Sunday, 17 September 2017

NATAKA KUZAA-EPISODE YA TANO


MTUNZI: JENNIFER ALPHONCE
SIMU: 0683777152
SEHEMU YA TANO
Nilikutana na Patrick kiasi kama miezi sita iliyopita, wakati huo ndiyo nilikuwa tu nimemaliza kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Ifakara Girls iliyopo Ifakara mjini.
Nilikutana na Patrick katika moja ya sherehe ambazo baba alikuwa amealikwa, baba alipenda kuhudhuria na mimi.
Patrick alikuwa ni mhasibu wa TANESCO pale Ubungo mataa na alikuwa akiishi Shekilango.
Alikuwa amepanga nyumba moja kubwa ambayo ilikuwa inajitegemea kwa kila kitu, nilimpenda sana Patrick.
Tatizo moja tu alikuwa nalo Patrick alikuwa ni mtu asiyeishiwa na ubize, kila wakati yuko bize, asipokuwa bize na kazi basi yupo bize na marafiki, asipokuwa bize na marafiki basi na kitu kingine chochote tu ilimradi yuko bize muda wote.
Siku ya jumamosi niliamua kwenda kwake.
Patrick alikuwa hafahamiki kwetu hivyo nilidanganya nyumbani kuwa ninaenda kwa rafiki yangu, mama aliniruhusu.
Niliondoka hadi kwa Patrick sikutaka kumuambia kwamba naenda.
Siku hiyo ya jumamosi Patrick hakuwepo nyumbani, kwakuwa ninafahamu sehemu ambayo Patrick huwa anaweka funguo yake nilifungua na kuingia ndani na kisha nikampigia simu.
“Patrick niko kwako nakusubiri.”
“Sociolah mbona umekuja bila kuniambia leo mimi siko nyumbani siku nzima.”
“Patrick you are not serious”
“Sociolah niko bize sana naomba tu uende nyumbani.”
“Patrick nina shida ndiyo maana nimekuja.”
“Sema unataka shilingi ngapi.” Kiukweli ilinikera sana.
Mbali na kuwa nilikuwa nikihitaji hela lakini pia nikihitaji faraja kutoka kwake.
“Sawa.” Nilikata simu.
Sikuwa na pa kwenda niliamua tu kumalizia tu siku yangu hapo, niliingia chumbani kwake na kulala.
Jioni ilifika Patrick hakuwa kweli amerejea niliondoka na kuelekea nyumbani.
Nilipofika sikutaka hata kula niliingia chumbani kwangu na kulala, mama alikuja kuniamsha,
“Sociolah amka uende kula.”
“Mama nimechoka sana.”
“Nimesema amka uende kula, siku hizi umekuwa mvivu sana kula sijui una matatizo gani Sociolah, utakonda chuo hakihitaji mchezomchezo kula mwanangu.”
Sikutaka kubishana naye nilielekea sebuleni nilikula kidogo na kisha kurudi chumbani kwangu.
Nilipofika tu nilikuta simu yangu inaita alikuwa ni Patrick, nilipotaka tu kupokea ilikata, nilikuta simu zisizopokelewa saba na meseji tano, zote zilikuwa za Patrick, alipiga tena nilipokea.
“Hello.”
“Am sorry Sociolah nilikuwa niko bize na saa hizi nimerejea nyumbani ulikuwa na tatizo gani.”
“Patrick….”
“Nakusikiliza.” Aliongea.
Patrick ni mtu ambaye ananisikiliza sana na kunijali na alikuwa akinipenda sana na zaidi ya yote alikuwa ana malengo mazuri tu na mimi ila ubize wake ulinikera sana.
“Niambie Sociolah shida ni nini mama?”
“Patrick kuna mambo yananichanganya sana nilikuwa nahitaji faraja kutoka kwako ingawa uko bize sana. Hata hivyo nilikuwa nahitaji pesa maana nimeibiwa hela zangu na siwezi kumuambia mama.”
