Monday, 4 September 2017

MAHAKAMA YA JUU NCHINI KENYA YAFUTA MATOKEO YA URAIS YAAMURU TUME KURUDIA UCHAGUZI NDANI YA SIKU 60
Mahaka ya Kenya Umefuta Matokeo ya Urais yaliyompa Ushindi Uhuru Kenyatta Dhidi ya Raila Odinga uliofanyika mwezi wa nane...Mahakama umeamuru uchaguzu urudiwe ndani ya siku 60

Mahakama ya Juu nchini Kenya imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mapema mwezi uliopita katika uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa na muungano wa upinzani National Super Alliance (NASA).
Uamuzi huo ulitangazwa na Jaji Mkuu David Maraga jijini Nairobi leo asubuhi akisema kati ya Majaji sita waliosikiliza kesi hiyo, wanne walifikia uamuzi kuwa uchaguzi huo haukufanyika kwa mujibu wa Katiba na sheria za Uchaguzi nchini humo.
Aidha, wamesema Uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 2017 haukuandaliwa kwa mujibu wa katiba na sheria hivyo kulikuwa na udanganyifu na haukuwa huru na haki hivyo matokeo yake ni batili.
Uamuzi huo ni ushindi kwa upande wa upinzani ambao uliwasilisha mahakamani kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Hatua hii ya Mahakama ya Juu inamaanisha kuwa, Uchaguzi Mkuu mpya utafanyika tena baada ya siku 60 kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.
Uamuzi huu umeleta furaha kwa wafuasi wa muungano wa upinzani NASA, waliokuwa wanasubiri uamuzi huu kwa hamu kubwa.
Wakili wa rais Uhuru Kenyatta, Abdulnasiir Muhammed amepinga uamuzi wa Mahakama na kusema kuwa, ulikuwa ni uamuzi wa kisiasa uliofikiwa.
Kwa upande wake Mgombea urais wa upinzani Raila Odinga amesema leo ni siku ya kihistoria kwa Kenya na kwa Afrika, kwa uchaguzi wa rais kufutwa imetoa mfano bora.
Naye Makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka amesema mahakama imekuwa mfano mwema kwa Afrika na dunia nzima na hawana imani kwamba tume ya uchaguzi ya sasa kama inaweza kuandaa uchaguzi huru na wa haki.
Kenyatta mwenye umri wa miaka 55, alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo wa Agosti 8 kwa kupata asilimia 54 ya kura.
Kulizuka vurugu za hapa na pale kati ya polisi na waandamanaji wanaomuunga mkono Odinga na kusababisha vifo vya watu 21.
Licha ya kuupongeza uamuzi huo wa mahakama ya juu, Odinga ametoa wito wa wale walioharibu uchaguzi wa Agosti 8 kushtakiwa na kupewa adhabu kwa mujibu wa sheria.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search