Sunday, 17 September 2017

NATAKA KUZAA-EPISODE YA NNE


MTUNZI: JENNIFER ALPHONCE
SIMU: 0683777152
SEHEMU YA NNE
Niliamshwa na pilikapilika za Melania na Fety pamoja na mwanachumba mwenzetu ambaye aliitwa Monica. Kiukweli nilikuwa nimechoka sana na nilihisi njaa,
“Kuna nini jamani mbona vuruguvurugu?”
Melania alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa, alikuwa akirusharusha nguo huku na kule, akipangua vitu na kuharibu mpangilio mzima wa chumba chetu.
“Kuna nini?” Niliuliza bila kujibiwa. Monica na Fety walikuwa kimya tu. Nilinyanyuka na kukaa.
Nilijinyoosha, “aanh…, nasikia njaa hatari.”
Melania alinigeukia na kunitazama kwa jicho kali,
“Unawaza kula tu huwazi hata ni nini kimetokea.”
“Si nimeuliza sipati jibu” Niliuliza kwa kupaniki.
“Kama hamtaki kunijibu mimi nifanyeje? Halafu matatizo yenu mimi hayanihusu kama nasikia njaa mbona nyie hamjali.” Fety alinikonyeza.
“Kwani kuna nini?” Niliuliza.
“Melania haioni simu yake.”
“ooh…” Kwakweli nilishituka sana.
Melania alikuwa akiipenda sana simu yake aina ya Samsung S6 ambayo alipewa zawadi na mama yake kwa kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar Es Salaam, ilikuwa ni simu nzuri na mpya kwahiyo sikushangaa kuona Melania amechanganyikiwa kuipoteza simu yake ile, ilikuwa ni nzuri sana hata mimi nilikuwa nikiipenda.
“Mmmh…. Patamu.” Nilisema.
Kiukweli Melania alikuwa amechanganyikiwa alitimuatimua vitu vyote na hakufanikiwa kuipata ilinibidi tu na mimi nijitahidi kumsaidia kuitafuta kwa maana alikuwa na hasira zisizo za kawaida
“Simu yangu nani kaiba jamani….?” Alikuwa akipiga kelele kama chizi.
“Jamani muda wa kipindi umekaribia mnaonaje tukaenda na tukarudi huku kuja kuitafuta, kwani mara ya mwisho ulikuwa nayo wapi?”
“Hata sikumbuki mimi nimechanganyikiwa kabisa hapa.” Melania alisema.
“Mimi nakumbuka ilikuwepo hapa jana.” Fety alisema.
“Basi itakuwepo hapahapa twendeni tukahudhurie kwenye kipindi turudi tuendelee kuitafuta.” Nilipendekeza.
Melania alikubali ingawa kwa shingo upande.
“Mimi bila simu yangu hata sijihisi kuwa niko vizuri.”
“mmh…” Nilitabasamu tu kwa pembeni maana angeniona ingekuwa ni kesi nyingine.
Tuliondoka na kwenda chuoni, muda wote alikuwa amekasirika hakutaka hata kujiongelesha na mtu.
Tulihudhuria kipindi hiko cha saa nne na baada ya hapo tulitoka na kuelekea Café kwa ajili ya kupata kifungua kinywa.
Melania aligoma kuagiza kitu chochote,
“Sasa utakaa bila kula jamani mbona unakuwa hivyo” nilimuongelesha Melania kwa namna ya kumshawaishi.
“Siwezi hata kula chochote, Sociolah simu yangu ni kila kitu kwangu najisikia vibaya sana bila kuwa nayo.”
“Usijali utaipata kula basi.” Nilimshawishi.
“Usinilazimishe kula Sociolah wewe kwasababu hujapoteza kitu hivi unafikiri ingekuwa ni ya kwako ungekula wewe, hebu niache usinisumbue.”
Kwa kweli nilinyoosha mikono juu kwa maana Melania alikuwa ni mtu ambaye asiyeshawishika, akiweka msimamo ni mgumu sana kuubadilisha.”
Fety alijaribu, “Kula basi hata kidogo”
Alinyanyuka tu na kuondoka hatukujua ameelekea wapi.
“Kuwa makini naye sana Sociolah akiwa na hasira huyo anaweza kummeza mtu.” Fety aliongea tulicheka.
Hazikupita dakika mbili Melania alirudi akiwa na glasi ya juisi, nilijua ni juisi ya maembe pamoja na ukwaju, juisi ambayo wote tulikuwa tukiipenda sana. Wakati huo nilikuwa nikinywa chai yangu na chapati, Fety alikuwa akinywa chai na maandazi.
