Tuesday, 9 May 2017

MKAGUZI WA VYETI FEKI AKUTWA NA VYETI FEKI


Muosha huoshwa. Ndivyo ilivyo kwa mmoja wa wahakiki wa vyeti vya elimu katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Mkaguzi huyo naye ametajwa  katika orodha ya watumishi wanaotuhumiwa kuwa na vyeti vya kughushi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kumaliza kwa mafanikio kazi ya kuhakiki wafanyakazi wengine iliyomsababishia lawama na sasa ni mmoja wa wanaotakiwa kuondoka kazini kabla ya Mei 15.

Mkaguzi huyo aliyetajwa kwa jina la Adolph Shayo, jina lake ni namba 1,023 katika orodha ya watumishi 9,932 iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Aprili 28.

Baada ya kupokea majina hayo kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Rais Magufuli aliagiza wote waliotajwa waondoke vituo vyao vya kazi kabla ya Mei 15 na watakaokaidi wafikishwe mahakamani, ambako wanaweza kukumbana na kifungo cha miaka saba.

Pengine sio ajabu kutajwa kwenye orodha hiyo kwa kuwa ukaguzi wa vyeti haukuacha mtu au cheo, lakini kugundulika kwake kunaibua maswali zaidi katika uhakiki huo ambao tayari umeshaonyesha dosari kama ya kutaja baadhi kuwa wana vyeti vya kughushi vya elimu ya sekondari wakati hawakuviwasilisha kwenye uhakiki uliofanyika.

Kutajwa kwa Shayo kunaweza kuibua utata mwingine wa usafi wa uhakiki kutokana na ukweli kuwa utakuwa umefanywa na mtu ambaye hakustahili kuhakiki wengine.

Shayo alijipatia sifa ya kuwa  mkali na msumbufu wakati wa uhakiki, akidaiwa kuwataka mara kwa mara watumishi wenzake kumpelekea vyeti.

Mmoja wa waliokaguliwa na Shayo, ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema walimu walipata shida wakati wa uhakiki kwa sababu walikuwa chini ya mhakiki huyo.

Alisema alishangazwa kusikia amekuwa mmoja wa watu waliotajwa kuwa na vyeti vya kughushi wakati yeye pia alihusika kuhakiki.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Nassib Mmbaga alisema baada ya ukaguzi kufanyika ilibainika kuwa vyeti vyake vilikuwa na matatizo (ambayo hakuyataja) na wakamtaka kuthibitisha, lakini hakufanya hivyo.

“Ni kweli alikuwa mtumishi katika idara ya elimu na msaidizi katika kitengo cha bohari ya manispaa, lakini lilipokuja suala la ukaguzi wa vyeti ilibidi afanye kazi kama msaidizi,” alisema.

“Hata kama ni mkaguzi ni lazima akaguliwe. Hata mimi (mkurugenzi) nilikaguliwa. Lakini tulivyokagua vyeti vyake (Shayo) tuligundua vina shida,” alisema.

Alisema pamoja na kupewa nafasi ya kuthibitisha uhalali wa vyeti vyake, alishindwa kufanya hivyo hadi majina yalipotangazwa.

Mkurugenzi huyo alisema hadi sasa amepokea zaidi ya barua 60 za rufaa, lakini hajaona jina la Shayo.

Sakata la vyeti feki limezidi kuchukua sura mpya baada ya baadhi ya waliotajwa kuamua kwenda vyama vya wafanyakazi kudai wameonewa.

Mmoja wa waliochukua hatua hiyo ni mratibu wa elimu wa Wilaya ya Chamwino, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, Charles Ulanga ambaye hajawahi kusoma elimu ya sekondari.

Ulanga anadai kuwa hakuwahi kuwasilisha vyeti vya sekondari wakati wa ukaguzi na hivyo anataka kujua wahakiki walivitoa wapi.

Katika Manispaa ya Temeke, jumla ya watumishi walioghushi vyeti ni 270, kati yao 120 wakitoka idara ya afya huku Hospitali ya Rufaa ya Temeke ikiongoza kwa kuwa na watumishi 53.

Pia, Shule ya Msingi ya Mbagala imetoa walimu saba.

Kuhusu athari za matokeo ya uhakiki huo, Mmbaga alisema zinazidi kujitokeza kutokana na kupunguza idadi ya watumishi katika hospitali na shule. “Tunajaribu kujaza nafasi za watoa huduma kutoka katika zahanati ambazo hazihudumii watu wengi ili huduma zisisimame,” alisema.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search