Monday, 10 July 2017

ROMA;NINGESEMA WALICHOTUFANYIA WATEKAJI HAKUNA MTU AMBAYE ANGEKUWA YUKO TAYARI KUKARIBIANA NA MIMI

Mwanamuziki Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki” amesema kuwa tukio lililotokea miezi mitatu iliyopita lilikuwa na sababu nyingine zaidi ya muziki anaoufanya, tofauti na watu wanavyodhani.

Roma amesema katika mahojiano na EATV kwamba alijua kuwa atawakwaza baadhi ya watu kwa kutosema na kuweka wazi mambo kadhaa kuhusu tukio hilo ikiwemo kutekwa, walipopelekwa, kilichowatokea wakiwa huko walikopelekwa n.k lakini aliamua kutumia busara na kutosema kitu ili aweze kulinda sanaa na maisha yake kwa ujumla.

“Mimi najua nini kilipelekea wale jamaa kututeka. Ni zaidi ya muziki, japo chanzo ni muziki ndio maana walikuja kututeka tukiwa studio na si kanisani wala nyumbani. Unajua wananchi tayari walikuwa na video kichwani wakijua Roma anakuja kuongea hiki na kile, tunamaliza pale halafu usiku mwema.”

“Lile tukio lilikuwa linahitaji busara ili maisha yaweze kuendelea. Labda ningesema ukweli pengine ungekuwa ndio mwisho wa Roma kwenye muziki. Mashabiki wangeshangilia lakini kwa wadau mbalimbali mchango ndio ungekuwa umekwisha,” alisema.

Roma alisisitiza kuwa kama angeweka wazi jambo hilo siku ile ambayo alitoka, ingepelekeaa yeye kuacha muziki na kurudi Tanga kufanya mambo mengine, kwani hakuna mtu ambaye angetaka kuwa karibu naye tena.

“Toka nimetoka mpaka sasa sitaki kutazama video mbalimbali ambazo zinaonesha jinsi watu walivyokuwa wakihangaika kututafuta. Sitaki kutazama kwa sababu sitaki kukumbuka kabisa hali ambayo nilikuwa nayo kipindi kile. Pia sipendi kabisa kuona mtu mwingine yeyote anakwenda huko chimbo ambako tulikuwa tumewekwa tukipata mateso,” alisema.

Roma na wenzake walitekwa mwezi wa nne mwaka huu walipokuwa katika studio za kutayarisha muziki za Tongwe Records na kupelekwa kusikojulikana kwa muda wa siku tatu na kuja kuonekana wakiwa na majeraha mbalimbali mwilini.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search