Friday, 12 May 2017

Ziara ya Jacob Zuma Tanzania: Mikataba 3 yasainiwa, aombwa Mkopo wa reli, Walimu Kufundisha A.Kusini

ZIARA YA RAIS ZUMA : Mapokezi ya Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alipowasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Tanzania John Magufuli akiwa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma katika ikulu Dar es Salaam. Rais Zuma yupo nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
[​IMG]

Tanzania na Afrika Kusini zimesaini leo hati za makubaliano ya ushirikiano katika sekta za Wanyamapori, Uhifadhi na Uchukuzi.

Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika ya Kusini zasaini mikataba mitatu ya ushirikiano katika sekta mbalimbali zitakazosaidia kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.

Hati za mikataba hiyo zimesainiwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Marais wawili Dkt. John Magufuli na Jacob Zuma na waandishi wa habari.

Mikataba iliyosainiwa baina ya nchi hizo mbili ni hati ya muhtasari wa makubaliano ya mkutano wa tume ya pamoja ya Marais kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika Kusini uliolenga kuboresha makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mkutano huo.

Hati ya makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Bi Anuwai kati ya Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini, inayolenga kuboresha ushirikiano katika sekta ya wanyamapori na uhifadhi.

Huku hati nyingine ikiwa ni makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi kati ya Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini uliolenga kuboresha ushirikiano katika sekta ya uchukuzi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Rais Magufuli alisema ziara ya Rais Zuma imekwenda sambamba na mkutano wa kwanza wa tume ya Marais ambapo ulibainisha baadhi ya maeneo ya makubaliano.

Rais Magufuli alisema kuwa maeneo ya makubaliano hayo yalilenga kuimarisha na kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili na njia za kundoa vikwazo vinavyokwamisha biashara baina yao.

“Hali ya biashara ya Afrika Kusini nchini kwa mwaka 2016 ni takribani Tsh Trilion 2.4 na uwekezaji wake ni Dola za Kimarekani 803.15 milioni iliyopelekea kupatikana kwa ajira kwa watanzania 20,916”alisema Rais Magufuli

Rais Magufuli alitaja maeneo mengine ya makubaliano kuwa ni kushirikiana katika sekta ya viwanda ambapo amewakaribisha wafanyabiashara kutoka nchini Afrika Kusini ili kuwekeza katika kujenga viwanda vya kusindika mazao na hivyo kukuza uchumi.

Kwa upande wa Sekta ya miundombinu na nishati wamelenga katika kuimarisha reli ya kati na upatikanaji wa umeme, ambapo Rais Dkt.Magufuli amemwomba Rais Zuma kutumia ushawishi wake katika Umoja wa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi (BRICS) ili kuisaidia Tanzania kupata mkopo kwa gharama nafuu, kwa lengo la kuendeleza ujenzi wa miradi ya reli ya kati na umeme.

Vilevile, Marais hao wamekubaliana kubadilishana uzoefu na wataalamu kupitia sekta ya utalii ikiwemo kuwakiribisha wawekezaji kutoka nchi ya Afrika Kusini kuwekeza kwa kujenga hoteli za kitalii pembezoni mwa fukwe za bahari ya Hindi.

Maeneo mengine ya makubaliano ni pamoja na sekta za madini kwa kubadilishana uzoefu na utaalamu, afya kwa kuwakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa, elimu, sayansi na teknolojia ambapo Rais Zuma amekubali kupokea wataalamu wa lugha ya kiswahili watakaofundisha Afrika Kusini.

Rais Zuma alisema wataendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na kukuza umoja wa Afrika ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyokabili bara hilo.

“Tumefurahi kusaini mikataba hiyo leo, pamoja na kupata taarifa ya mawaziri iliyojitosheleza katika kuainisha maeneo ya ushirikiano na utekelezaji wake itakayosaidia kuleta maendeleo katika nchi hizi mbili” alisema Rais Zuma

Rais Jacob Zuma anakamilisha ziara yake ya siku mbili leo usiku iliyolenga katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, ikiwa ni pamoja na kuanisha maeneo mapya ya ushirikiano yatakayochochea maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Gedleyihlekisa Zuma amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ameahidi kuunga mkono ujenzi huo.

Mhe. Rais Zuma ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo rasmi na alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini kupitia vyombo vya habari Ikulu Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni katika ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku mbili hapa nchini kwa mwaliko wa Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Zuma amesema anatambua kuwa ujenzi wa reli ya kati utaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi za maziwa makuu na hivyo amekubali ombi la Mhe. Rais Magufuli la kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika ya Kusini kushirikiana na Tanzania kufanikisha mradi huo mkubwa.

Wakiwa katika Mazungumzo rasmi viongozi hao wamezindua rasmi Tume ya Pamoja ya Marais (Bi-National Commission-BNC) kwa kufanya kikao cha kwanza cha tume hiyo tangu ianzishwe mwaka 2011 ambapo wamepokea makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha tume ngazi ya mawaziri.

Kabla ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Zuma wameshuhudia utiaji saini wa hati tatu za ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini ambazo ni Muhtasari wa makubaliano ya mkutano wa tume ya pamoja ya Marais, Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya bioanuwai na uhifadhi na makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi.

Akizungumzia makubaliano na mazungumzo yao Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Zuma kwa kuitikia mwaliko wake na kukubali kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano na uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania hususani kuwahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, ujenzi wa miundombinu, utalii, madini na afya kwa kutumia uwezo mkubwa uliopo Afrika Kusini.

Mhe. Rais Magufuli amesema hivi sasa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini kwa mwaka ni Shilingi Trilioni 2.4, uwekezaji wa Afrika Kusini hapa nchini ni Dola za Marekani Milioni 803.15 uliozalisha ajira 20,916 na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi endapo ushirikiano utaimarishwa zaidi.

“Na ili tufanikiwe kukuza biashara tumekubaliana kuondoa vikwazo na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi zetu mbili kutumia fursa ya uhusiano na ushirikiano mzuri wa kirafiki na kidugu uliopo kati ya nchi zetu kufanya kazi pamoja” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Dkt. Magufuli ameongeza kuwa Tanzania itapeleka walimu wa lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na watu takribani milioni 120 ili wakafundishe lugha hiyo katika vyuo vya Afrika ya Kusini na hivyo kuimarisha zaidi ushirikiano.
Kwa upande wake Mhe. Rais Zuma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amesema nchi yake itahakikisha makubaliano yote ya Tume ya Pamoja ya Marais yanatiliwa mkazo na kutekelezwa kwa kuzingatia muda uliopangwa.

Mhe. Rais Zuma amesema Afrika Kusini inatambua na kuheshimu mchango wa mkubwa wa Tanzania kwa ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Afrika Kusini ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere alishirikiana na Waasisi wa Taifa hilo walioongozwa na Hayati Mzee Nelson Mandela kupigania ukombozi na uhuru na kwamba anafurahi kuona Tanzania bado inatoa mchango mkubwa kupigania amani katika bara la Afrika.

“Mhe. Rais Magufuli naomba nikuhakikishie kuwa Afrika Kusini itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na ndugu na marafiki zake Tanzania katika kujenga uchumi kwa manufaa ya wananchi na pia kupigania amani kwa kuwa bila amani na usalama hakuna maendeleo” amesema Mhe. Rais Zuma.

Pamoja na kufanya mazungumzo rasmi, viongozi hawa watashiriki mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini (Business Forum) unaofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere na jioni Mhe. Rais Zuma atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam kabla ya kurejea Afrika Kusini baadaye leo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Mei, 2017

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search