Friday, 29 September 2017

NATAKA KUZAA-EPISODE YA NANE


MTUNZI: JENNIFER ALPHONCE
SIMU: 0683777152
SEHEMU YA NANE
Ilikuwa ni siku ya jumamosi nilitoka nyumbani eneo la Mbezi beach na kuelekea Mabibo hostel kwa ajili ya kusuka. Nilikuwa nikipendelea sana kusuka kwenye saluni za Mabibo hasa hasa saluni flani hivi ambayo nilikuwa nimeizoea sana walinihudumia kwa ucheshi na mara zote walikuwa wananishauri jinsi ya kutunza nywele zangu na mtindo mzuri wa kusuka mara zote nilipenda kusuka kwenye saluni hiyo.
Na siku hiyo niliamua kwenda kushonea weaving refu.
Niliondoka nyumbani nikiwa nimevaa gauni langu la rangi ya maruni lililokuwa fupi kidogo, jepesi na mikono yake ilikuwa ni miembamba sana, chini nilivaa viatu vya wazi.
Sikutaka kuondoka na gari niliamua kupanda usafiri wa jumuiya.
Nilifika Mabibo mida ya saa nane nikaelekea dukani, nikanunua weaving na baada ya hapo nikaelekea saluni kwa ajili ya kusuka.
Nilimaliza muda ulikuwa umeenda kidogo kiasi kama saa kumi na moja za jioni baada ya hapo niliamua kwenda kumsalimia Monica chumbani kwetu kwa maana hakuwa ameondoka kwa ajili ya likizo. Watu wengi hawakuwepo mule ndani nafikiri asilimia kubwa ya watu walikuwa wameondoka kwa ajili ya likizo.
Nilienda moja kwa moja hadi chumbani kwetu niligonga sana lakini mlango haukufunguliwa, nilijaribu kumpigia simu Monica hakuwa akipatikana sikujua alikuwa ameelekea wapi hata hivyo haikuwa na umuhimu sana niliamua kutoka zangu na kurejea nyumbani.
Nilipofika nje ya block yetu nilishangaa kuona giza limetanda kulikuwa na wingu zito lililoashiria kwamba mvua itanyesha muda si mrefu nilishangaa sana.
“Hizi mvua za ajabu ajabu zinatokea wapi dakika mbili tu kuingia ndani na kutoka ndiyo wingu limejaa hivi, eenh!” Nilishangaa.
Nilipiga hatua za haraka haraka kwa ajili kuondoka wala sikufika mbali mvua ilianza kunyesha kwa nguvu zote kana kwamba ilikuwa inazuia nisiondoke.
Mvua kubwa ilinyesha radi zilianza kupiga na upepo mkali ulivuma nilikuwa nikitembea kwa shida nilianza kuogopa kila mtu alikuwa akikimbia na kujificha, nilishindwa niende wapi nilibakia tu nimechanganyikiwa nilikuwa sijui hata naelekea wapi.
Mara gafla nakutana na Frank akitokea getini akiingia ndani alikuwa ameshika mwamvuli na alikuwa akitembea kwa hatua za haraka haraka.
“Frank..” Niliita baada ya kuonyesha dalili za kutaka kunipita.
“Sociolah unaenda wapi?”
“Naenda nyumbani.” Niliongea kwa kutetemeka.
“Na mvua hii..? Huko nje hakufai kabisa.”
“Sasa nitakaa wapi na kule chumbani kwetu hakuna mtu.”
Radi kubwa ilipiga nilikimbia kwa nguvu zote na kwenda kumkumbatia Frank nikijificha kwake.
“Aah, twende kule kwetu mvua ikiisha utaondoka.” Hata sikujishughulisha kufikiria hakika nilikuwa nikiogopa radi kuliko kitu chochote.
Tulitembea kwa hatua za haraka haraka huku nikiwa nimejifunika katika mwamvuli wa Frank hadi tulipofika kwenye block yao, Frank alikuwa akikaa block C.
“Unakaa Room namba ngapi?” Nilimuuliza.
“Nakaa room namba 415.” Alisema.
“Huuu…! Ghorofa ya tatu?”
“Ndio.”
“Sasa huko si karibu sana na radi.” Nilimuuliza, alicheka.
“Karibu na radi..?! Mmh!”
“Mimi ninaogopa radi jamani twende haraka.” Nilisena.
Tulipanda ngazi haraka haraka hadi kufikia ghorofa ya tatu, tuliingia umo nilishangaa kukuta hakuna mtu.
“Frank wenzio wako wapi?”
“Wameondoka wote wameenda likizo.”
“Aanh! We Frank si unatokea Morogoro? Kwanini hukuenda likizo sasa si hapo tu karibu?” Nilimuuliza.
“Kama ningeenda likizo unafikiri leo ungepata wapi hifadhi.” Aliongea kitu kilichonifanya nijisikie aibu sana niliishiwa namna ya kutaka kuendelea kuongea naye, maswali yote yaliniisha niliamua tu kunyamaza kimya.
Niliamua kutoa simu kwa ajili ya kumpigia mama ili nimwambie nimekwama Mabibo kutokana na mvua na radi.
Lahaulaa…!!
Simu ilizima.
“Mungu wangu nitatoaje taarifa nyumbani?” Nilibaki tu nimeshangaa.
“Hauna chaja?”
Nilifungua pochi yangu na kutoa chaja yangu, chaja yangu haikuwa ikitumia USB niliichomeka na kuanza kuchaji. Hazikupita dakika mbili umeme ulikatika.
“Ooh my God! Niliishiwa puimzi nilibaki tu nimesimama uko chumbani kana kwamba sijui nifanye nini.
