Monday, 17 July 2017

Ushuhuda: Nilimlisha mume wa mtu limbwata la nyama ya bundi – Sehemu Pili


NAPEWA DAWA ZA KUMPUMBAZA MUME WA MTU.
Mungu wa Kabili aliniambia, nikisha fanya mapenzi na huyo mwanaume, niende kwake ili anipe dawa za kumpumbaza. Nilipofika akaniambia, vitu vinavyo hitajika katika kutengeneza hiyo dawa ya kumpumbaza huyo mwanaume, ni NYWELE ZA MWANAUME MWENDAWAZIMU, NYWELE ZA MWANAUME ASIYE SIKIA ( KIZIWI ) , NYWELE ZA MWANAUME KIPOFU AU FIMBO ILIYO TUMIWA NA MWANAUME KIPOFU, KAMBA ILIYO TUMIKA KUMFUNGA KONDOO , pamoja na UCHAFU WA JALALANI.
Vitu vyote hivyo vilitafutwa vikapatikana, vikachanganywa na dawa nyingine za kichawi,kisha vikatumika kutengeneza uchawi. Nikaambiwa nitamuwekea kwenye maji ya kuoga na nyingine nitamuwekea kwenye chakula .
Halafu nikapewa na kibuyu, ndani ya kibuyu kile kulikuwa na kipande cha nyama. Mganga akaniambia hiyo ni nyama ya ndege wa usiku mwana wa jinni, ambayo baadae nilikuja kujua kuwa ni Bundi wa Kichawi, ambae ni tofauti na bundi wa kawaida.
Mganga akaniambia utapika nyama, katika nyama utakayo pika ambayo utamuwekea ndumba, mwanaume wako, utachanganya na nyama hiyo, pamoja na kucha zako, na nywele zako za siri.
Nilipo rudi nyumbani, nikafanya kama nilivyo elekezwa.
Baada ya kufanya uchawi huu, K alikuwa kama mwendawazimu kwangu, hakusikia wala kuambiwa na mtu yoyote Yule. Akawa anafanya kila ninacho taka akifanye mimi. Akaanza kuwa ananipa mali zake, magari, viwanja, nyumba, biashara pamoja na miradi yake..
NATEGA UCHAWI WA KUTOA MIMBA YA MKE MWENZANGU.
Mapenzi yangu na K yalipamba moto, nyumba aliyo nipangishia haikuwa mbali sana na mahali alipokuwa anaishi yeye na mkewe, wao walikuwa wanaishi Tabata Mawenzi, mimi akanipangia nyumba nzima Tabata Kimanga.
K alihama kwa mke wake, akawa anaishi nyumbani kwangu. Taarifa za K kuishi na “mchepuko” zilimfikia mke wake, lakini hakuwa na kitu cha kufanya kwa sababu K alikuwa ndio anamuweka mjini yeye na familia yake na mwanamke alikuwa mama wa nyumbani tu.
Mara nyingi K alikuwa ananishauri amfukuze mke wake, ili nikaishi nae kwenye nyumba yake, ili kuninonyesha kuwa ananipenda sana na mimi ndio kila kitu kwake.
Ila kuna kitu kimoja, alinifundisha Mungu wa Kabili, kwamba unapokuwa mchawi, unatakiwa uwe mnafiki. Usiache kabisa watu wajue kwamba una jambo Fulani kwa sababu ya uchawi . Hivyo nikawa najifanya kama namuonea huruma mke wa K lakini moyoni nilikuwa nataka afukuzwe mimi nikakae, pale.
Kuna kitu kimoja kilikuwa kinaniumiza moyo. Mke wa K alikuwa na ujauzito wa kama miezi mitano hivi. Sikutaka mwanamke huyo azae na K kwa sababu nilijua, angezaa na K mtoto angekuwa kiunganishi kwao, Mimi nilitaka K akisha achana na mke wake, basi iwe ndio moja kwa moja na kusiwe na chochote cha kuwaunganisha. Hivyo nikaanza kupanga njama za kuharibu ujauzito wa mke wa K kwa kutumia uchawi.
Suala hili nikalifikisha kwa Mungu Wa Kabili. Mungu wa Kabili akaniambia nitakupa dawa utaenda kutega kwenye mlango wake. Mti huo ni wa ajabu sana. Jina lake linafanana na jina la moja kati ya wilaya zilizopo kusini mwa Tanzania bara.
Baada ya kupewa dawa hiyo, nikafanya ujanja nikaenda kuitega kwenye mlango anaoutumia kupita. Alipo ruka mimba ikatoka. Kutoka kwa mimba ya mke wa K kulinipa sababu ya kurudi kwa mganga kwa ajili ya kuwatenganisha kabisa K na mke wake. Nilijua, majirani wangesema K kamuacha mke wake kwa sababu mke ana matatizo ya uzazi.
