Tuesday, 20 June 2017

Magufuli Alichowafanyia Vigogo Hawa Haijawai Kutokea

Ikiwa ni siku 593 kamili tangu Rais Dk. John Pombe Magufuli (pichani) aingie madarakani Novemba 5, 2015, serikali yake imevunja utaratibu na mazoea ya miaka mingi, baada ya kuchukua maamuzi magumu ambayo hayakuangalia sura, cheo, hadhi wala utajiri wa mtu katika kulinda na kutetea masilahi ya taifa, UWAZI, limegundua.

Kamishna Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya (katikati) sambamba na Waliokuwa Wafanyakazi wa Benki ya StanBic Tanzania, Sioi Sumari (kushoto) na Shose Sinare (kulia) wakiwa mahakamani.

ILIVYOKUWA HAPO AWALI

Kabla ya Rais Magufuli kuingia madarakani, kulikuwa na mazoea ya kuamini kuwa watu wenye nyadhifa nzito katika mashirika ya umma, serikalini au matajiri wasingeweza kuonja shubiri za vyombo vya dola, kutokana na kukithiri kwa tabia ya kulindana kutegemea na cheo au hadhi ya mtu.

Mgawe na wenzake watatu wakifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
“Unanijua mimi ni nani?” Haya yalikuwa ni maneno ya kawaida kutamkwa na mabosi wengi walipohitaji kuwatisha watendaji wa serikali katika kutimiza majukumu yao, kama vile kudai kodi, kuhimiza utekelezaji wa matakwa ya kijamii na mambo mengine kadha wa kadha.

Aidha, halikuwa jambo la kawaida kwa kigogo wa taasisi kubwa, mathalan meneja,mkurugenzi au tajiri, kushikiliwa na vyombo vya dola kwa muda mrefu, kwani simu zingepigwa kutoka ‘juu’ na mara moja mtu angekuwa huru uraiani, kitu ambacho kilichangia sana kuwepo kwa jeuri miongoni mwa wenye fedha, vyeo na hadhi huku wananchi wa kawaida wakiishi kinyonge na kuweka mazingira ya kuonewa na kudhulumiwa.

JPM SASA ALIVYOMALIZA ‘MAZOEA’

Ujio wa Rais Magufuli umeleta mabadiliko mengi yenye tija kwa wananchi wa kawaida, kwani siyo tu utu na haki yao imewekwa mbele, bali mazoea ya watu kutumia majina, hadhi na utajiri wao yamefikia mwisho, kwani sheria imekuwa ni msumeno unaokata pande zote.

Aidha, ile tabia ya viongozi wa serikali, walioharibu huku kuhamishiwa kule nayo imekoma, kwani mara kadhaa, amechukua maamuzi magumu kiasi cha kuwashangaza wengi.

WATEULE WAKE WAONJA JOTO YA JIWE

Tofauti na ilivyozoeleka katika uongozi wa marais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, katika utawala wake Rais Magufuli amewatoa kazini viongozi walioaminika kuwa ni watu wake wa karibu, huku akisisitiza kuwa katika masilahi ya taifa, hana urafiki.

Kiongozi wa kwanza kuonja joto ya jiwe ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ambaye alitolewa katika nafasi yake kwa makosa ya kimaadili, baada ya kudaiwa kuingia bungeni kufanya kazi ya serikali akiwa amelewa.

Baadaye akafuata Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakati huo, Anna Kilango Malecela ambaye alijikuta akipoteza nafasi yake baada ya kutoa tamko kuwa katika mkoa huo, hakukuwa na wafanyakazi hewa, jambo ambalo halikumridhisha kiongozi huyo wa nchi. Baadaye kulibainika kuwepo kwa watumishi kadhaa hewa, akatumbuliwa.

Mteule wa karibuni kabisa kukosa kazi ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alijikuta akipoteza kazi kufuatia ripoti ya kamati ya kuchunguza sakata la usafirishaji mchanga wa madini. Rais Magufuli alisema pamoja na kuwepo kwa urafiki kati yao, jambo hilo halikubaliki na anastahili kuwajibika.

MABOSI KIBAO SERIKALINI WALALA SELO

Tofauti kabisa na miaka ya nyuma, serikali ya awamu ya tano, imekuwa haina mchezo linapofika suala la maadili ya kazi na ofisi za umma. Hadi sasa, makumi ya watumishi katika nafasi mbalimbali wamejikuta wakilala selo, kitendo ambacho kilikuwa ni nadra kufanyika miaka ya nyuma.

