Wednesday, 10 May 2017

BEI YA SUKARI YAPAA

BEI ya sukari katika jiji la Dar es Salaam imeendelea kupaa, huku baadhi ya maeneo ikianza kuadimika.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA umebaini kupanda kwa bidhaa hiyo kutoka Sh 2,300 hadi 2,800 kwa kilo moja.

Gazeti hili lilifika kwa Wakala Mkuu, Haroun Zacharia na kukuta mfuko wa sukari wenye uzito wa kilo 50 umepanda kutoka Sh 104,000 hadi 116,000.

Mfuko wa kilo 25 unauzwa Sh 58,000 badala ya Sh 52,000, huku ule wa kilo 20 ukipanda kutoka Sh 42,000 na sasa unauzwa kwa Sh 46,000.

Kwa Wakala Mkuu mwingine, Mohamedi Enterprises, mfuko wa kilo 50 umeuzwa kwa Sh 118,000 hadi 120,000, mfuko wa kilo 25 unauzwa Sh 58,000 na wa kilo 20 umeuzwa kwa Sh 47,000.

Mmoja wa wafanyabiashara wa jumla, Lucas Tarimo, alisema kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kunatokana na viwanda vya sukari kufungwa ili kufanyiwa usafi.

Alisema sukari imeanza kuadimika na kusababisha baadhi ya wafanyabiashara rejareja kupandisha bei na kuzusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Mara nyingi viwanda hufungwa katika miezi hii ili kufanya usafi na hivyo kusababisha upungufu wa sukari,” alisema Tarimo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search