Thursday, 7 September 2017

Kampuni iliyomuhonga Kigogo almasi ya Bilioni 450, Kikwete alikataa


WAFANYAKAZI WA WILLIAMSON DIAMOND LTD.
KAMATI Maalum ya Bunge iliyochunguza mwenendo wa almasi nchini, imeibua mambo mazito kwa kumtaja "kiongozi mkubwa wa serikali" kuwa alipewa zawadi ya almasi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 200.
Kiasi hicho cha fedha ni sawa na Sh. bilioni 448, kwa mujibu wa viwango vya kubadilishia fedha jana.
Hayo yamo kwenye ripoti hiyo iliyowasilishwa jana na kamati hiyo katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jana.
Kampuni ambayo inatuhumiwa kumhonga kigogo huyo kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni Williamson Diamond Ltd inayochimba almasi katika mgodi ulioko Mwadui mkoani Shinyanga.
"Kamati yetu pia kwenye kutekeleza majukumu yake ilibaini kuwa kuna kiongozi mkubwa wa serikali alipewa zawadi ya almasi ambayo kwa sasa ina thamani ya Dola za Marekani milioni 200," alisema mwenyekiti wa kamati maalum ya Bunge iliyochunguza almasi, Azan Mussa Zungu.
Mwishoni mwa Bunge la Bajeti, Spika Job Ndugai aliunda kamati maalum mbili kuchunguza na kutoa ushauri bora kwa serikali kuhusu uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya almasi na Tanzanite nchini.
Matukio ya viongozi wakubwa kupewa zawadi za vito si nadra kutokea nchini. Rais wa awamu ya nne, Jakaya 'JK' Kikwete aliwahi kukataa kupokea zawadi ya dhahabu kutoka kwa kampuni ya Nyamigogo GVH ya mkoani Geita.
Taarifa ya Ikulu ya Novemba 11, 2013 ilisema kampuni hiyo ilitaka kumkabidhi JK gramu 227 za dhahabu safi wakati alipotembelea mgodi wake.
JK aliitaka Nyamigogo GVH kuuza dhahabu hiyo na fedha zitakazopatikana zisaidie watoto yatima, taarifa hiyo ilisema zaidi.
Alikabidhiwa zawadi hiyo wakati wa sherehe za uzinduzi wa kinu cha uchenjuaji dhahabu cha kampuni hiyo nje kidogo ya mji wa Kharuma wilayani Nyang'wale mkoani Geita.
Kiasi hicho cha dhahabu kilikuwa na thamani ya Sh. milioni 16 katika soko la dunia wakati huo.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, taarifa ya Ikulu ilisema, Kikwete aliuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa watoto yatima.”
JK alizindua mgodi huo ikiwa sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Geita, moja ya mikoa minne ambayo aliianzisha mwaka 2012. Mikoa mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.
Aidha, wakati wa ufunguzi wa mgodi wa dhahabu wa Golden Pride, Nzega mkoani Tabora uliokuwa unamilikiwa na kampuni ya Resoluted Mining Limited ya Australia Februari 7, 1999 Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa alionekana akipokea pande la dhahabu kama zawadi.
Kutokana na ‘zawadi’ hiyo, baadhi ya wanasiasa akiwamo Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) wakati huo, Augustine Mrema, walitaka dhahabu hiyo irudishwe na kuuzwa ili fedha zake zisaidie kutatua matatizo ya wananchi.
Siku tatu baada ya mjadala huo kuibuka katika mdahalo ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kuhusisha vyama vya siasa, Mkapa alitangaza kurudisha dhahabu hiyo na kusema hakupewa kama zawadi.
Kamati za Bunge jana ziliweka hadharani ripoti zake na zilizoonyesha pia madudu ya kutisha yaliyofanywa na viongozi wa serikali yaliyosababisha serikali kupoteza mabilioni ya shilingi.
