetumia takriban dola za Marekani milioni 40 ambayo ni sawa na takriban Sh90 bilioni,” alisema Nkamia ambaye baada katika mchango binafsi alisema ana uchungu na TBC kwa kuwa ndiko alikokulia.

Alisema kama kweli Serikali ina nia ya dhati kuifanya TBC kuwa shirika la utangazaji la Taifa, basi iwekeze vya kutosha kwa kutenga bajeti nzuri na kupeleka fedha za tozo za ving’amuzi.

Alishauri Serikali iiwezeshe TBC katika kujenga studio ya kisasa Dodoma kwa kuwa iliyopo haiendani na kadhi ya makao makuu.

Kuhusu bajeti, Nkamia alisema pamoja na Serikali kuongeza bajeti kwa asilimia 22, kamati inaona fedha hizo bado hazitoshi hivyo iziongeze na kuzitoa kwa wakati.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel alisema mitambo ya TBC imechoka mno na inatakiwa ibadilishwe.

“Ukiona jinsi watangazaji wa shirika hilo wanavyojituma lakini utawaonea huruma kwa jinsi mitambo yao ilivyochakaa,” alisema.

Alisema hata posho hawapati, wanadai posho za miezi saba na hivi karibuni wamelipwa za miezi minne.

Alimtaka waziri Mwakyembe alieleze Bunge tangu TBC iingie ubia na Star Times wamefaidika vipi.

Alisema alipoingia Mkurugenzi Tido Mhando aliikuta ina Sh6 bilioni ndiyo maana ikafanya vizuri haraka, lakini huyu wa sasa Dk Ayub Rioba ameikuta haina kitu na kuhoji, atawezaje kufanya vizuri.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search