“Ni kweli hata katika tawala zilizopita kuna vigogo walikuwa wanafanya makosa na wanafikishwa katika vyombo vya dola, lakini ilikuwa ni kwa muda tu, kwani wengi walitoka nje hata kwa makosa ambayo walistahili kusubiri mahabusu wakati kesi zikiendelea, au wengine kesi zao zilifutwa katika mazingira ya kutatanisha na kwa ujumla, mahabusu hakukuwa sehemu ya mabosi na matajiri,” alisema Enock Masulungu alipoombwa kuoanisha utendaji wa serikali hizo tatu (awamu ya pili, tatu, nne na tano).

“Hiki anachokifanya Magufuli ni jambo zuri na kilishatabiriwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, mzee Yusufu Makamba mjini Dodoma wakati anamkampenia urais kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho aliposema, Jakaya Kikwete alibatiza kwa maji lakini Magufuli atabatiza kwa moto,” alisema Masulungu.

Akaongeza kuwa ilikuwa ni vigumu kwa serikali zilizopita kuona wakurugenzi wakuu au makamishna kufikishwa mahakamani lakini serikali ya Magufuli imefanya hayo, hivyo kuandika rekodi kwa marais wa Tanzania waliopita.

HII HAPA ORODHA YA VIGOGO MATATANI

Tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015 vigogo walioshitakiwa ni wengi na baadhi yao ni hawa wafuatao.

Maofisa nane wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakiongozwa na Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki wapo matatani baada ya kufikishwa mahakamani Desemba 4, 2015 kwa tuhuma za kutoa makontena 329 bandarini bila ya kulipiwa kodi na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 12.7.

Vigogo wengine waliopandishwa kortini pamoja na Masamaki ambao tangu wakati huo wako mahabusu ni Habibu Mponezya, (Meneja wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja) na Bulton Mponezya.

Kamishna Mkuu Mstaafu wa TRA, Harry Msamire Kitilya na wenzake wawili, Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon nao wapo mahabusu wakiendelea na kesi yao tangu walipopandishwa kizimbani Aprili Mosi, 2016 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaamu.

BANDARINI HAWAKUACHWA

Katika Bandari ya Dar es Salaam, moja kati ya milango ya uchumi nchini, moto wa Rais Magufuli umewawakia mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na naibu wake, Hamadi Koshuma wakajikuta wakikabiliwa na kesi na kutakiwa kujibu mashitaka ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Januari 16,2016.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa katika utendaji wao wa kazi kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba wa kibiashara bila kuitisha zabuni.

NIDA NAO HAWAKUBAKI SALAMA

Serikali ya Rais Magufuli pia imemburuza mahakamani aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na maofisa wengine saba waandamizi Agosti 17, 2015, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka 27 yakiwamo madai ya matumizi mabaya ya ofisi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.2.

Washitakiwa wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibiashara, Avelin Momburi, Meneja wa Fedha na Uhasibu, Benjamini Mwakatumbula, Meneja wa Bajeti na Miliki, Joseph Makani, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima na Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.

Wengine ni Xavery Kayombo ambaye wadhifa wake haukutajwa, na Astery Ndefe ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers Company Limited.

PEDESHEE NDAMA

Mwingine aliyekumbana na ‘mkono’ wa dola ya Magufuli ni mfanyabiashara Ndama Shaabani ‘Pedeshee Ndama Mutoto ya Ng’ombe’ ambaye alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu kwa tuhuma za kughushi, kutakatisha fedha na kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu. Kwa muda wote wakati kesi yake ikiendelea, amekuwa mahabusu. Moja ya mashtaka yake ametiwa hatiani na amelipa faini ya shilingi milioni 200. Kesi bado inaendelea.

Licha ya vigogo hao, wapo pia vigogo mbalimbali katika ngazi za wilaya na mikoa ambao wanashikiliwa kwa tuhuma mbalimbali, kitu ambacho huko nyuma, kilionekana kuwa si cha kawaida.

Hata hivyo, enzi za Jakaya Kikwete, serikali yake ilimudu kuwapeleka mahakamani na kuwakuta na hatia mawaziri wawili wa zamani, Daniel Yona na Basil Mramba huku vigogo waliohusika na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nao wakipelekwa mahakamani.

Vigogo hao ni Meneja wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Kyabukoba Mutabingwa, Mkurugenzi wa Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Julius Angello pamoja na Mwanasheria Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),Steven Urass

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search