Saturday, 9 September 2017

NATAKA KUZAA-EPISODE YA TATU


MTUNZI: JENNIFER ALPHONCE
SIMU: 0683777152
SEHEMU YA TATU

Kwa kweli nilishindwa kujizuia kucheka, hakika kilikuwa ni kitu cha kuchekesha kuliko vyote ambavyo niliwahi kukutana navyo katika maisha yangu. Nilicheka sana lakini mwishowe niliingiwa na huruma,
“hivi huyu mtu ana akili kweli? Hajui kama anafanya haya mambo mbele za watu ona watu wanavyomuangalia.” Niliongea kwa sauti.
Fety na Melania walinigeukia na kunitazama wakiwa wameduwaa.
Kushoto kwangu alikuwa Frank, alikuwa akinywa chai pamoja na sahani ya matunda. Matunda yale yalikuwa ni mchanganyiko wa matikiti, machungwa, mananasi na maparachichi.
Lilikuwa ni tukio la kushangaza sana mtu kunywa chai na matunda. Kila mtu alikuwa akimtazama yeye na kumuongelea yeye. Tukio langu la kukaa naye mbele darasani na kisha kuongea naye mawili matatu lilikuwa kama gumzo pale chuoni. Watu wote walikuwa wakiongea wakimtazama na kisha walinigeukia mimi na kucheka, hakuonekana kujali kwani alikuwa akilamba michuzi ya matunda iliyokuwa ikichuruzika mikononi mwake bila haya wala aibu huku akipigia miruzi kana kwamba yuko peke yake.
“ooh gosh hii ni aibu.” Niliwaza.
Nilinyanyuka kwa hasira sana. Melania aliongea kwa kupaniki,
“kwani wewe ni ndugu yako?” Nilimuangalia kwa jicho kali na kisha nikaenda nilipokuwa nataka kwenda.
Nilijongea moja kwa moja hadi kaunta walipokuwa wakiuza vitafunwa, niliagiza chapati mbili na andazi moja na kisha nikampelekea mezani kwake nikamuwekea kwa hasira na  kurudi kukaa kwenye meza yangu.
Hata sikujua ni nini kilichonivuta kufanya hivyo ingawa aibu yake ilikuwa kama yangu pia kwa maana tu nilijiweka karibu naye asubuhi ya siku hiyo.
Moyoni mwangu nilijisikia vibaya sana kwa nini nilikaa karibu yake asubuhi ya siku hiyo.
Aliniangalia na kisha akatabasamu tu.
Dakika mbili si nyingi chapati zile zilikuwa zimeishia mdomoni mwake, alizikunja chapati zile mbili na kuzitafuna kwa mikupuo miwili tu zikawa zimeisha.