NAMTENGANISHA K NA MKE WAKE.
Nikarudi kwa mganga ili tufanye uchawi wa kumtenganisha K na mke wake. Mganga alichukua nyoya la ndege ambaye simfahamu jina lake, pamoja na dawa ambazo sikuzijua pia, akachukua majina ya K na mke wake, akaenda kuchoma jalalani.
Alipomaliza hapo, tukaenda kaburini, kwa ajili ya kuuzika rasmi uhusiano wa K na mke wake. Baada ya kuzika uhusiano wa K na mkewe, yalifanyika matanga kwa ajili ya kuomboleza “kifo’ cha ndoa ya K. Mganga alisema, kitu kilicho kufa, kinastahili kupewa maziko ya heshima. Usipofanya hivyo, roho ya kitu hicho itakusumbueni.
Niliporudi mjini nikakuta mke wa K kaondoka kwake, kahamia kwa dada yake. Mimi nikahamia moja kwa moja kwa K nyumba niliyokuwa nimepangiwa Kimanga nikamuweka mdogo wangu wa kiume.
NAANZA KUFUATILIWA NA NDUGU WA MKE WA ‘K’.
Ndugu wa mke wa K hawakufurahishwa na kuachana kwa K na mkewe, hivyo wakafanya kila juhudi kuwapatanisha, lakini msimamo wa K ulikuwa ni ule ule, kwamba hataki tena kuwa na mke wake na ameamua kuishi na mwanamke mwingine ambae ni mimi. K alikataa hata kushiriki kwenye vikao vya usuluhishi. Ndugu wote wa upande wake na upande wa mke wake wakawa wamemsusia K.
Watu wawili hawakutaka kukubaliana na matokeo. Nao ni baba wa mke wa K, pamoja na kaka mkubwa wa mke wa K. Watu hawa waligundua kilichotokea kati ya K na mke wake sio hali ya kawaida bali ni nguvu za ushirikina. Hivyo wakaamua kutafuta suluhisho kwa waganga. Walipo zunguka kwa waganga, hawakufanikiwa, hadi wakakata tamaa kunidhuru kwa njia ya uchawi.
Mwisho wa siku wakaamua, kunikodia majambazi, waje wanipige risasi. Walijua mimi ndio kikwazo kwa mtoto wao kurudiana na mume wake, hivyo njia pekee ikawa ni kifo tu.
Nilisurika kuuwawa na majambazi zaidi ya mara saba. Wakati huo Mungu wa Kabili alikuwa Lubumbashi nchini Kongo kwa shughuli zake. Alipo rejea nikamfuata kwa ajili ya kuomba ulinzi wake.
Kuna mnyama mmoja wa mwituni, ana ndimi mbili, yani ulimi wake una ndimi mbili, Mungu wa Kabili akatafuta ulimi wa mnyama huyo, mavi ya chatu pamoja na dawa zingine anazo zijua, lengo lake likiwa ni kuwatenganisha na kuwafarakanisha baba na kaka wa mke wa K ili wasipate nafasi ya kukaa pamoja na kunifuatilia.
Halafu baada ya hapo, akaagiza nipeleke mchanga wa kwenye kaburi la mtu aliyepita duniani bila kuonekana, ili anitengenezee dawa ya kuwafunga adui zangu wasinione. Pamoja na hivyo, akanipa hirizi iliyo tengenezwa kwa Mti Mkuu wa Wachawi.
Katika ulimwengu wa wachawi, mtoto aliye kufa akiwa tumboni kwa mama ake. Huitwa mtu aliyepita duniani bila kuonekana.
Nilivyo mpelekea udongo wa kwenye kaburi la mtu aliye pita duniani bila kuonekana, mganga akauchukua akafanya ulozi wake, halafu tukaenda wote hadi mtoni, akaenda akatega ndumba zake, pale, kesho yake tukakuta chura amenasa pale.
Wachawi wana amini, roho za watoto wanao kufa kabla hawajazaliwa, huwa zinaenda kuishi mtoni kama Chura. Lakini sio chura wote wapo hivyo, ni baadhi. Waganga wana utaalamu wao wa kujua chura yupi anahusika hapo.
Basi kaka na baba wa mke wa K, walikosana kwa ugomvi mkubwa, kiasi mtoto akawa anamtukana baba ake mzazi tusi la mama. Na kuhusu vitisho vya majambazi havikutokea tena
NATUMIA UCHAWI KUOKOA UHUSIANO WA KAKA ANGU.