“Nitafanyaje Frank?”
“Hauna USB?” Aliniuliza.
“Si unaona kabisa chaja yangu haina USB.”
“Basi pole.” Alisema.
“Ooh my God….!”
“Bahata mbaya hata mimi chaji yangu haina USB ningekuunganishia kwenye kompyuta yangu ungechaji.”
“Ooh, usiongee basi.” Nilishikwa na hasira.
“Aanh, ngoja ninyameze kimya.” Alivuta kiti na kukaa.
Nilienda kukaa pembeni ya kitanda na baridi lilianza kuwa kali na mvua haikuonyesha dalili ya kukatika. Nilianza kutetemeka, nguo yangu nyepesi ilinisaliti.
“Frank hauna koti?” Hatimaye nilishindwa kuvumilia. Aligeuka akanitazama na kisha akaachia tabasamu murua.
“Kwa kweli sina, ningekuwa nalo ningekuwa nimekwishakupa muda mrefu sana nakuona jinsi unavyoteseka na baridi.” Maneno yake yalinitia faraja ingawa hayakuweza kunisaidia.
“Ooh…” Nilikuwa nikitetemeka mpaka meno yakingongana.
Frank hakuwa mchafu kama alivyozoeleka, mavazi yake tu hayakuwa nadhifu, kitandani kwake palikuwa pamepangiliwa vizuri, shuka lililopauka rangi na mto ulionesha kwamba umechoka kulaliwa kwakuwa umetumika muda mrefu ulikuwa na kila dalili zote za kulegea pamoja na blanketi ama shuka zito zito.
“Chukua blanketi hilo ujifunike.” Alisema.
Nilivuta bila kuuliza nikalichukua nikalifunika, nikiwa nimekaa pembezoni mwa kitanda.
Giza nalo lilianza kuingia na umeme ulikuwa umekatika.
“Frank hauna hata tochi.”
“Hapana sina.”
Nilizidi kuchanganyikiwa sikuwa hata najua ni nini cha kufanya.
“Hebu niazime simu yako basi nipige simu nyumbani.” Alinipa.
Kwenye kioo cha simu yake Frank aliweka picha yake hakika alionekana ni mkaka mzuri na wa kuvutia kuliko wote niliowahi kukutana nao nilimfaninisha na ile picha hakika walifanana sana ingawa picha ilionekana kuwa na uzuri, nilimuangalia tu bila kukoma wakati Frank alikuwa akitazama nje, mvua nayo ilizidi kuongezeka.
Nilibonyeza namba za simu za mama yangu na kisha nikapiga.
“Halloo…”
“Hallo.”
“Mama.”
“Mwanangu Sociolah uko wapi? Tumekaa hapa tunamashaka sana juu yako, uko salama mwanangu.” Mama aliongea mfululizo.
“Niko salama mama lakini niko Mabibo nimeshindwa kuondoka huku kwasababu ya mvua.”
“Uko mahali salama mwanangu?” Nilimuangalia Frank.
“Ndio mama.”
“Naomba tu usirejee nyumbani maana huku njiani hapafai ni maafuriko kila kona kuna magari yamesombwa hapo na abiria, ningeweza kuja kukufuata mwanangu lakini nahofia usala wako na wangu pia, kama uko salama endelea kukaa mvua itakapoisha nitakuja mwenyewe kukuchukua mwanangu, sawa.” Mama aliongea na kisha simu ikakata ghafla, simu ya Frank nayo ilikuwa imezima chaji.
“Oooh…” Nilivuta pumzi na kuzishusha.
Baridi ilianza kuwa kali ilinilazimu kupanda kitandani kabisa, nilivua viatu vyangu na kisha nikasogea hadi mwisho wa kitanda.
Frank naye alianza kutetemeka nilimuonea huruma.
“Frank…” Nilimuita, alinigeukia.
“Unahisi baridi?”
“Hapana, kawaida tu.” Alijinyoosha kuonesha kuwa yuko kawaida ingawa nilimuona kabisa alikuwa akiteswa na baridi ile.
Radi ziliendelea kupiga nilizidi kupiga kelele.
“Sasa Socialah kelele za nini?”
“Wewe huoni radi zinapiga?”
“Kwahiyo ukipiga kelele ndiyo radi zinaacha?” Niliamua kunyamaza tu kimya.
Giza lilizidi kuwa zito mule ndani.
“Frank giza linazidi.”
Alinyanyuka bila kuongea chochote, alienda kufungua kabati lake na kisha kutoa kompyuta yake ndogo, alikuja na kuiweka pale kitandani, aliiwasha na kisha kuweka filamu ya kiamerika.
Filamu hiyo ilikuwa ikiitwa “Perfect Match.”
Kwa kiasi Fulani mwanga wa kompyuta ile ulileta mwangaza mule ndani.
“Sogea huko.” Aliniambia.
Nilisogea na kisha akaja kukaa pembeni yangu, nilimuonea huruma jinsi alivyokuwa akitetemeka.
“Chukua blanketi.” Nilimuambia.
“Hapana, usijali niko salama.” Aliongea.
Muda ulizidi kwenda filamu ilikuwa nzuri sana ambayo ilinifanya muda mwingine niachie kicheko cha nguvu, alikuwa akinitazama tu.
Muda ulizidi kwenda nilianza kuhisi kuchoka, usingizi ulianza kunivamia kwa kasi.
Nilishindwa kuendelea kujizuia, nilijikuta nimedondokea begani kwake na kisha nikadondokea moja kwa moja kwenye mapaja yake.
INAENDELEA………

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search