Wednesday, 17 May 2017

POLISI MWENYE CHEO CHA OCD AUAWA KIKATILI

IGP ERNEST MANGU.

MKUU wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Uvinza mkoani Kigoma, Amedeusi Malenge, ameuawa na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa polisi, imeelezwa, alikuwa likizo jijini akitokea Kigoma na alipatwa na umauti saa tatu usiku juzi, baada ya kupigwa na kitu kizito na watu wasiojulikana, alipokuwa anatoka katika matembezi.

Habari za kuaminika zinasema Malenge ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) ya Kibaha kabla yakuhamishiwa Uvinza, alikutana na watu ambao walikuwa wamewateka walinzi wa nyumba yake iliyoko Kinyerezi wakati akirudi kutoka katika matembezi, ambao walimuua.

“Taarifa za awali tulizopata ni kwamba alikuwa anatoka kula maana pale anapoishi haishi na mke,” alisema mmoja wa mtu aliyewahi kufanya kazi na marehemu.

"Ndipo alipokuwa anarudi akawakuta walinzi wake wametekwa nje karibu na nyumbani kwake, akasimamisha gari na kushusha kioo na kuuliza kulikoni.

"Wakati anauliza wale watu walimvamia katika gari lake na kumpiga kichwani na kitu kizito ambapo alifariki papo hapo."

MICHANGO ‘SEND OFF’
Habari zaidi zilidai Malenge alifanya sherehe ya kumuaga nyumbani binti yake aliyekuwa aolewe (sendoff) wiki iliyopita katika ukumbi wa Msimbazi Center, jijini Dar es Saalam.

“Kifo hiki, kweli tutaonana baadaye, wala siamini," alisema Masoud Juma ambaye ni mkazi wa Kibaha. "Tulimpa michango ya ‘sendoff’ ya binti yake juzi tu hapa tukanywa (pombe) naye, eti leo kafariki!

"Kweli inauma.

"Alikuwa mtu mwenye uhusiano mzuri kazini na hata jamii ya wana Kibaha... tulimpenda, lakini ndio hivyo hatuna jinsi."

Nipashe ilifika eneo la tukio Kinyerezi jana na kuzungumza na mmoja wa majeruhi ambaye ni jirani wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina moja la Urio.

Alisema juzi majira ya saa 5 usiku akiwa amelala aliamshwa na mlinzi wa nyumba iliyo jirani na marehemu akimtaarifu kuwa wamevamiwa.

Alisema baada ya kuchungulia dirishani aliona gari la marehemu likiwa jirani na nyumba yake na ndipo alipotoka nje kutaka kujua kinachoendelea.

Alisema alipotoka hakumwona mlinzi aliyemuita, lakini alikutana na kijana mwingine mrefu asiyemfahamu ambaye alikuwa ameshika shoka.

Alisema kijana huyo alianza kumshambulia kwa shoka na kumjeruhi eneo la kisogoni.

“Nilijitetea kwa kumwambia jirani yangu (marehemu) nimetoka kukusaidia halafu vijana wako wananipiga," alisema lakini "kabla sijaendelea kuongea nikajikuta nimepigwa na nondo shingoni na kudondoka chini."

"Ndipo nikatambaa mpaka nyuma ya choo kwenye kichaka, nilikaa kwa zaidi ya dakika kadhaa ndipo nikainuka na kukimbilia ndani kwangu.”

Imeandikwa na Margaret Malisa, KIBAHA na Romana Malya

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search