“Unahitaji kama shilingi ngapi?”
“Yoyote tu mimi siwezi kukupangia.”
“Umeibiwa shilingi ngapi?”
“Nimeibiwa kama laki tano hivi.”
“Pole, nitakutumia.”
“Nitashukuru sana.”
“Aya, usiku mwema.”
“Patrick hautaki hata kuongea na mimi kidogo.”
“Kuna kazi nafanya hapa mama, nitakupigia nikimaliza.”
Nilijua kwamba hatonipigia kwa maana hamalizagi kazi zake.
“Sawa usiku mwema.”
Alikata simu yake.
Kwa kiasi Fulani nilijihisi afueni.
Haikupita dakika kadhaa Patrick alinitumia laki tano, nilifurahi sana.
Siku ya jumapili nilirejea bwenini kwetu Mabibo na siku ya jumatatu tuliingia kwenye vipindi kama kawaida.
Melania bado hakuwa amepata simu yake hivyo alikuwa mtu mwenye Hasira muda wote na manung’uniko.
“Usijali utapata.”
Ilipofika saa sita kasoro dakika tano tuliingia kwenye semina.
Kiongozi wa semina ile alitupa maelekezo machache kuhusu semina yetu na kisha akatugawa katika makundi kwa ajili ya kazi ya kuwasilisha.
Daktari Kisayeye alianza kwa kuongea.
“Makundi yapo matano kundi la kwanza mtawasilisha jumatatu ijayo, kundi hili lina watu wanne, Sociolah Kivamba”
“Mmmh..!” Kwanza nilishituka lakini pia nilifurahi kuwa wa kwanza kuwasilisha kazi bila kuwa na uzoefu wowote ilikuwa siyo jambo dogo.
“Melania Petro”
“Woow...!” Nilifurahi sana…. Nilifurahi kuwa na Melania katika kundi moja.
“Innocent Chande.” Hata sikuwa nikimfahamu ni kwa mara ya kwanza nimekutana naye.
Watu wote tuliotajwa ilibidi tusimame ili tufahamiane alisimama huyo Innocent, alikuwa ni mkaka mzuri sana nilifurahi kuwa naye Kundi moja alikuwa mtanashati mno.
“Na wa mwisho atakuwa ni Franklin Kazimana.” Nilihisi kuzimia.
“Frank tena?!”
Melania ambaye uso wake ulipambwa na Tabasamu ulibadilika ghafla, alichukia kupita maelezo nilishindwa hata kumtazama usoni.
Daktari Kisayeye aliendelea kutaja watu katika makundi yao tofauti tofauti.
Kiukweli nilianza kuichukia ile semina yetu.
Kiongozi wetu alipoondoka tu Melania alikuwa wa kwanza kutoka darasani.
Innocent aliniita, “Sociolah.”
Niligeuka na kumfuata.
“Unajua tuna kama siku chache tu hivi kabla hatujawasilisha kazi yetu inabidi tukutane tuanze kupanga mikakati, mbona mwenzio amekimbia.”
“Aanh.. atakuwa hajisikii vizuri, tunakutana lini?”
“Kwani nyie mnakaa wapi?” Aliuliza.
“Tunakaa mabibo.”
“Basi tukatane leo saa moja Mabibo.”
“Sawa.” Niliongea na kuondoka, nyuma yake nilimuacha Frank akipiga hatua kumkaribia Innocent, niliwaacha waendelee na maongezi yao na mimi niliondoka.
Baada ya kumaliza vipindi vyote tulirejea Mabibo.
Saa moja kamili ya siku hiyo ilitukuta katika Vimbweta vya Block A.
Melania alikuwa bado amenuna.
“Huyu mwalimu shetani kweli akachagua watu akaona bora atuweke na huyu chizi.”
“Melania acha bwana aaah.”
“Mimi sijui kama nitakuwa Comfortable kwa kweli na huyu taahira huyu.”
Frank na Innocent walikuwa wakipiga hatua wakijongea upande wetu.
INAENDELEA……..

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search