Monday, 19 June 2017

CHAMA CHA ACT-WAZALENDO CHALAANI POLISI KUPIGA WALEMAVU

Chama cha ACT Wazalendo kimelaani vikali hatua za jeshi la polisi nchini kutumia nguvu kuwatawanya watu wenye ulemavu ambao walikuwa wameandamana Ijumaa katika barabara ya Sokoine, Posta Jijini Dar es salaam ili kwenda kumuona Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.

Walemavu hao walikuwa wamefanya maamuzi hayo ili kukutana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kwa lengo la kuwasilisha malalamiko yao kutokana na watu hao kukamatwa na kuzuiliwa kuingia mjini.

"Chama cha ACT Wazalendo kinalaani vikali na kwa nguvu zote kitendo cha jeshi la polisi kutumia mabomu ya machozi na virungu dhidi ya watu wenye ulemavu wasio na silaha yoyote. Katika tukio husika lililotokea Juni 16, 2017 jijini Dar es salaam, askari wa jeshi la polisi waliwavamia, kuwapiga, kuwaswaga na kuwaburuza watu wenye ulemavu kwa kisingizio kuwa hiyo ilikuwa njia ya kurahisisha kukamatwa na kutawanywa kwao" Alisema Ado Shaibu

Chama Cha ACT kinasema kuwa wao wanaamini kuwa jeshi la polisi lingeweza kuwakamata au kuwatawanya walemavu pasipo kutumia nguvu yoyote zile kwa kuwa watu hao hawakuwa na silaha zozote zile, ACT wanasema kitendo hiki cha polisi hakivumiliki hata kidogo.

"ACT Wazalendo tunaamini kwa dhati kabisa kuwa jeshi la polisi lingeweza kuwakamata na kuwazuia watu hao wenye ulemavu, ambao hawakuwa na silaha yoyote, bila kutumia nguvu kubwa kama walivyofanya. Pia, badala ya kuwatawanya na kuwakamata, jeshi la polisi lingeweza kuwaongoza walemavu hao hadi Manispaa ya Ilala walikotaka kwenda kuwasilisha kilio chao. Vitendo hivi vya polisi kutumia mabavu na nguvu kubwa hata kwenye mazingira ambayo njia nyingine zingeweza kutumika havivumiliki hata kidogo" alisisitiza Ado Shaibu

Mbali na hilo ACT Wazalendo wamemtaka Waziri mwenye dhamana ya jeshi la polisi kuomba radhi kwa Jumuiya ya watu wenye ulemavu huku Waziri mwenye dhamana ya watu wenye ulemavu wakimtaka kuhakikisha kuwa madai ya walemavu yanafanyiwa kazi.

"ACT Wazalendo tunamtaka Waziri mwenye dhamana ya jeshi la polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani, ndugu Mwigulu Nchemba kuiomba radhi jumuiya ya watu wenye ulemavu hapa nchini kwa kitendo cha jeshi la polisi na kuhakikisha vitendo kama hivi havirudiwi tena. Pia tunamtaka Waziri mwenye dhamana ya watu wenye ulemavu, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Ndugu Jenister Mhagama kuhakikisha madai ya watu hawa wenye ulemavu yanasikilizwa na kutolewa majawabu" alisisitiza Ado Shaibu

Kwa kumalizia Ado Shaibu ambaye ni Katibu mwenezi wa ACT Wazalendo Taifa aliitaka jamii kiujumla kuzingatia misingi yetu ya Utu, Upendo na Udugu, kusimama pamoja na watu wenye ulemavu kukipinga kitendo hiki cha kuwavunjia utu wao.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search