Thursday, 1 June 2017

Akaunti za aliyekuwa Rais wa Gambia Yahya Jammeh Zafungwa, Waziri wa Serikali Mpya Adai Alikwapua Dola Milioni 50


WAZIRI wa Sheria wa Gambia, Abubacarr Tambadou, amesema kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Yahya Jammeh, ameiba kiasi cha dola za Marekani milioni 50 kutoka katika kampuni ya mawasiliano ya taifa hilo na tayari mahakama imetoa amri ya kutaifisha mali zake.

“Rais Yahya Jammeh yeye binafsi au kwa kutoa maelekezo mahsusi amekwapua dola za Marekani zisizopungua milioni 50,” anasema waziri huyo na kuongeza; “..Jumatatu (Novemba 22, 2017) tumepata amri ya mahakama kuhusu kutaifisha mali zake au kuzizuia.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, hii ni mara ya kwanza kwa serikali mpya ya taifa hilo kutoa maelezo rasmi kuhusu wizi alioufanya rais huyo wa zamani aliyeongoza taifa hilo kwa miaka takriban 22 mfululizo.

Waziri Tambadou aliwaeleza waandishi wa habari kwamba mahakama ya nchi hiyo imeamuru kufungwa kwa akaunti takriban 88 zenye jina la Jammeh katika benki mbalimbali, sambamba na ‘kuzishikilia’ kampuni 14 zinazohusishwa na mkuu huyo wa nchi wa zamani.

Yahya Abdul-Aziz Jemus Junkung Jammeh alizaliwa Mei 25 mwaka 1965, ni mwanasiasa aliyetokea katika jeshi na alianza kuiongoza Gambia kuanzia mwaka 1994 hadi 2017, akiwa mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Kijeshi (AFPRC)  na baadaye kuwa rais wa nchi hiyo kuanzia 1996 hadi 2017

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search