Wednesday, 12 July 2017

HALIMA MDEE SASA KUKUTANA NA KIBANO CHA BUNGE

Siku moja baada ya Mbunge wa Kawe Halima Mdee kuachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, amesema Mdee, atafikishwa mbele ya Kamati ya Maadili ya bunge, pindi utaratibu utakapokamilika.

Mdee alikamatwa Julai 4 kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi akidaiwa kutoa lugha ya kumkashifu Rais John Magufuli. Hapi aliagiza Mdee awekwe mahabusu kwa saa 48 lakini alikaa siku sita.

Juzi Mbunge huyo aliachiwa kwa dhamana mahakamani hapo baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati yenye thamani ya Sh10 milioni na yeye mwenyewe. Alisomewa shitaka moja ya kumkashifu Rais.

Baada ya kuachiwa kwa mbunge huyo jana, Mwananchi Digital lilihitaji kufahamu ni lini mbunge huyo atafikishwa mbele ya kamati ya maadili ya bunge kama agizo la Spika lilivyotaka.

Dk Kashilila amesema alikuwa hafahamu kama mbunge huyo ameachiwa kwa dhamana lakini muda utakapofika na ratiba ikapangwa kamati itayatekeleza yale maagizo ya Spika.

“Sidhani kama nina sababu ya kukuambia mimi jambo ambalo hata kamati yenyewe bado haijakutana kufanya hiyo kazi, kamati itakapokutana sisi tutatoa hiyo taarifa,” amesema Kashililah.

Baada ya kupiga simu ya Mdee kwa muda mrefu bila kupokewa tulizungumza na Katibu wa Chadema wa Mkoa, Henry Kilewo juu ya suala hilo na kusema ingawa taarifa ya Spika ilitolewa mbele ya wabunge lakini Mbunge huyo hawezi kufika mbele ya kamati ya maadili hadi taratibu zitakapofuatwa.

“Kuna taratibu za kibunge zinazotakiwa kufuatwa endapo unamuhitaji mtu kufika mbele ya kamati yoyote. Kwa kawaida hutumiwa wito unaoonyesha ni lini anahitajika ili aweze kusikiliza alichoitiwa,” amesema Kilewo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search