Tuesday, 30 May 2017

KAMA MPENZI WAKO ANATABIA HIZI,UNAHITAJI KUFANYA MAAMUZI YA HARAKA

Katika mahusiano, kila mmoja huwa na malengo ambayo hudhani yatakuwa nafaida kwake na kwa mpenzi wake katika maisha yao. Kila mmoja hufurahi kama malengo yake yatatimia ndani ya mahusiano aliyopo.
Lakini wengi huudhiwa na kuvunjika moyo pale ambapo hukosa kile wanachokitarajia, haswa kupotezewa muda katika mapenzi. Hili huwaathiri sana wasichana kwani wao huwa na hulka ya kupenda na kusahau mambo mengine. Hivyo anapogundua kuwa mtu uliyenaye katika mahusiano siyo sahihi bali anampotezea muda tu, huwa wanavunjika moyo.
Haya ni baadhi ya mambo yanayoonyesha kuwa, uliye naye huenda si mtu sahihi;
Hataki ujulikane
Matapeli wengi wa mapenzi huwa na tabia hii na huwa ni watu wa kufanya mambo kwa upekee sana. Kila dakika hakaukwi na neno ‘I love you’, lakini moyoni mwake hakuna alama hata moja ya mapenzi kwako. Ni vigumu kumtambua mtu wa aina hii lakini chunguza kuhusu hili, hapendi kabisa kukukutanisha na rafiki zake na hata mkikutana nao kwa bahati mbaya hatakutambulisha na kama atakutambulisha , hawezi kukutambulisha kama mpenzi wake rasmi. Hata ukimuuliza ni kwa nini hatokuwa na jibu la kueleweka.
Mtu kama huyo anakulaghai tu, na unapaswa kujiuliza kama anashindwa kukutambulisha tu kwa rafiki zake, je ataweza kufika kwa wazazi wako na kufuata taratibu zote za ndoa?
Msiri kupitiliza
Siku zote watu wa aina hii hufanya mambo yao kwa siri kubwa. Kama mna miadi ya kukutana, hataki muongozane, atakuwambia mkutane moja kwa moja sehemu husika. Hata muda wa kuondoka atafanya kila njia ili kila mmoja aondoke mwenyewe na kama mkiondoka pamoja basi ujue ni usiku na hakuna atakayewaona.
Ikitokea akakubali kuongoza na wewe, hatapenda muongozane pamoja. Atalazimisha utangulie mbele yeye afuate nyuma, kwa sababu anaogopa kujulikana kuwa ni mpenzi wako. Fikiria, kama anaogopa kujulikana, huyo anakupenda kweli? Anakupotezea muda huyo. Hakuna mapenzi yanayofanywa kwa siri.
Hapendi ndugu wafahamiane
Mpenzi wa aina hii huwa ni mjanja sana, kwanza kabisa atajifanya mtu mwenye ubize sana. Yote hii ni kukwepa kuwajua ndugu zako au wewe kuwajua ndugu zake. Wakati mwingine anakuwa hapendi ndugu zako na wake wakutane wakijua wazi kuwa nyie mna uhusiano.
Hakuna uhusiano wenye heri na malengo ya kuishi pamoja siku zijazo ukawa kwa kificho cha kiasi hicho. Kama ana nia na wewe basi atahakikisha anawafahamu baadhi ya ndugu zako na wewe unawafahamu baadhi ya ndugu zake, hayo ndiyo mapenzi ya kweli. Mapenzi hayaishii kwa ninyi wawili pekee, bali hata kwa ndugu zenu. Mnapojuana inakuwa rahisi kusaidiana hata katika mambo mengine ya kawaida.
Lakini kumbuka, jambo hilo haliwezi kuwa la muhimu wakati mwenzako hana wazo la kukuoa. Wakati ukiwaza maisha , ukiwa na ndoto za kuolewa naye, mwenzako anawaza ngono tu. Kumbuka mwili wako una thamani kubwa sana, uheshimu. Usijishushe kiasi hicho, ukigundua hayo na mengine yanayofanana na hayo ni boara kuchukua hatua kwa kuangalia ustaarabu mwingine.
Kumbuka huyo anayekupotezea muda na kukuchezea hivi sasa, hana thamani kama aliyeandaliwa kwa ajili yako. Yupo lakini hujakutana naye, ni suala la muda tu

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search