Monday, 31 July 2017

MSIKILIZE MH MBOWE AKIZUNGUMZIA HALI YA UCHUMI NCHINI TANZANIAChama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Leo kimekutana na Wanahabari katika mkutano uliofanyika Upanga kwenye Hotel ya Courtyard, Protea.

Huu ni Mkutano wa Uongozi wa Juu wa Chama na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari waandamizi, umekafanyika kuanzia Saa 04:30 asubuhi, katika hoteli ya Protea Courtyard

Hii inatokana na uamuzi ambao Kamati Kuu ya CHADEMA imeufanya katika mkutano wake wa siku mbili; tarehe 29-30 Julai, 2017 katika Hotel ya Double Tree, jijini Dar es Salaam.

Maeneo ambayo yamejadiliwa na kuridhia kuchukuliwa kwa hatua ni;

1. Hali ya mwenendo wa siasa katika nchi na ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya awamu ya tano.

2. Kuporomoka kwa uchumi na hali ngumu ya maisha kwa Watanzania

3. Kamata kamata inayoendelea kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA maeneo mbalimbali nchi nzima.

Nimefika maeneo haya, ntahakikisha nawahabarisha kila kinachojiri. Karibuni.


CDM1.jpegCDM2.jpeg 

Kamati kuu ilikua na kikao cha siku mbili kilichotanguliwa na Mkutano maalum. Viongozi wakuu walijumuika na Viongozi wa kanda mbalimbali za CHADEMA. Tulitafakari kwa kina hali za kisiasa na kamatakamata kwa viongozi wa Upinzani na hali ya Uchumi wa taifa.

Kikao cha leo kitajadili jambo moja nalo ni Hali ya uchumi katika taifa. Tumezoea kuzungumza maswala ya kisiasa, lakini sisi kama taifa hatujajipa nafasi ya kutambua hali ya uchumi.

Rais wetu tumempa likizo sana sababu yeye na Serikali yake hawajabanwa vizuri kuhusu hali ya uchumi. Vyombo vyetu vimekua vikiangalia uchumi kutokana na kauli za Serikali na sio mbaya lakini inatakiwa tujue hali hii inatupeleka wapi.

Benki ya dunia huwa inatoa taarifa IMF na BOT. Taasisi inayotoa taarifa halisi za uchumi nchini ni Benki Kuu na kila mwezi inatoa taarifa ya kiuchumi na leo tutatumia taarifa za Benki Kuu.

Kwa Sababu ya faida ya kikao hiki nitazungumzia mambo madogo sita ili kuona Mei 2015- Mei 2017 ni mambo gani yanaendelea katika nchi.

Wataalam wetu wamefanya uchunguzi wa kinachosababisha uchumi kuporomoka.

1. CHAKULA

Chakula ndio maisha yetu na 75% ni wakulima katika nchi yetu. Rais anasema hatatoa chakula, sisi tunasema "Magufuli, hiki chakula si chako"!

2015, tukiwa chini ya Serikali ya Awamu ya nne tulikuwa na tani zaidi ya laki nne(400,000) lakini 2017 kuna tani sabini na nne elfu(74,000) ambayo ni Asilimia 18 ya chakula ukilinganisha na Awamu ya nne.

Vyakula vyote sasa vimepanda bei wakati mapato kwa wananchi yanashuka. Mishahara haijaongezwa wala rais halimsumbui hilo. Wakati mataifa mengine yanasaidia nchi zao kupata chakula sisi hatufanyi hivyo.

Sekta ya kilimo imekua kwa 1.7% tangu Rais aingie madarakani. Tume ya maji ya kuboresha kilimo cha umwagiliaji haijapewa kitu. Uchumi unakua kwenye mifuko ya watu wachache, Uchumi unakua wakati umasikini unaongezeka.

Sekta ya Kilimo ufugaji na uvuvi inasinyaa. Kipaumbele cha rais ni kununua ndege. Hii fedha ya ndege ingepelekwa kwenye kilimo, watanzania milioni 40 wangecheka.

2. HALI YA UKATA WA NCHI

Ukata unasababishwa na usimamizi mbovu wa Uchumi. Mzunguko wa fedha umeathirika sana. Fedha iliyoingizwa kwenye mzunguko imepungua kwa asilimia tano(5%) na hali hii inasababisha mdororo wa uchumi.

Sekta binafsi ndo sekta inaongeza uchumi wa taifa lakini Rais anaamini kila mmoja kwenye sekta binafsi ni mpiga dili. Rais bado anaamini anaweza kurudisha hili taifa kwenye ujamaa.

3. UBINAFSISHAJI

Kuna ugonjwa ambao ukiusikia kama unajua biashara utajiuliza hivi sisi tuna akili? Jambo linalohusu ubinafsishaji. Tangu rais huyu aingie madarakani anasema viwanda tutavirejesha serikalini na wananchi wanapenda kauli hii. Wananshangilia na watu wakimshangilia naye anavimba kichwa.

