Monday, 22 May 2017

GAMBO Atangaza Kusitisha Kupokea Pesa za Rambirambi za Msiba wa Wanafunzi wa Arusha


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAPATO NA MATUMIZI YA MSIBA WA AJALI YA LUCKY VINCENT MKOANI ARUSHA
TAREHE 21 MAY 2017
Mnamo tarehe 19 May 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha ilitoa taarifa ya mapato na matumizi kuhusu michango ya Rambirambi ya ajali ya basi ya shule ya Lucky Vincent iliyotokea Wilayani Karatu eneo la Rhotia. Ajali hiyo ilitupotezea wapendwa wetu 35, wakiwemo wanafunzi 32, walimu 2 na dereva 1.

Aidha, ajali hiyo pia ilitubakishia Majeruhi 3 ambao hali zao zilikuwa ni mbaya sana. Tunaamini Mwenyezi Mungu ana makusudio yake kuwaacha hai hawa Majeruhi 3 kwenye ajali mbaya kama ile.

Baada ya Serikali na wadau mbalimbali nchini kushilikiana kufanikisha kuihifadhi miili ya wapendwa wetu ikiwa ni pamoja na kutoa fedha taslimu za rambirambi kiasi cha shilingi 3,857,000 kwa kila familia iliyofiwa kwa familia zote 35. Kwa ujumla tumeona ni vema sasa nguvu kubwa ikapelekwa kwenye kuwahudumia majeruhi ili waweze kupona na makusudio ya Mungu yaweze kutimia.

Tunapenda kuujulisha Umma kuwa hadi Ijumaa ya tarehe 20 May 2017 kutokana na wadau kuendelea kuchangia tumebakiwa na kiasi cha Shilingi 67,993,885. Kwa mantiki hiyo busara imeelekeza kuwa nguvu kubwa sasa ipelekwe kwenye kuwahudumia majeruhi, maana hata tufanyeje kwa wale ambao Mungu kwa mapenzi yake amewachukua hatuna namna tena ya kuwarudisha.

Hivyo, tunapenda kuujulisha Umma kuwa Jumatatu tarehe 22 May 2017 tutazitumia familia za majeruhi pamoja na Madaktari wetu waliojitoa kuwasindikiza majeruhi kiasi cha Dola za kimarekani 20,000 (Sawa na 44,720,000 kwa Exchange rate ya 2,236 , kila familia itapata Dola 5,000 (Jumla ni Dola 15,000 kwa familia 3), Daktari Dola 2,500 na muuguzi Dola 2,500 kama sehemu ya kuendelea kuwafariji na kuwapunguzia changamoto huko ugenini.

Kwa ujumla baada ya yote hayo tutabakiwa na kiasi cha shiliingi 23,273,885 huku tukiendelea kuangalia hali za majeruhi wetu. Kiasi cha fedha kilichobaki kitaendelea kuwekewa utaratibu kupitia timu ya wafiwa 4 walioteuliwa na wafiwa wenzao kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mapato na matumizi ya suala hili yanaeleweka vema kwa Umma.

Pia tunapenda kuuhabarisha Umma kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha imehitimisha rasmi zoezi zima la kupokea rambirambi ili ipate muda zaidi wa kufuatilia Mustakabali wa Majeruhi wetu walioko haspitalini nchini Marekani.

Imetolewa na:
Mrisho Mashaka Gambo
Mkuu wa Mkoa Arush

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search