Wednesday, 9 August 2017

HIVI NDIVYO SIMBA ILIVYOTAMBULISHA WACHEZAJI WAKE WAPYA KWENYE SIMBA DAY

Mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Simba dhidi ya Rayon Sport kutoka Rwanda imemalizika huku Simba ikipata ushindi wa goli 1-0.
Lengo kubwa la mchezo huo lilikuwa ni kutambulisha kikosi cha Simba kitakachocheza mashindano mbalimbali msimu ujao. Imekuwa desturi kwa Simba kutambulisha wachezaji wao siku ya August 8 kila mwaka huku siku hiyo ikijulikana kwa Simba Day.
Goli pekee la mchezo huo limefungwa na kiungo mshambuliaji Mohamed Ibrahim dakika ya 16 kipindi cha kwanza akiwa amepokea pasu kutoka kwa Emanuel Okwi na bao hilo kudumu kwa dakika zote za mchezo.
Haruna Niyonzima ndio amekuwa gumzo kwenye Simba Day kutokana na namna ambavyo amesajiliwa lakini kubwa akiwa ametoka kwa watani wao wa jadi Yanga.
Mashabiki wengi wa Simba walikuwa wakisubiri kwa hamu utambulisho wa Niyonzima kutokana na kuwepo kwa mpishano wa maneno wengine wakidai amesaini Simba huku wengine wakiwa hawaamini.
Vigogo wa Simba walimsaini Niyonzima mapema lakini iliwalazimu kusubiri hadi mkataba wa mchezaji huyo na Yanga umalizike kabisa ndio wamtangaze rasmi kuwa ni mchezaji wao ili kukwepa usumbufu wa kumtangaza mchezaji akiwa bado ana mkataba na timu yake ya awali.
Miongoni mwa wachezaji wapya waliotambulishwa ni Aishi Manula, Said Mohamed ‘Nduda’, Erasto Nyoni, John Bocco, Paul Mukaba, Ally Shomari, Yusuph Mlipili na Salim Mbonde.
Wengine ni Nicolas Gyan, Shomari Kapombe Emanuel Okwi na Haruna Niyonzima.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search