Hii ni sera ya mtu asiyejua uchumi. Hakuna mfanyabiashara duniani ambaye atapewa kitega uchumi kinachoingiza faida akakifunga kwa sababu anaichukia Tanzania. Hivi viwanda vilibinafsishwa baada ya serikali kushindwa kuviendesha kwa kukosa ruzuku ya Serikali. Viwanda hivi vilivyobinafsishwa vilikuwa vinaendeshwa kwa hasara, wengi walijaribu kivifufua wakashindwa kwa sababu vilikuwa havipati ruzuku, vina teknolojia ya zamani au tulikuwa na soko hodhi, hapakuwa na ushindani wa biashara lakini sasa kuna soko huria.

Rais anasema tutachukua viwanda, anachukuwa viwanda anavipeleka wapi? Serikali haiwezi kujenga viwanda bali viwanda vinajengwa na watu binafsi. Kwanza serikali haina hela.

Kuwekeza nchi hii ni maumivu makubwa sana. Rais anatoa hii kauli kwa sababu ya kutokujua tu. Tunaongozwa na viongozi ambao hawajui misingi ya biashara na hawajui uzito wa wawekezaji binafsi. Serikali hii haipambani na wawekezaji wa nje, bali inapambana sana na wawekezaji wa ndani.

Serikali imejiondoa kwenye biashara na ili biashara iende lazima sekta binafsi zikope lakini ukiangalia taarifa ya Benki Kuu utaona anguko la sekta binafsi.

Watu wetu wa kilimo hawakopi nje ya nchi bali kwenye Benki zetu. Sekta ya kilimo mikopo ilikuwa inakopwa 6% ya mikopo ya kibenki lakini sasa imeshuka hadi - 8% yaani hasi ikimaanisha hakuna uwekezaji mpya kwenye kilimo.

Sekta ya biashara, Ujenzi, zote zimeshuka; hii ina maana kuna miradi imefungwa. Sekta ya viwanda ambayo Waziri wake sijui kama anajua biashara au aliwahi kuuza mkaa, 32% walikuwa wanakopa ila sasa hawajakopa chochote yaani 0%. Hivi viwanda vinavyofunguliwa ni viwanda vilivyotafutia mikopo serikali ya Kikwete, Serikali hii haijajenga kiwanda hata kimoja.

4. BIASHARA YA MAUZO NJE NA NDANI

Kuhusu Biashara ya mauzo nje na ndani. Uchumi wetu ni wa kuagiza bidhaa za nje. Bidhaa za kuagiza zimeshuka kwa asilimia kumi na nne, vifaa vya usafirishaji zimeshuka kwa asilimia kumi na tano. Malori yamelala pale bandarini hakuna kazi.

Mafuta yanayoagizwa kutoka nje, yamepungua kwa 14.3%. Kitu pekee kilichoongezeka kutoka nje ni chakula yaani katika vitu kumi, chakula ndo tunaagiza sana na imeongezeka wakati sisi ndo tulitakiwa tuuze nje. Tumeshindwa kuzalisha.


5. DENI LA TAIFA

Ili serikali ijiendeshe inabidi kukopa. Tunapolalamika tupunguze kukopa, wanasema Tanzania bado inakopesheka. Deni la taifa limekuwa jini linalonyonya Serikali damu na sasa hivi hawakopesheki tena.

Deni la nje dola bilioni 7 kwa miaka miwili, deni la ndani dola bilioni 11.7 kutoka bilioni 7.7 mwaka 2015. Wastani wa mapato ni trilioni 1.2. Deni la nje kila mwezi tunalipa bil 650-800. Makusanyo ya ndani tuliyoyataja hapa hayatoshi kulipa deni, fedha za maendeleo, na kila kitu.

6. ⁠⁠⁠MAKINIKIA

CHADEMA tumekuwa tukipiga kelele kuhusu haya maswala. Huyu jamaa karekebisha lakini alivyorekebisha sivyo.⁠ ⁠Kilichofanywa kwenye makinikia ni papara. Rais na wabunge walifanya papara na wananchi wakalishwa papara. Tulisema jambo hili lifanywe katika misingi ya kutoathiri uchumi wa Taifa. Kumkamata mwizi ni sifa ya taifa, lakini kuua mwizi bila kumuonesha ni jinsi gani umemuua ni fedheha.

Dola bilioni 190 tunawadai ACACIA. Bajeti ya serikali ni dola bilioni 13, lakini tumeitoza kampuni moja dola Bil 190. Tunaonekana machizi na tumekuwa watu wa kudhalilishwa duniani. TRA tafuteni fedha sio za kutia aibu. Kwa mwendo huu hatufiki.

