Tuesday, 12 September 2017

Mgogoro wa Maalim Seif na Prof Lipumba wahamia Bungeni

Mvutano kati ya wabunge wa CUF umejitokeza ndani ya Bunge baada ya Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya kupeleka majina ya viongozi wapya wa chama hicho ndani ya Bunge.
Jana asubuhi Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson mara baada ya matangazo ya wageni, alisoma taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai ikionyesha safu mpya ya uongozi wa wabunge wa chama hicho.


Dk Tulia alisema Spika alipokea taarifa juu ya uchaguzi wa viongozi hao iliyopelekwa kwake na Sakaya.
Kwa mujibu taarifa hiyo Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma kuwa mwenyekiti wa wabunge chama hicho bungeni.


Alisema katibu wa wabunge hao ni Rukia Kassimu wakati mnadhimu wao ni Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia.
Hata hivyo, Mbunge wa Malindi ambaye ndiye aliyekuwa mnadhimu kabla ya majina mapya kutangazwa, Ally Salehe aliomba mwongozo wa Spika akisema kuwa wabunge wa chama hicho wakiwa zaidi 40 walifanya uchaguzi na kuchagua viongozi wao.


Alisema baada ya wabunge nane kufukuzwa kuna nafasi zilibaki wazi ambazo walizijaza kwa kuwachagua wabunge wengine.
Alisema katika uchaguzi huo nafasi ya uenyekiti iliyoachwa wazi na Riziki Ng’wali walimchagua Mbunge wa Temeke, Abdalah Mtolea.
Alihoji ni nani anaamua kuhusu uongozi wa wabunge bungeni kama ni wabunge wachache ama walio wengi.


Pia, alihoji inakuwaje kunakuwa na safu mbili za uongozi katika uchaguzi uliofanywa na wabunge wachache.
Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia alisema Spika amepokea taarifa ya viongozi hao lakini hajapokea taarifa ya uchaguzi wa upande wakina Ally Salehe juu ya uchaguzi huo.
“Hiki chama cha CUF kinaonekana kuwa kina makundi mawili. Kundi moja limefanya uchaguzi halijamtaarifu Spika. Kundi lingine limefanya uchaguzi likamwambia Spika,”alisema.


“Hii taarifa imesomwa kama ilivyoletwa hapa mezani. Mtakapofikia mahali mtataka kuzungumza na Spika mtafanya hivyo lakini Bunge hili hatutaweza kujadili jambo hilo sasa hivi,”alisema.
Alisema hata hiyo taarifa nyingine ya uchaguzi Spika atakavyoamua itapelekwa ndani ya Bunge na kwamba hawezi kuelezea kuwa linaruhusiwa ama haliruhusiwi kwa sababu chaguzi za ndani ya CUF hazijafanyiki ndani ya Bunge.


Wakizungumza nje ya Bunge kwa nyakati tofauti kuhusu uchaguzi huo, wabunge hao walionekana kila mmoja kuvuta kamba upande wake.
Mtulia alisema kuwa awali walikuwa hawamtambui Profesa Ibrahim Lipumba kwa sababu alikuwa amejiuzulu lakini hivi sasa kutokana na vyombo vyote vya sheria na Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), na Bunge kumtambua yeye hana sababu ya kutokubali.


“Kuendelea kung’ang’ania kuwa humtambui Profesa Lipumba ni kujisumbua wakati vyombo vyote vinamtambua,”alisema.
Alisema kuwa CUF wote wanaamini kuhusu Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) kwa sababu walianza pamoja na waliona manufaa kwa vyama vilivyojiunga na umoja huo.
“Lakini ukiwa na CUF katika Ukawa ambayo ni dhaifu itakufanya uwe na kazi ya kukibeba hiki. Viongozi wahakikishe kuwa mgogoro ndani ya CUF unamalizika ili kuwa na CUF moja,” alisema.


Akizungumzia kuhusu kuchaguliwa kwake kushika nafasi hiyo, alisema anajisikia vizuri na kwamba atajitahidi kutenda haki kwa wabunge wote wa CUF.
Ally Salehe alimlaumu Spika kwa kuwaunga mkono upande wa Profesa Lipumba kwa madai kuwa anazidi kukivuruga chama hicho.


Alisema hakupata taarifa za kufanyika kwa uchaguzi huo na kwamba hata angezipata asingeenda kwa sababu waliouitisha walishafukuzwa ndani ya chama.
Kwa upande wake Sakaya alisema hawakuwashirikisha wabunge wanaomuunga mkono katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif katika uongozi kwa sababu walishasema hawatashirikiana nao.


“Sisi tulifanya uchaguzi wabunge 10, saba walioteuliwa juzi na sisi tuliobakia na hatukuwachagua kwa sababu walisema hawatashirikiana nasi,”alisema.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search