Monday, 19 June 2017

KIJANA Ajinyonga Kwa Kamba Juu ya Mti Kisa Ugumu wa Maisha

Picha ya Tukio jingineKijana Paulo Ezekiel, amejinyonga kutokana na kile kinachodaiwa ugumu wa maisha.

Paulo (17) alikuwa anaishi na wazazi wake Mtaa wa Mazinge Kata ya Ndembezi mjini Shinyanga, alifariki dunia juzi usiku kutokana na kudaiwa kujinyonga kwa kamba juu ya mti jirani na nyumbani kwao.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa kumi alfajiri baada ya marehemu kutoka nje ya geti la nyumba yao na kuelekea kwenye mti huo kisha kijipiga kitanzi kunakodaiwa kusababisha kifo chake.

Akizungumza tukio hilo jana, baba mzazi wa marehemu, Ezekiel alisema awali kijana wake alikuwa na ugomvi na marafiki zake ambao ni madereva bodaboda, lakini huo ulisuluhishwa na akaendelea na majukumu yake.

Alisema chanzo cha kifo chake hakijafahamika vizuri, lakini mara kwa mara alikuwa akilalamika kuwa maisha ni magumu.

"Ilipofika majira ya saa 10 usiku nilisikia mlango wa chumba cha kijana wangu ukifunguliwa, nikajua ametoka kwenda kujisaidia lakini muda mrefu ulipopita bila kusikia amerudi, ndipo nikatoka nje na kukuta geti la uani likiwa wazi, nikaanza kumtafuta bila mafanikio", alisema. 

Aliongeza:
"Niliporudi ndani nikamwamsha mama yake mzazi na wadogo zake wa kike, tukaanza kumsaka ndipo tukamuona akiwa juu ya mti jirani na nyumba yetu, akiwa ameshafariki kwa kujinyonga na kamba". 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Jumanne Murilo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi la hilo kuhusiana na tukio hilo.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga na unatarajiwa kuzikwa leo kwenye Makaburi ya Mtaa wa Dodoma mjini hapa.

Chanzo: Nipashe

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search