Tunataka serikali iweke hadharani ripoti za makinikia wachumi wazipitie. TRA watueleze wamepataje hiyo kodi? Watueleze tujue maana hii ni mara nne ya pato la taifa.

Watu wanawekeza kwenye nchi zinazoheshimu sera na sheria. Tunajidanganya kwamba Tanzania ni nchi ya kipekee sana. Hatupingi mapambano ya kutafuta haki ya rasilimali zetu lakini mambo haya yatumie akili na busara na hekima.

Maamuzi ya Rais yanawatesa watanzania. Tunataka serikali ije na mpango wa kufufua uchumi wa nchi hii. Tanzania tulikuwa tunaenda katika hali ya kuridhisha lakini sasa tumerudi nyuma. Tutaanza kukosa hata sabuni.

Mbowe amemaliza na amezungumza kwa niaba ya chama taifa. Ametoa tamko kwa niaba ya Kamati Kuu ya CHADEMA.


MASWALI

1. Je hamuoni kuna haja ya kutokukimbia bajeti kama mnavyofanya Bungeni ili msimamie haya mambo?
2. Je hela inayokopwa inakwenda wapi?
3. Je hawa wafanyabiashara hawakuwa na uzoefu wa viwanda?
4. Je kamati ya bajeti inapewa ushirikiano na Serikali?
5. Leo unamlaumu Rais kunyang'anya watu viwanda ambavyo mlikuwa mnalalamika zamani wanyang'anywe. Je kulikoni?

MAJIBU

Halima Mdee (Mbunge wa Kawe) anajibu ni kwanini wanapiga kura ya hapana kwenye swala la Bajeti.

Anasema, "Ndani ya Bunge kuna kura za ndio, hapana au hayupo kotekote. Hii ni haki ya mbunge. Serikali wao kwa mtazamo wao wanaona ni mambo ya kipaumbele lakini sisi tunaona sio kipaumbele. Pale Bungeni tunajadiliana ni nini kianze kama kipaumbele. Tulipiga hapana sababu tunaamini haiwezekani ukaja na utekelezaji wa bajeti wa 34%, halafu unakuja kuleta bajeti ya trilioni 32. IMF juzi wamesema bajeti ya Tanzania ni ya hovyo na haitekelezeki."

Anaendelea, "Wizara inayoongoza fedha nyingi haigusi wananchi moja kwa moja. Tukiwekeza kwenye Elimu, kilimo ndio tungefanikiwa kuliko Viwanda. Ununuzi wa ndege sio kipaumbele ndo maana hatujaiunga mkono bajeti. Tulipelekwa bungeni kuisimamia serikali na kutoa mawazo mbadala"
⁠⁠⁠⁠
Mbowe anajibu baadhi ya maswali

⁠⁠⁠⁠Jipeni muda wa kusoma bajeti mbadala. Sisi hatupo pale kuunga mkono kila kitu cha Serikali. Ikifanya vizuri tutaiunga mkono. Kama wabunge tungekuwa na umoja, hii bajeti isingepita. Ndio maana kabla ya bajeti, wabunge wa chama fulani walipewa milioni kumi kumi Bajeti ikapita. Wakati sisi tumeandaa hotuba makini, ukatengenezwa mkakati wa makinikia. Watu hawakujua wapinzani wana hoja gani.

Deni la taifa hili nyongeza imeenda wapi? Anayeisimamia hii nyongeza sio kambi ipinzani bali ni BoT. Hii ni ripoti ya CAG, alisema sheria inayosimamia deni imepitwa na wakati. Na hili deni linakwenda wapi? Tuliomba kabla ya kukopa Bunge tuambiwe.

Viwanda vilivyobinafsishwa vipo vya aina mbalimbali. Vipo vinavyoendeshwa kwa faida kama kiwanda cha bia na Sigara. Hivi vilibinafsishwa kwa bei ya kutupa na ubinafsishaji ulifanyika kwa upendeleo na haukuwa wa wazi. Ninachokipinga sio zoezi zima kwa ujumla. Ukinipa kiwanda nikaona godown inalipa kuliko kiwanda ntakifanya godown huo ndo ukweli. Mfanyabiashara anatafuta faida na biashara ni kubadilika.

Bunge leo ni mateka wa serikali, ambacho kinatoka serikali Kuu Bunge leo haliwezi kukataa. Kamati ya bajeti haiwezi kupinga kitu. Uhuru wa Bunge kufanya mambo yake haupo. Bunge linaangalia maslahi ya Rais, Chama halafu ndio Taifa.

Sijasema namlaumu rais kurejesha viwanda, nimesema kwenye biashara ni kitu cha kawaida mtu kubadilisha biashara.

Sheria za madini zimepitishwa harakaharaka na bado tunarudia kosa lile lile. Tumepitisha sheria tatu kwa muda siku tatu tu

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search