Ripoti za Kamati hizo zimewagusa baadhi ya mawaziri waliopita ambao zimependekeza wahojiwe na mawaziri wawili wa sasa ambao ripoti hizo pia zimependekeza wahojiwe na kuwajibishwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, ni mmoja wa mawaziri waliotajwa katika ripoti za kamati zote mbili zilizosomwa jana.
Mwingine aliyetajwa na ambaye imependekezwa awajibishwe ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Mhandisi Edwin Ngonyani ambaye wakati madudu yanafanyika alikuwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi na baadaye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye alitajwa kwenye ripoti ya mchanga wa dhahabu (makanikia) Juni mwaka huu, pia ametajwa tena kwenye ripoti za kamati zote mbili kuwa ni miongoni mwa watu wanaostahili kuhojiwa kwanini walizembea na kuisababishia serikali hasara.
Mwingine aliyetajwa kuzembea na kuisababishia serikali hasara kwa mujibu wa uchunguzi huo ni Prof. Abdulkarim Mruma, ambaye ndiye aliongoza kamati ya kwanza ya kuchunguza makinikia iliyoundwa na Rais John Magufuli.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, ni mmoja wa watu waliohojiwa na kamati maalum ya kuchunguza almasi ambayo imemtia hatiani kwa uzembe na kuisababishia serikali hasara kubwa.
Waziri mwingine mstaafu aliyetajwa ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, ambaye kamati imependekeza ahojiwe kwa nini alizembea na kuisababishia hasara serikali.
Prof. Muhongo alitumbuliwa mara baada ya kamati ya kwanza ya makinikia kuwasilisha ripoti yake Ikulu jijini Dar es Salaam, huku ikionyesha namna serikali ilivyopata hasara kwenye biashara ya dhahabu.
Uwasilishaji wa ripoti hizo ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika Ndugai, wabunge, makatibu wakuu na baadhi ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
MADUDU MENGI
Wa kwanza kuwasilisha ripoti yake alikuwa Mwenyekiti wa kamati iliyochunguza almasi, Zungu, ambaye alisema kamati ilichambua nyaraka mbalimbali na mahojiano na watendaji mbalimbali wa serikali.
Alisema kamati yake imebaini madudu mengi kwenye biashara hiyo na uzembe mkubwa uliofanywa na baadhi ya watumishi wa umma walioaminiwa kusimamia rasilimali za taifa.
Alisema kamati ilibaini kuna watalamu wawili tu nchini wa kuthamini madini wakisaidiwa na wengine ambao ni wa kigeni, hali inayosababisha taifa kupata hasara.
Alisema wathamini hao wawili wamefanya kazi hiyo peke yao kwa zaidi ya miaka 18 na hakuna hatua zozote ambazo serikali ilichukua kwa ajili ya kuongeza wataalamu ili kuokoa udanganyifu unaofanywa kwenye sekta ya madini hayo.
Alisema kamati yake ilibaini kuna udanganyifu mkubwa kwenye almasi inayosafishwa nje kwa kuwa kuna uwezekano wa kusafishwa nchini na wanaoipeleka nje wanafanya hivyo ili kuiibia serikali.
Alisema kampuni ya Williamson Diamond Ltd (WDL) ilipata msamaha mkubwa wa kodi wa vifaa vya kazi wakati ilikuwa ikinunua vifaa chakavu na kutaja kwenye vitabu kuwa imenunua vifaa vipya.
Alisema mgodi huo ulikuwa ukiibambika serikali gharama kubwa za uendeshaji lakini wajumbe wa bodi hawakuwa wanajadili ubambikaji huo, akitolea mfano kununua mitambo chakavu na kuandika kuwa ilinunuliwa ikiwa mipya.
Alisema kuna haja serikali kuangalia upya matumizi ya misamaha ya kodi kwenye migodi yote kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiitumia vibaya.
