Thursday, 4 May 2017

NCHI KUMI BORA KIUCHUMI DUNIANI 2017.


1. MAREKANI
Marekani ndilo Taifa linaloongoza kiuchumi duniani kwa kigezo cha pato la jumla la ndani. Inamiliki dollar trilioni 18 sawa na asilimia 24.5 ya pato lote la dunia. Marekani kama taifa lenye nguvu kiuchumi, imepiga hatua kubwa katika Nyanja ya kiteknolojia na miundombinu na taifa hili lina hifadhi kubwa ya rasilimali.
2. CHINA
China ni nchi ambayo imeweza kufanya mageuzi makubwa kiuchumi tangu miaka ya 1970 hadi kufikia kuwa na uchumi wa viwanda na kuwa wauzaji wakuu wa bidhaa nje kwa miaka mingi sasa. Viwanda na utoaji wa huduma umechangia kukuza uchumi wa Wachina kwa karibu asilimia 45 kila kimoja huku asilimia 10 ikiwa ni pato kutoka sekta ya kilimo. China inashika nafasi ya pili kiuchumi duniani ikiwa na pato la dollar trilioni 11.
3. JAPANI
Japan ni taifa la tatu kiuchumi duniani, likiwa linamiliki pato lenye thamani ya dollar trilioni 4.4 za kimarekani. Hata hivyo uchumi wa Japani ulipata misukosuko tangu mwaka 2008, kulipotokea dalili za mdororo wa kiuchumi ingawa serikali iliweka nguvu kubwa kuunusuru kabla tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2011 kuweka ufa mwingine. Katika siku za karibuni Japani imejikwamua na kuweza kujongea kufika hapa ilipo.
4.UJERUMANI
Taifa la nne kwa uchumi duniani ni Ujerumani. Wao wanamiliki pato la jumla la ndani lenye thamani ya dollar trilioni 3.3 za kimarekani. Wajerumani ni watengenezaji na wasafirishaji wakubwa wa mashine za viwandani, magari, vifaa vya majumbani na madawa.
5. UINGEREZA
Uingereza inamiliki pato la jumla la ndani lenye thamani ya dollar trilioni 2.9 na hivyo kuwa katika nafasi ya tano kwa uchumi mkubwa duniani. Sekta ya huduma inachangia wastani wa asilimia 75 ya pato la nchi, kilimo asilimia moja tu, viwanda ni sekta ya pili kwa mchango wa uchumi wa Uingereza. Ingawa kilimo hakina mchango mkubwa kwa pato la nchi, bado Uingereza inazalisha zaidi ya 60 ya chakula kinachotumika nchini hapo.
6. UFARANSA
Inamiliki pato la jumla la ndani lenye thamani ya dollar trilioni 2.4 za kimarekani. Ufaransa ni taifa linaloongoza kupokea idadi kubwa ya watalii kutoka kote duniani. Taifa hili lina kiwango kidogo sana cha umasikini miongoni mwa raia wake na ambao wana kiwango kizuri cha maisha kwa wastani ukilinganisha na nchi nyingine. Pia Ufaransa ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uuzaji mkubwa wa bidhaa nje ya nchi.
7.INDIA
India ni taifa la saba katika mataifa yenye uchumi mkubwa. India inamiliki dollar trilioni 2 pato la jumla la ndani. Uchumi wa taifa hili unategemea kilimo kwa asilimia 17, sekta ya huduma asilimia 57 na viwanda asilimia 26.
8. ITALIA
Italia ni Taifa la nane kiuchumi, wakiwa wana pato la jumla la ndani lenye thamani ya dollar 1.8 za kimarekani. Italia ni miongoni mwa wazalishaji wakuu kwenye ukanda wa nchi za Euro. Tatizo kubwa linaloikumba Italia ni ukosefu wa ajira pamoja na deni la taifa.
9. BRAZILI
Brazili ni taifa la tisa kwa uchumi mkubwa. Taifa hili linamiliki uchumi wa dollar trilioni 1.8 kwa pato la jumla la ndani. Sekta ya huduma inachangia asilimia 68, asilimia 26 viwanda na kilimo ni kinachangia kwa asilimia sita. Pamoja na kuwa na pato kubwa la ndani, bado wananchi wa Brazili wengi wana vipato vya hali ya chini.
10. CANADA
Canada ni taifa la kumi kiuchumi.Canada imepanda na kushika nafasi baada ya kuipiku na kuiondoa Urusi kwenye hii orodha ya kumi bora. Taifa hili linamiliki pato la ndani la thamani ya dollar trilioni 1.5.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search