Monday, 15 May 2017

MO ATAKA ARUDISHIWE PESA ZAKE NA SIMBA BAADA YA KLABU HIYO KUINGIA MKATABA NA SPORT PESA

Baada ya taarifa kusambaa kuwa Mohammed Dewji maarufu kwa jina la ‘MO’ amefuta mpango wake wa kuendelea kuwekeza kwenye Klabu ya Simba, mdau huyo ametoa kauli.
Imefahamika kuwa Mo ambaye ni mdau mkubwa wa timu hiyo ametaka alipwe shilingi bilioni 1.4 za Tanzania kutokana na viongozi wa Simba kukiuka makubaliano ikiwa ni muda mfupi baada ya Simba kusaini mkataba wa udhamini na Kampuni ya SportPesa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mo ameandika haya: “It's sad that the SIMBA leadership has signed a long term sponsorship deal without consulting with me. I have put my blood for the club.”

Kauli hiyo inamaanisha kuwa amesikitishwa na uongozi wa Simba kwa kusaini mkataba wa muda mrefu bila kumshirikisha yeye wakati amekuwa mdau mkubwa wa klabu hiyo na kujitolea mambo mengi.

Mei 12, 2017, uongozi wa Simba ukiongozwa na rais wa klabu, Evans Aveva ulisaini mkataba wa miaka mitano na Kampuni ya SportPesa wenye thamani ya Sh 4.9 bilioni.

MO anataka kulipwa fedha zote za mishahara alizokuwa akiwalipa wachezaji wa Simba tangu mwaka jana baada ya kubaini kuwa Simba imeingia mkataba na Kampuni ya SportPesa bila kumshirikisha.

Kuibuka kwa taarifa hiyo kumesababisha kuwe na mitazamo tofauti katika mitandao ya kijamii na makundi ya mitandao hayo ambapo wanachama na mashabiki wa Simba wamekuwa wakitofautiana mitazamo, wapo wanaoona uongozi haukutenda haki na wapo wanaoona hakuna tatizo.

Awali kabla ya mkataba huo, Simba ilishaanza mchakato wa marekebisho ya katiba yao ili kuruhusu kipengele cha uwekezaji kwa mfumo wa hisa kama lilivyokua ombi la MO kuwekeza katika klabu hiyo kwa asilimia 51 za hisa huku wanachama wakibaki na asilimia 49.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search