Mwenyekiti wa kamati iliyochunguza Tanzanite, Doto Biteko, alisema biashara ya madini hayo imetawaliwa na wizi na usiri mkubwa, akieleza kuwa ni asilimia 20 tu ya Tanzanite yote inayozalishwa nchini ndiyo inaingia kwenye mfumo wa kulipa kodi na asilimia 80 zinatoroshwa na kuuzwa nje ya nchi.
Alisema kwa mujibu wa takwimu kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita, imebainika mauzo ya Tanzanite duniani yalifikia Sh. trilioni 8.58 lakini taarifa ya mauzo ya Tanzanite nchini na kwa takwimu za Mamlaka ya Mapato (TRA), katika kipindi hicho mauzo ndani yalifikia Sh. bilioni 454.5 ikiwa ni asilimia 5.2 ya Tanzanite yote inayouzwa duniani.
"Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo, alitoa leseni ya ubia bila kushauriana na Bodi ya Madini na leseni hiyo ilikuwa na mazingira ya uharaka yasiyoelezeka kwani hakukuwa na vikao vyovyote vilivyokaa," Dotto alisema.
KINYUME CHA SHERIA
Mbunge huyo wa Bukombe (CCM) alisema leseni iliyotolewa na Prof. Muhongo ilikuwa inachanganya madini ya kawaida na yale ya vito jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Madini ambayo inataka leseni isichanganye aina ya madini hayo.
Alisema kampuni ya Sky Associate Ltd imekuwa ikihusika na utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na watumishi wa serikali waliopewa dhamana ya kulinda rasilimali hizo za taifa na mikanda ya kamera za CCTV zimepatikana na ushahidi upo.
Alisema kumekuwa na udanganyifu mkubwa sana kwenye takwimu za madini hayo kwa kuwa takwimu za Stamico na Tanzanite One zimekuwa zikitofautiana, hali inayoonyesha wamekuwa wakila njama za kutorosha madini hayo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hizo kabla ya kuzikabidhi kwa Waziri Mkuu, Spika Ndugai alisema Bunge linaunga mkono jitihada zilizoanzishwa na Rais Magufuli katika kulinda rasilimali za taifa na ndiyo sababu liliamua kuunda kamati hizo mbili.
Aliwashangaa baadhi ya watanzania wanaopewa nafasi za uongozi na wanaruhusu wizi na ufisadi kwenye rasilimali za taifa wakati wametokea kwenye familia za kimaskini.
"Hao wanaoandika mikataba wamesoma kwenye vyuo ambavyo na sisi tulisoma na unaweza kukuta hata tulikuwa tukiwazidi alama kwenye masomo... sasa inakuwaje watuandikie mikataba mibovu na tunasaini hivyo hivyo?" Alihoji Ndugai.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizipongeza Kamati hizo kwa kazi nzuri na kuahidi kuwa serikali itayafanyia kazi mapendekezo ya kamati zote mbili.
Alisema leo atakabidhi ripoti hizo kwa Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na ana imani kubwa mapendekezo hayo yote yatafanyiwa kazi kwa haraka.
"Ndugu zangu Tanzania tumebarikiwa kuwa na madini mengi sana, tena mengine yanapatikana hapa kwetu tu kama Tanzanite inayopatikana Mererani pekee, watanzania huu ni wakati wa kuwa kitu kimoja kulinda rasilimali zetu kwa maslahi ya watanzania wote," alisema.
Alisema kwa kuwa Rais Magufuli ameonyesha uzalendo kwa kuanzisha vita ya kulinda rasilimali za taifa, ni wajibu wa kila mtanzania kuunga mkono jitihada hizo.
Katika hafla hiyo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema kamati hizo zimefanya kazi kubwa, hivyo alitaka serikali ifanyie kazi mapendekezo yaliyotolewa.
Aliwasifu wajumbe wa kamati hizo kwa kuweka kando itikadi za vyama vyao na na kufanya kazi kwa maslahi ya taifa

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search