Kaka angu ambaye nimempita miaka mitano, alikuwa anaishi kwenye nyumba ambayo K alinipangia. Nyumba hii ilikuwa maeneo ya Tabata Kimanga. Kaka angu alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke ambaye alikuwa Baa Medi kwenye bar inaitwa Mawenzi Garden.
Alimuachisha kazi ya ubaa medi baada ya mimi kumuwezesha kiuchumi kutokana na hela na mali nilizo hongwa na K pamoja na kumpa mradi mmoja wa K ausimamie. Mdogo wangu alimpenda sana mwanamke huyo .
Ila tatizo moja la mwanamke huyo, alikuwa na tabia ya umalaya. Umalaya ulikuwa kwenye damu yake .
Basi siku moja mdogo wangu alikuja kwangu kunishitakia kuhusu tabia ya wifi yangu. Mdogo wangu alikuwa anampenda sana mwanamke huyo, na alikuwa hawezi kumuacha kwa sababu yoyote ile, ila alikuwa anamuumiza sana kwa sababu ya tabia yake ya umalaya.
“ Ninampa kila kitu huyu mwanamke, ninampa hela, nimemfungulia biashara, nimempa gari, nawasomesha wazazi wake na kusaidia familia yake,. Lakini haridhiki tu, mwisho wa siku anatumia hela ninazo mpa kuhonga wanaume wengine.. ( HELA , GARI NA VITU VYOT AMBAVYO MDOGO WANGU ALIKUWA AKIMPA WIFI YANGU, VILIKUWA MALI YA K ALIZO CHUMA KWA JASHO LAKE NA MKE WAKE)
Nilimuonea huruma sana mdogo wangu, na nikaamini sio akili yake ila atakuwa amerogwa na mwanamke Yule. ( UNAJUA UKIWA MSHIRIKINA, KILA KITU UNAKUWA UNAAMINI KIMESABABISHWA NA USHIRIKINA )
Nikamwambia mdogo wangu usijali, kesho nitakwenda Bagamoyo kwa mtaalamu wangu, nitamuelezea tatizo lako, halafu nitamsikia atakacho niambia, nitakujulisha, ila usijali kama mwanamke huyo amekufanyia mambo ya Kiswahili, itajulikana tu na utakuwa huru.
Nilipo fika kwa Mungu wa Kabili, nikamueleza kila kitu, akaniomba majina ya mdogo wangu pamoja na jina la huyo wifi yangu, akatazama kwenye radar zake, halafu akacheka sana.
Mungu wa Kabili akaniambia, hakuna haja ya kumfunga mwanamke huyu. Huyu mwanamke ana sumbuliwa na damu ya umalaya. Umalaya upo kwenye damu yake. Hata tukimfunga kwa mdogo wako, tutakuwa tunajisumbua tu, atampenda sana mdogo wako, lakini atatoka nje tu kwa wanaume wengine. Hapa cha msingi, afanyiwe dawa ya kumfanya aache umalaya.
Mungu wa Kabili akachukua dawa moja inaitwa GEGEZI. Hii Gegezi ina ukubwa kama tunda linaitwa DADANSI na ina mibamiba.
Halafu akachukua dawa nyingine ambayo ni chakula cha ndege mmoja wa porini. Ndege huyo simkumbuki jina lake, ila ni mweusi, ana mdomo mrefu, ndege huyu akilia, vinyonga wote waliopo katika eneo hilo wanakimbia, huwa anakula vinyonga pia.,
Sasa ndege huyu huwa anakula majani ya mti Fulani wa porini ambao nimeusahau jina lake, hayo majani ndio ambayo Mungu wa Kabili aliya chukua.
Kitu kingine akachukua majani Fulani hivi, hayo majani ndio majani pekee yanayo liwa na mnyama wa porini ambae chakula chake kikuu ni nyama.
Pamoja na dawa hizo akachanganya na dawa zake nyingine ambazo sikuweza kujua ni dawa gani, halafu akaagizwa itafutwe minyoo ipatayo saba. Vito vyote hivyo vikaunguzwa pamoja kwenye chungu, hadi vikawa unga unga halafu vikachanganywa na mafuta ambayo sikujua ni mafuta ya kitu gani.
Mungu wa Kabili akanipa dawa hiyo akaniambia mpelekee kaka ako. Mwambie akiwa anafanya mapenzi na huyo mwanamke wake, afanye ujanja wake, achovye kidole chake kwenye hiyo dawa halafu akichomeke kwenye uke wa mwanamke huyo.
Tangu siku hiyo, mwanamke huyo hatokuwa Malaya tena . Nikafanya kama alivyo nielekeza na tangu mdogo wangu afanye hivyo, sikuwahi kumsikia tena akinipa kesi za wifi yangu, zaidi ya kumsifia mpenzi wake ametulia. Mwisho wa siku walifunga ndoa na kuzaa watoto.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search