Wednesday, 31 May 2017

MKASA MAALUMU: SIKUJUA THAMANI YA MKE WANGU, NAJUTA AMEKUFA SABABU YA UJINGA WANGU.


Inasikitisha sana ilikua ni kawaida ya mume kupuuza maombi na mahitaji ya mkewe, aliyapuuza kutokana na kumdharau kumuona hana thamani tena, ameshazaa amejichokea, ule urembo na uzuri wake wa zamani umeyeyuka hakika sasa uzee unamnyemelea.
Mume alikua akitumia kila aina ya kejeli na dharau dhidi ya mkewe, hakika alimchoka, alisahau kuwa kuchoka kwa mkewe yeye ndio chanzo. Siku moja
Mume alirejea nyumbani na kukuta ujumbe juu ya meza umeandikwa.
"NIMEONDOKA WAANGALIE HAO WATOTO"
Ilikuwa jioni, alienda jikoni na kukuta kukavu, aliwaita watoto na kuwauliza "mama yenu yuko wapi"?
Wakasema walimuona Mama akiondoka na begi lakini hakuwaambia anaenda wapi.
Mume alichanganyikiwa, alijaribu kuchukua simu kumpigia lakini ilikuwa haipatikani, kabla hajafanya chochote mtoto wao wa mwaka mmoja alikuja akilia na kusema ana njaaa.
Ilibidi kuingia jikoni na kutaka kupika huku akitukana matusi yote, kila kitu kilikuwa hakuna, hapo ndipo alipokumbuka kuwa asubuhi mkewe alimuomba pesa ya kununua chakula akamuambia hana afanye maarifa yoyote anayoweza.
Akaendelea kufoka, "ataondokaje ghafla namna hii, huyu mwanamke mshenzi kabisa.."
Aliwaza lakini alikumbuka kuwa asubuhi hiyo hiyo, baada ya kumnyima mkewe pesa ya chakula mke alilalamika kuwa amechoka maisha yale na yeye akamjibu, "Kama umechoka si uondoke, wanawake wako wengi ukiondoa kitu na weka kitu..."
Akili yake iliwaza sana akakumbuka mchepuko wake, aliupigia simu uje nyumbani, lakini ulistuka kusikia kwamba eti Mama watoto, ameondoka na kamuachia watoto wote wa nne.
Mchepuko ulijifanya hausikii vizuri na baada ya muda ukazima simu.
Sasa alikuwa amechanganyikiwa, alitaka kupiga simu Kijijini ndipo alikumbuka kuwa hata namba ya Mama mkwe wake alikuwa hana, hakuwa na kawaida ya kuongea nao. na mara chache alipoongea ni pale ambapo mkewe alipiga simu na kumuambia kuwa aongee na familia.
Alikumbuka ana namba ya rafiki wa mke wake, akampigia kumuuliza mkewe yuko wapi akasema hajui lakini mara ya mwisho alipompigia alimuambia kuwa "ANAENDA KUPUMZIKA".
Alizidi tena kutukana, alitoka jikoni nakuwachukua watoto kwenda kwenye mgahawa alizunguka nao mpaka kupata sehemu ya kula, watoto walifurahi sana siku hiyo kutoka na Baba yao, waliongea na kucheka kula nje ya nyumbani, kidogo alipata faraja na kutabasmau lakini bado alikuwa akiwaza kuhusu mkewe.
Baada ya kumaliza chakula aliwarudisha watoto nyumbani alitaka kwenda kuwalaza lakini walikataa na kutaka kuogeshwa.
Kimbembe kilianza katika kuwaogesha wale wadogo. Walihtaji kuoga kwa maji ya moto, alienda moja kwa moja kuwasha jiko la umeme akakuta haliwaki.
Akaanza kutukana ndipo alipokumbuka miezi mitatu iliyopita liliharibika na mkewe alipomuambia alisema watumie mkaa, akaenda kwenye jiko la gesi, hata hakuwasha kwani alikumbuka kuwa siku tatu zilizopita mkewe alimuomba hela ya gesi akamtukana
"Mwanamke gani mvivu kuwasha mkaa, unatumia tu hela wakati huna chakufanya, Pumbavu!"
Alichanganyikiwa zaidi, akaenda kuwalaza watoto kwa lazima ile na yeye anapanda kitandani mtoto mdogo akaanza kulia kwa sauti ya juu, joto, alitaka kuoga, ilibidi kunyanyuka kutaka kuwasha mkaa, atauwashaje hata mafuta ya taa hajui yako wapi labda angeweka ili uwake.
Ilibidi kunyanyuka kuwasha TV watoto waliangalia mpaka walipopitiwa na usingizi, hata hakuwanyanyua yeye na watoto walilala, pale pale kwenye kochi mpaka asubuhi.
Wote walipitiwa, asubuhi alistuka amechelewa kazini na watoto walitakiwa kuandaliwa kwaajili ya shule.
********
Kichwa kilizidi kumuuma, hakujua aanzie wapi aishie wapi, akanunue vitafunwa au apike chai lakini atapika na nini? Akawaambia siku hiyo hakuna kwenda shule, akawasha gari kwenda kununua gesi na vitu vya nyumbani. Bado mkewe alikuwa hapatikani.
Alinunua jiko na kuja kupika chai akawapa watoto, akaanza kumtumia meseji mkewe za kumuomba msamaha, kumuomba arejee nyumbani kwani peke yake asingeweza kuwalea watoto lakini meseji hasikupokelewa.
