Wednesday, 7 June 2017

HIKI NDICHO ALICHOKISEMA MTATIRO BAADA YA ANNA MGWIRA KUKUBALI UTEUZI WA KUWA RC MKOANI KILIMANJARO


Na. Mtatiro J

#UTEUZI_WA_KITILA
Niliunga mkono uteuzi wa Prof. Kitila kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kitila tangia hapo amekuwa mtendaji ndani ya Serikali kwa hiyo kilichofanyika ni kumhamisha tu kutoka kutumikia Chuo Kikuu hadi Wizara mojawapo serikalini.

#UTEUZI_WA_BI_MGHWIRA
Siungi mkono Uteuzi wa Anna Mghwira kuwa RC, japo naendelea kumheshimu na kuheshimu uamuzi wake wa kupokea uteuzi. Kama JPM angelimteua kuwa Mbunge, ningeunga mkono na kumpigia makofi makubwa sana.

#UTEUZU_WANGU
Na hapa ieleweke kuwa, kama leo JPM ananiteua mimi kuwa Mbunge, ntakwenda Bungeni na ntabakia na hadhi ya kutumikia mawazo ya wananchi na ntaipa changamoto serikali na kuisaidia huku nikijenga chama changu. Lakini leo JPM akiniteua kuwa Waziri au Mkuu wa Mkoa ntamshukuru kwa kiingereza. "NO, THANK YOU!"

#MANDELA
Unajua, hizi siasa tulizomo zina misingi yake na lazima uijue, uisimamie na uipiganie. Nelson Mandela alifuatwa Gerezani mara kadhaa na Makaburu, wakamuomba akubali kutolewa gerezani ili apewe Umakamu wa Rais wa Afrika ya Kusini na hadhi kubwa sana. Mandela alisema "NO, UNTIL MY PEOPLE ARE FREE FROM APARTHEID" (Sitaki, hadi watu wangu wawe huru na kuondoka kwenye Utawala wa Kibaguzi).

Maneno ya Mandela yanatukumbusha kuwa, tunapokuwa na majukumu makubwa na tumeaminiwa na kupewa nyadhifa kubwa za kisiasa kwenye taasisi zetu, kipaumbele chetu kinapaswa kuwa AGENDA ya Taasisi yetu na chombo tunachokitumia kuisimamia ajenda hiyo (Forum).

#MASHARTI
Mathalani, ukitaka mimi nifanye kazi katika Serikali ya Magufuli (katika cheo kisicho Ubunge) ntakupa masharti magumu na ya msingi. Sharti la kwanza, Je Serikali ya Magufuli iko tayari kusimamia Demokrasia hapa Tanzania? Je, iko tayari kuruhusu Uhuru wa Mawazo na Tofauti ya Mawazo? Je iko tayari kuruhusu Uhuru wa Bunge na Ukuu wa Katiba? Je iko tayari kufuata na kulinda Sheria za nchi? Je iko tayari kuwa sikivu na isiyofanya maamuzi kwa ubabe na ukuu wa mtu mmoja?

Ikiwa Serikali ya Rais Magufuli ingelikuwa imeamua kufuata utaratibu wa kuleta mabadiliko nchini kwa njia ya kulinda demokrasia, kuheshimu katiba na sheria za nchi, kuimarisha nguvu na umuhimu wa Bunge na Mahakama na Kukuza Misingi ya Umuhimu wa Vyama Mbadala na Uhuru wa Kutoa mawazo; ningeliunga mkono uteuzi wa Mama Mghwira!

#UTAMADUNI_NA_UTARATIBU
Lakini niwakumbushe jambo lingine, kwamba masuala ya VIONGOZI wa chama kimoja kuteuliwa kujiunga na Serikali ya Chama kingine, hufanywa kwa heshima kubwa. Yaani, uteuzi wa KIONGOZI wa chama cha ACT kujiunga Serikalini duniani kote, ulipaswa kufanywa kwa heshima. Kwa kawaida, Rais alipaswa kuwasiliana na Kiongozi Mkuu wa chama na kumjulisha nia hiyo, hata kama Kiongozi Mkuu wa ACT na chama chake wangelikataa, Rais angelikuwa ametimiza wajibu wake wa Ustaarabu wa Kidemokrasia.

Ndiyo maana, Katibu Mkuu wa UN alipotaka kumteua Dk. Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN kwanza aliomba ruhusa kwa Rais Kikwete (Rais aw Tanzania), huo ndiyo utaratibu IKIWA UTEUZI UNAFANYWA KWA NIA NJEMA!

#GNU_ZNZ
Ama, unapotaka kuteua Kiongozi kutoka Chama kingine kunapaswa kuwa na mazungumzo ya kivyama. Mathalani, uundaji wa GNU Zanzibar (2010 - 2015) ambapo wakati wa kuandaa Baraza la Mawaziri, CUF ilipendekeza majina ya watu wanaopaswa kuteuliwa na Rais Shein, na Shein akawateua, hakujiamulia tu! Mambo haya huhitaji utaratibu, na unapovunjwa yanachukuliwa kama michezo michafu, kudhoofishana, kushughulikiana, kupeana rushwa za madaraka, vyeo, ukubwa, mali, fedha n.k.

#SISI_NA_WAO
Sisi ambao tunathubutu kujadili teuzi hizi za JPM tunaambiwa tuna wivu, tuna gere n.k. huo ni upuuzi tu. Sisi binadamu tulivyoumbwa, wapo watu akiona VX kubwa la Serikali na Walinzi wa kumlinda, anaona AMEUKATA! Tupo watu tunaoona vitu hivyo kama MATERIAL THINGS (vitu vya kupita tu). 

Wapo watu huamini kuwa siku wakiteuliwa na kuwa na MAMLAKA juu ya Maelfu na Makumi Elfu, huko ni KUUKATA...Tupo sisi wengine ambao tunaamini vyeo ni vitu vya kupita tu. Leo mama Anna Mghwira ameteuliwa, amekubali uteuzi huo, amekiacha chama chake "bila kukubaliana nacho," ameacha misingi yake alokuwa anaisimamia, na ameungana na wale wasiotaka kabisa chama chake kifanye hata mkutano wa hadhara, amepokea uteuzi bila hata kumwambia mteuzi "heshimu katiba na sheria za nchi." 

#TUSIMHUKUMU
Tusimhukumu, tumjadili tu ili itupe mafunzo mbeleni. Lakini nataka kuwaambia kuwa ANAYESALITI imani yake kwa sababu ya cheo hujidanganya yeye mwenyeww, vyeo, ukubwa, mamlaka na ukuu vinapita haraka mno, kama upepo na historia inaandikwa juu ya kila mmoja wetu.

#BOB_MARLEY
Hayati Bob Marley alipata kusema "Wapo wanamuziki wana Pesa na Utajiri mkubwa sana kwa sababu ya muziki lakini fedha zao hazitadumu. Mimi (Marley) nina utajiri wa Mashairi, siyo fedha, mashairi yangu yatadumu milele, ujumbe wake utadumu milele, maana sikuwa naimba ili kupata pesa, bali kusimamia misingi nayoiamini."

Mtatiro J,
juliusmtatiro@yahoo.com
Whatsup; 0787536759.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search