Kicheko cha watu kiliongezeka sasa hivi walishindwa kujizuia kucheka kisirisiri walicheka kwa sauti kubwa. Nilinyanyuka kwa hasira na kuondoka
“kwa kweli nimejiingiza kwenye mkenge, mama yangu akisikia kwamba nafanya mambo ya ajabu hapa chuoni hakika baba hatonielewa anaweza akachukua hatua kali.”
Niliondoka nikiwa na mvurugiko wa mawazo kutoka café mpaka kwenye madarasa yetu, nilichagua darasa ambalo halina watu na kisha nikakaa.
“oooh my god! Huyu ni mtu wa aina gani hivi hajui kama yuko katika jamii ya watu anapaswa kuwa na heshima na adabu mbele za watu. Kwanini anafanya mambo kama chizi alafu ananiingiza mimi kwenye mkenge huu, Shiit…”
Nilijawa na hasira sana kuwa karibu naye nilikumbuka maneno ya Melania:
“utajutia hapa ni chuoni.”
Ningejua ningemsikiliza Melania sijui kwanini niliruhusu kuwa karibu na huyu mkaka.
Watu walianza kuingia darasani kila mtu akiliongelea tukio lile nilibaki kimya nilikuwa nimekaa kwenye siti za mbele kama kawaida na mhadhara ulikuwa unakaribia kuanza.
Watu waliingia, Melania aliiingia darasani pia hakutaka hata kunisemesha alienda kukaa siti za nyuma kabisa.
Nilikuwa nimejiinamia kwenye kiti nikiwa na huzuni, mawazo pamoja na hasira.
Ghafla nilihisi mtu amekaa pembeni yangu.Sikujushughulisha kumuangalia niliendelea tu kuwaza na kuwazua.
“hello” sauti yake ilinishitua.
Niligeuka kwa mshituko huku nimetoa macho nikimtizama,
“ahsante kwa breakfast” aliongea na kisha aligeuka kutazama mbele kama ilivyokuwa kawaida yake kana kwamba anamsikiliza mhadhiri.
Nilishikwa na hasira sana nilinyanyuka kwa hasira nikavuta begi langu na kisha kujongea kuelekea nyuma kila mtu alibaki ananishangaa.
Nilifika mpaka viti vya nyuma ambapo Melania alikuwa amekaa aliniangalia kana kwamba anamuona mwendawazimu.
“sogea huko” nilimuambia. Alisogea na kisha nikakaa nikalaza kicha changu kwenye meza.
Mchanganyiko wa hasira, mawazo ulinifanya nisielewe mhadhara ule.
Mhadhara ulipoisha tu mhadhiri wetu alinichagua kuwa mwakilishi wa darasa ama CR. Nafikiri ilitokana na kwamba alikuwa akifahamiana na mama yangu hivyo baada ya kujua kwamba niko katika darasa lake aliamua kunichagua mimi kuwa CR.
Kiukweli akili yangu haikuwepo kabisa hapo darasani, mhadhiri alipoondoka tu nilibeba begi langu na kisha kuondoka sikutoa vitu vyangu kabisa tangu tumeingia hapo darasani.
Niliondoka moja kwa moja hadi Shuttle point kwa ajili ya kusubiri gari kuelekea Mabibo.
Gari lilipofika tu nilipanda wa kwanza na kisha nikakaa siti ya mbele kabisa sikutaka kukaa karibu na mtu yoyote.
Melania hakuwepo mbali ingawa hatukuweza kuwa karibu kivile, alikuwa akiniangalia kile nilichokuwa nikifanya huku akinishangaa.
Gari lilipofika Mabibo sikutaka hata kuagiza chakula nilishuka na kisha kuelekea chumbani kwetu mabweni ya Mabibo Block A, Room namba 147.
Nilivyofika tu niliingia na kulala sikuvua hata viatu nililala navyo.
Fety ambaye alikuwa ameshafika bwenini alibaki akinishangaa,
“una nini wewe we Sociolah…. Sociolah…..” sikutaka kugeuka.
Melania alifika, alifungua mlango na kisha akaenda kukaa kwenye kiti alivuta pumzi na kushusha.megombana? Kuna nini?” Fety aliuliza maswali mfululizo sikutaka kuendelea kumsikiliza niliamua kuutafuta usingizi. Nadhani Melania alimuelezea kila kitu kwa maana nilipokuja kuamka baada ya kuhisi njaa Fety hakuwa tena akiuliza maswali.
Niliamka nikiwa na uchovu sana, “nyie mimi nina njaa twendeni tukale.”
“Ndiyo unakumbuka saa hizi kwamba hujala.”
“aah twendeni bwana tukale” tulijiandaa na kisha kutoka nje.
Tulitoka hadi café ambapo walikuwa wanauza chakula, niliagiza chipsi kuku na kisha kukaa nikisubiria chakula changu. Melania na Fety waliagiza chakula na kisha kukaa pamoja.
Tulianza kula huku tukiongea mawili matatu ingawa bado nikihisi uchovu mwingi na kichwa kikiniuma,
“Mungu wangu balaa gani tena hili?!!” nilishituka.
Frank alikuwa akija kuelekea upande wetu, watu wote mule ndani ya café waligeuka na kutuangalia sisi. Melania alionesha kuchukia sana, kwa hakika alikuwa hampendi sana Frank.
“Anakuja kufanya nini huyu tena” niliwaza bila majibu.
Frank alisogea hadi upande wetu
“haloo” alinisalimia mimi tu.
“Unataka nini?” nilimuuliza kwa sauti iliyopoa
“samahani dada nilikuwa naomba….”
Melania alisimama na kuanza kumrushia matusi,
“wewe umechanganyikiwa mbona unapenda kushobokea watu usiowajua eenh yani kuongeleshwa tu kidogo basi ndiyo unafikiri kama umeunga ukoo kwanini unapenda kumsumbuasumbua rafiki yangu, samahani wewe hauko kwenye level zetu naomba uachane na sisi tena umkome Sociolah.”
“aah nilikuwa sijui anaitwa nani kumbe anaitwa Sociolah.” Frank aliongea, nilizidi mkushangaa.
“Frank kuwa na akili sikia nikuambie sitaki ukaribu na wewe naomba kuanzia leo usinizoee.” Nilipatwa na ujasiri wa kuongea.
“usijali.” Alisema.
Watu wote walikuwa wakituangalia sisi mule ndani
“shiit… nilishindwa hata kula nilinyanyuka na kuondoka kuelekea chumbani kwangu.
Nafsi ilinisuta sana kumtukana ingawa nahisi alistahili sana matusi yale,
“Yani yupo kama hayupo sijui kama ana akili sawasawa huyu.”
Nilifika chumbani kwangu na kujilaza, muda haukupita Fety na Melania waliingia nao walikuwa wamepaniki sana.
Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza Fety anamuona lakini ilionesha kiasi gani hampendi. Walikuwa wakiongea maneno ya kulaani kitendo cha kutuijia pale usiku ule,
“tumemuacha pale mezani maana anatushobokea sijui hata ameona nini, anafikiri sisi ni level sawa na yeye, fyuu…” mwishoni alifyonza.
Niligeukia upande wa pili usiku huo ulipita.

INAENDELEA……

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search