Thursday, 11 May 2017

Taarifa kwa Umma: ACT Wazalendo Wafanya Mabadiliko ya Uongozi


Zitto Kabwe 2011.jpg
Katika kikao chake cha pili kwa mwaka 2017 kilichofanyika tarehe 07 Mei 2017 Mjini Kahama, Kamati Kuu ya Chama iliazimia kwa kauli moja kumsimamisha nafasi yake ya uongozi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, ndugu Ramadhan Ramadhan.
Kabla ya hatua hii Ndugu Ramadhan aliwahi kukutwa na makosa mbalimbali na Kamati ya Chama ya Uadilifu ambapo Kamati Kuu ilimpa adhabu ya onyo kali na kumtaka kutorudia makosa yake tena.
Makosa ambayo Ndugu Ramadhan Ramadhan alikutwa nayo ni pamoja na:
I) Kupingana na msimamo rasmi wa Chama wa kutoutambua na kutoshiriki kwenye uchaguzi batili wa marudio wa Zanzibar uliofanyika Machi 20, 2016
II) Kutangaza kupitia vyombo vya habari kuwa Chama cha ACT kinamtambua na kumuunga mkono Ndugu Mohamed Shein kinyume na matamko rasmi ya Chama
III) Kusababisha mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa Chama kutoka Zanzibar na kuhujumu ustawi wa Chama kwa upande wa Zanzibar kutokana na matamko yake mbalimbali
Kutokana na kukaidi adhabu yake ya onyo kali na kuendelea na matamko aliyokatazwa, Kamati Kuu ya Chama imeamua kumsimamisha nafasi yake ya Makamo Mwenyekiti Zanzibar, ndugu Ramadhan Ramadhan hadi hapo suala lake litapoamuliwa na Halmashauri Kuu.
Kutokana na kusimamishwa kwa ndugu Ramadhan Ramadhan, Kamati Kuu imemteua ndugu Juma Sanani aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar/Kaimu Katibu Mkuu kuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chama kwa upande wa Zanzibar. Ndugu Hamad Yusufu ameteuliwa kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zanzibar kuchukua nafasi ya Ndugu Juma Sanani.
Pia, Kamati Kuu imemuidhinisha Ndugu Dorothy Semu kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Chama kushika nafasi iliyoachwa wazi baada ya ndugu Sanani kumaliza kipindi chake cha mwaka mmoja wa kukaimu nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba ya ACT Wazalendo. Ndugu Dorothy Semu atashika nafasi hiyo hadi uchaguzi wa nafasi hiyo utapofanyika Mwezi Machi 2018. Kabla ya uteuzi huu Ndugu Dorothy Semu alikuwa Katibu wa Kamati ya Sera na Utafiti.
Pamoja na salamu za Chama, ACT Wazalendo, Taifa kwanza leo na kesho.
Abdallah Khamis,
Afisa Habari - ACT Wazalendo
Dar es salaam
Mei 10, 2017

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search