Monday, 15 May 2017

MWANAMKE AJIOA MWENYEWE NCHINI TAIWANI

Mwanadada May Chen, kutoka nchini Taiwan, amefanya tukio la aina yake mara baada ya kuamua kufunga ndoa ya mtu mmoja (kujioa mwenyewe) kwa kuwa amesubiri muda mrefu bila ya kupata mchumba.
Mwanamke huyo aliyekuwa na ndoto za kuolewa alikuwa akiwaza namna ambavyo siku ya harusi yake itakavyokuwa, pamoja na matukio yote ya upigaji wa picha akiwa na mwenza wake siku yao ya harusi.
Ndoto zake zilizimika ghafla baada ya kuathiriwa na ugonjwa wa saratani ya matiti mwaka 2013 ambapo ilimlazimu kukaa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Baada ya muda mrefu wa matibabu, ndoto zake ziliamshwa tena baada ya kuambiwa kuwa amepona ugonjwa ule wa saratani ya matiti uliokuwa ukimsumbua.
Miaka miwili baadae, matumaini yake yalizimika baada ya kugundulika kuwa ugonjwa ule umemrudia kwa mara nyingine na kumfanya kuwa na hali mbaya zaidi kiafya.
“Nilipokuwa mdogo, nilipenda sana mavazi, na nilikuwa nina imani kuwa siku moja nitapiga picha nikiwa nimevaa gauni la harusi. Hivyo nilingoja… Lakini nilikuwa mgonjwa na hili ndilo jambo nililoona ni vyema kulifanya,”Alisema Chen.
Kutokana na hali ya ugonjwa alio nao Chen, ndipo alipoamua kufunga ndoa ya peke yake, ili tu atimize ndoto yake aliyokuwa nayo muda mrefu ya kuolewa pamoja na kupiga picha za harusi (photo shoot).
Chen aliongeza kuwa, baadaye mwaka huu atasafiri yeye pamoja na mama yake kwenda Bali (kisiwa kilichopo nchini Indonesia) kwa ajili ya kula fungate (honeymoon).
“Sikutambua kuwa saratani hii ilikuwa inanisubiri. Lakini nitatumia muda mfupi nilionao kufanya mambo yanayonifurahisha,” alisema.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search