Simu ilianza kuita, ilikuwa namba ya bosi wake, alikuwa akimhitaji kupeleka taarifa ofisini, aliamua kumtafuta mdogo wake aje akae na wanae lakini naye alikuwa bize na kazi zake. Ili bidi kuwaacha watoto nyumbani na kwenda ofisini hivyo hivyo.
Alifika ofisini na kukabidhi taarifa, baada ya muda meseji simu ilipiga kelele kuashiria kuwa meseji alizomtumia mkewe ziliingia, simu ilikuwa imewashwa.
Harakaharaka alinyanyua simu na kupiga, ilipopokelewa alianza kuomba msamaha aliongea maneno mengi ya kujilaumu na kumtaka mkewe kurejea nyumbani.
"Wewe ndiyo mume wake?" Upande wapili uliuliza.
"Ndiyo! Ndiyo Mimi! Kuna nini kimetokea! Mke wangu kafanya nini na yuko wapi?"
Aliuliza maswali mfululizo lakini kwa utaratibu upande wapili ulisikika unasema
"Mimi ni nesi nipo Hospital......... mwenye hii simu ame..."
Hakusubiri wala amalizie alianza kupiga kelele kulia kwa uchungu, nguvu zilimuishia na kukaa juu ya kochi la mapokezi. Wafanyakazi wenzake walimsogelea kutaka kujua ni nini, bado alikuwa ameshikilia simu, walichukua na kuongea na mtu wa upande wa pili.
Baada ya muda alisikia wakimuambia, "Unalia nini sasa yaani baada ya ufurahi unalia, Hongera mke wako ana uchungu tunaomba kama upo karibu tunahitaji vifaa tafadhari ufanye haraka kwa sababu pia dalili zinaonyesha anaweza kupasuliwa ana matatizo kwenye moyo wake ni muhimu tukaokoa uhai wake na mtoto".
Hapo ndipo alipokumbuka kuwa mke wake alikuwa mjamzito.
Alikuwa akimuona kila siku lakini kwakuwa alikua hajali hata alikuwa hajui kuwa ujauzito wa mkewe ulikuwa na muda gani.
Akili yake ilishatekwa na mchepuko kiasi cha kuisahau familia yake. Aliendelea kulia kwa uchungu uliokuwa umechanganyika na furaha, alifurahia kuwa mkewe yuko salama lakini alipata uchungu kwa ukatili wake kiasi kwamba amesahau hata kuwa mkewe alikuwa amekaribia kujifungua.
Haraka haraka aliingia kwenye gari,akatafuta mipira {gloves}karatasi, beseni pamoja na vitu vingine kama baby show, akaenda hospitallini kumuomba mkewe msamaha,. watu walishangaa kumuona amepiga magoti analia kama mtoto mdogo.
Mkewe alimuambia nilishakusamehe muda mrefu, naamini sasa unafahamu thamani ya familia.
Alinyanyuka na kukubali kweli sasa anafahamu maana ya familia, siku ile amejifunza mengi kuliko mambo aliyokuwa amejifunza kwa maisha yake yote.
Baada ya kuruhusiwa kusalimiana na mkewe ndani ya wodi ya wazazi ilibidi awapishe madaktari ili wamhudumie mkewe huduma ya mwisho ili wamruhusu arudi na mmewe nyumbani.
Na baada ya kama dakika 30 kumbe mke alikuwa kashaaga dunia kwa sababu zilizokuwa nje ya madaktari ila walifanikiwa kuokoa uhai wa mtoto, kwa kweli ilikuwa siku ngumu sana kwa mume haielezeki.
.................................................................................
Sikiliza niseme na wanaume jambo;
Ukiumwa hutarudi kwa Mama yako, ukiumwa hutaenda kwa dada zako, hutarudi kwa ndugu zako au ule mchepuko ambao kila siku unajitahidi kuupelekea vijizawadi zawadi wakati mkeo hujui hata chupi anavaa saizi gani.
Utarudi kwa yule yule mwanamke unayemnyanyasa, unayemtesa na kumdhalilisha, unayemuona si kitu kwako.
Utamrudia Mungu na kusingizia ushenzi wako kwa shetani na yeye mkeo kwakuwa anajua maana ya ndoa basi atakupokea na kukuhudumia, atakupikia, atahakikisha unakunywa dawa, atakusafisha kama hujiwezi na ndiye atakuwa nesi wako.
Uanaume wote na ubabe wote wa kijinga uliokuwa ukiufanya utaisha ukiwa huwezi kunyanyuka.
Marafiki watakuja kukusalimia na kuishia kusema pole, wataleta matunda tu kana kwamba matunda yatakupeleka chooni, yatakufulia nguo, yatakupikia au kukuuguza.
Hebu badilika, wakati mwanamke atakufanyia yote hayo yeye akiumwa basi utamtafutia mfanyakazi, utamuambia mdogo wake aje kutoka kijijini kumhudumia, utamuita Mama mkwe aje kumhudumia au hata kumpeleka kwao akahudumiwe.
Utaendelea bado kuchepuka na hata wakati mwingine utasahau kuwa mkeo ni mgonjwa.
Utakuwa ni mtu wa kutoa pesa tu na kuleta matunda kama wale rafiki zako.
Lakini bado atapona na kuendelea kukupenda kama zamani na atasahau na kuona kama ni kawaida.
Mpende huyo mwanamke uliyenaye, muonyeshe mapenzi ya kweli kwani hao unaodhani wanakupenda,watakugeuka, ukishikwa tu na malaria.na yeye atakuwa yupo kwajiri yako wakati wowote.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search