Tukio la ghafla lilitokea na la kushangaza. Wakati Melania anafika mezani kwetu Frank naye alifika mezani kwetu, nilibaki na mshangao nilishindwa kuongea chochote.
“Samahani, mambo.” Frank alimsalimia Melania.
Nilimuona Melania hasira zikimzidia na ghafla alimmwagia ile juisi aliyokuwa nayo Frank, alimmwagia juisi yote kwenye shati lake jeupe la mikono mirefu ambalo alilivalia na suruali yake ya bluu, hakuchomekea na chini alikuwa amevaa malapa bila kusahau kofia yake.
Masikini ya Mungu roho iliniuma sana.
“Melania umefanya nini?” Melania aliniangalia tu kana kwamba anaongea na mimi kupitia macho na alipokwisha kumaliza aliondoka bila kusema chochote.
Frank alibakia amejiinamia tu nilimuonea huruma lakini nilishindwa cha kufanya.
Fety alitoka pale alipokuwa amekaa hadi karibu ya Frank
“Ndiyo ukome.” Alimuambia na kisha kuondoka.
Nilimuangalia Frank kwa huruma sana, nilishindwa kufanya chochote nikabeba begi langu na kisha kuondoka.
Nilikuwa nikimfuata Fety alipokuwa akielekea, tulienda hadi yalipokuwa madarasa yetu. Tulikaa eneo la Vibweta.
“Melania kwanini umalizie sasa hasira zako zote kwa Frank? Kakufanya nini lakini?” Hakunijibu kitu.
“Yani hasira zako za simu ndiyo unakuja kummalizia Frank ona ulivyomuaibisha mkaka wa watu jamani kwa nini lakini?” Alisonya tu.
“Angalia sasa sijui hata anakaa wapi masikini, umemmwagia juisi atatembeaje hapa chuoni kumbuka kwamba bado hatujamaliza vipindi kwanini lakini?” Niliendelea kufoka tu huku ikionesha kumba Melania hakuwa akinisikiliza hata kidogo.
“Shiit…. Fety tumchangie Melania hela akanunue simu, hata kwa kipindi kifupi tu, mimi nitatoa baadhi ya hela nilizokuwa nazo.” Niliongea kwa hasira bila kujua.
Nilifungua pochi yangu na kuanza kutafuta wallet yangu ambayo niliyokuwa nikihifadhi kiasi kikubwa cha hela. Hiyo ilikuwa ni hela ya matumizi ya wiki hili ambayo nilipewa na mama kiasi kama laki tano hivi.
Lahaula..! Haikuwepo!
Nilichanganyikiwa, nilitupa kila kitu kilichokuwepo kwenye pochi yangu na sikufanikiwa kuiona hiyo wallet.
“Mungu wangu wallet yangu iko wapi?” Kila mtu alishituka.
“Sioni wallet yangu jamani, nani kachukua?”
“Hapana.” Kila mtu alijibu.
“Shiit..” Nilishindwa cha kuongea hasira zilinikaba kooni.
“Nyie au tunaibiana sisi kwa sisi.” Fety alisema.
“Hata mimi naijiwa na mawazo hayo, haiwezekeni jana simu ya Melania imepotea leo wallet yako imepotea, kuna nini kati yetu?”
“Mungu wangu nitaishije mimi bila hizi hela, nitamuambia nini mama? Hakika hawezi kunielewa… Hawezi kunielewa kabisa.” Nilichanganyinkiwa si kidogo.
“Haaa….” Nilivuta pumzi na kushusha sikuwa nikielewa nini cha kufanya.
Niliingia darasani lakini hakika sikuambulia chochote.
Muda wa vipindi ulipoisha tulirudi bwenini kwetu Mabibo.
Kwa kweli sikuwa na nguvu za kumsaidia Melania kutafuta simu yake kila mtu alichanganyikiwa kwa kiwango chake.
Weekend nilirudi nyumbani, kwa kweli nilikuwa nashindwa jinsi ya kumuanza mama, naanzaje kumuomba mama hela.
Melania naye hakufanikiwa kuipata simu yake hakika alikuwa na majonzi sana.
Weekend kwangu ilikuwa chungu sana maana kila mara nilipokuwa nikijaribu kutafuta njia ya kupata hela nilishindwa, mwisho wa yote nilimkumbuka mpenzi wangu Patrick, niliamua kumtafuta.
INAENDELEA……..

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search