Monday, 15 May 2017

KITILA BAJETI YA MAJI INATOSHA

-Amesema endapo pesa zote Bil672 zinatosha kutekeleza mipango yote ya mwaka huu.
-Amesema pamoja na kujitosheleza kwa miladi hiyo, bado wizara hiyo imepata mkopo wa Dola 500 Mil kutoka Exim Bank India, ambayo itatolewa kwa muda wa miezi 30 itakayosaidia miradi katika miji 16 Tanzania bara na mmoja Zanzibar.
-Wakipata fedha hizo zitasiaidia zaidi katika kutekeleza miradi yao.


Dar es Salaam. Wakati Bunge likipitisha bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ya Sh 672 bilioni iliyozua mjadala mzito kuhusu kiwango cha fedha, katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo amesema endapo fedha zote zitatolewa na Serikali, bajeti hiyo itajitosheleza utekelezaji wa miradi ya mwaka huu.

Profesa Kitila ametoa kauli hiyo alipoulizwa na gazeti hili kama kiwango hicho cha fedha kitatosheleza mahitaji ya miradi ya maji kama wabunge walivyoonyesha wasiwasi.

Wakati wa kujadili bajeti hiyo, wabunge walipinga vikali kitendo cha Serikali kupunguza fedha kulingana na mwaka uliopita--kutoka Sh915 bilioni hadi takriban Sh620 bilioni--wakisema hakionyesha dhamira thabiti ya kuwatua wakina mama ndooo kama CCM ilivyoahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Akizungumzia mijadala hiyo, Profesa Kitila aliwatuliza wabunge akisema fedha hizo zitatosha.

“Katika miradi hiyo ipo inayotekelezwa na Tamisemi katika kupitia halmashauri, inayotekelezwa na Serikali Kuu na mingine inayotekelezwa na sekta binafsi. Sasa sina takwimu hapa ila muhimu ujue tu miradi ni mingi na haiwezi kutekelezwa kwa mwaka mmoja, lakini fedha hiyo ikitolewa yote inaweza kutusaidia kwa kiasi kikubwa sana,” alisema.

Profesa Mkumbo alisema pamoja na kujitosheleza kwa bajeti hiyo, wizara hiyo imepata mkopo wa Dola500 milioni za Marekani kutoka Benki ya Exim ya nchini India.

Alisema mkopo huo utatolewa katika kipindi cha miezi 30 ijayo na utasaidia kutekeleza miradi katika miji 16 ya Tanzania Bara na mmoja wa Zanzibar.

“Sasa tukipata na fedha hizo bajeti yetu itakuwa imeongezeka zaidi katika kusaidia utekelezaji wa miradi ya maji,” alisema.

Hata hivyo, Profesa Kitila aliunga mkono hoja zote zilizotolewa na wabunge wakati wa kujadili bajeti hiyo, akisema mwelekeo wa hoja hizo ulionyesha wasiwasi wa bajeti hiyo ukilinganisha na changamoto iliyopo.

Alisema baada ya kikao cha mkutano huo, Kamati ya Bunge inayohusika na wizara hiyo ilikutana na Serikali na kuyachukua mapendekezo hayo ili kuyafanyia kazi.

“Mapendekezo yana tija kubwa sana, yanalenga kusaidia wizara kuongeza uwezo wake ili kufikia malengo yake,” alisema.

Miongoni mwa wabunge waliopinga kiwango hicho cha fedha ni mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) ambaye aliwataka wabunge wasikubali kuipitisha.

Naye mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alisema licha ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza na kasi ya kurejesha nidhamu serikalini, kubana matumizi, kuondoa wafanyakazi hewa huku uchumi ukikua kwa kasi ya asilimia saba, wananchi hawatairudisha madarakani CCM endapo haitashughulikia kero ya maji kote nchini.

Kilio cha maji kilitawala mikutano mingi ya kampeni za wagombea urais na wabunge.

Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search