Tuesday, 9 May 2017

Rais Magufuli Amegawa Magari ya kubebea wagonjwa kwa wabunge Watatu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa magari mapya matatu ya kubebea wagonjwa kwa Wabunge watatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yao ya ubunge.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amekabidhi magari hayo aina ya Land Cruiser Hardtop kwa niaba ya Rais Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mkoa wa Rukwa Mhe. Ally Keissy, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa waTabora Mhe. Munde Tambwe na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Lucy Mayenga.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Balozi Kijazi amesema Mhe. Rais Magufuli ametoa magari hayo baada ya kuguswa na kilio cha muda mrefu cha Wabunge hao waliokuwa wakiomba wananchi wao wapatiwe magari ya wagonjwa.

“Mhe. Rais ameamua kuwakabidhi nyinyi haya magari kutokana na vilio vyenu ambavyo amekuwa akivisikia mara kwa mara, Mhe. Keissy umekuwa hata ukitafuta miadi ya kuja kumuona Mhe. Rais kwa suala hili, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyazungumza haya kwa muda mrefu.

“Tunafahamu kila Mbunge katika jimbo lake anahitaji kupata huduma kama hii, na huduma kama hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa hiyo sisi Serikali kila tunapopata uwezo basi tunasaidia pale tunapoweza kufikia kwa wakati ule, tulishatoa magari mengine matatu kama haya Chalinze na vituo vingine vya Morogoro.”Amesema Balozi Kijazi

Balozi Kijazi amewapongeza Wabunge hao kwa kupata magari hayo kwa ajili ya wananchi wao na amewasihi kuhakikisha yanatunzwa vizuri ili yadumu muda mrefu na yawahudumie wananchi wote bila kujali dini, kabila, itikadi zao za kisiasa wala makundi.

Kwa upande wao Mhe. Ally Keissy, Mhe. Munde Tambwe na Mhe. Lucy Mayenga wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuitikia kilio chao cha kuwasaidia wananchi magari ya kubebea wagonjwa, na wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuwapigania Watanzania wote hasa wenye shida na pia kwa juhudi kubwa za kuleta maendeleo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Mei, 2017
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi (kati) akiwa na Katibu Mkuu Ikulu Mhe. Alphayo Kidata (Kushoto) na Mkurugenzi wa Huduma Ikulu  Bw. Charles Mwankupili (kulia) na  Wabunge Mhe Ali Mohamed Kessy (mbunge wa Nkasi Kaskazini)  Mhe. Munde tambwe na Mhe Lucy Mayenga (wabunge viti maalumu)  baada ya kuwakabidhi magari la kubebea wagonjwa waliyopewa msaada na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam leo Mei 9, 2017

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search