Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
George Simbachawene ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya
kutajwa katika ripoti za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na
Almasi iliyoonyesha namna serikali lilivyopoteza matrilioni ya fedha
kutokana na sababu mbalimbali.
Waziri Simbachawene ameandika barua hiyo muda mfupi tu tangu Rais
Magufuli alipowataka viongozi wote aliowateua na wametajwa katika ripoti
hiyo wakae pembeni ili kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.
Mbali na Simbachawene, wengine waliokuwa wametakiwa kukaa pembeni ni
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin
Ngonyani ambaye alituhumiwa kutotekeleza majukumu yake kikamilifu
alipokuwa akifanya kazi katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
lenye dhamana ya kusimamia madini.
Mbali na Ngonyani, mwingine ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakim
Maswi naye amepaswa kupisha uchunguzi ambao Rais ameagiza ufanywe na
vyombo vya ulinzi na usalama haraka iwezekanavyo.
Rais Dkt Magufuli ametoa maagizo hayo leo alipokuwa akipokea ripoti hiyo
ya uchunguzi wa madini kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye
aliipokea jana kutoka katika kamati zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job
Ndugai.
Akiyasema hayo, Rais Magufuli aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama
kufanya uchunguzi kwa wateule wake waliotajwa tajwa katika ripoti hizo
lakini akasema kuwa, uchunguzi hauwezi kufanyika wakati kiongozi akiwa
bado yupo serikali. Baada ya kusema hivyo, Rais Magufuli alisema
anaamini kuwa viongozi hao watakaa pembeni kupisha uchunguzi.
Hafla hiyo ya kukabidhi ripoti ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali
akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai,
Wenyeviti wa kamati mbili za Tanzanite na Almasi, Dotto Biteko na Mussa
Azzan Zungu ambao wote ni wabunge.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na viongozi mbalimbali wa vyombo vya
ulinzi na usalama, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa jumuiya ya
wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na viongozi waandamizi wa serikali.
Rais Magufuli ameendelea kuwasisitiza watanzania kuwa wazalendo kwani
rasilimali za nchini za nchi zinaibiwa na watanzania wanazidi kubaki
katika umasikini uliokithiri.
Baada ya kuhutubia, Rais Magufuli alikabidhia nakala za ripoti hiyo kwa
viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili vianze kufanya kazi mara
moja na sio kuendelea kukaa huku mali za watanzania zikiibiwa
Post a Comment