Tuesday, 12 September 2017

UTAFITI:-Tanzania Yaporomoka kwa Ukarimu Duniani

Tanzania imeporomoka nafasi sita katika utafiti wa ukarimu duniani ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kufanya vizuri, jambo linaloonyesha Watanzania wameanza kuwa na mkono wa birika katika kuchangia wenye uhitaji.

Ripoti mpya ya ukarimu ya mwaka 2017 iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita inabainisha sasa Tanzania inashika nafasi ya 63 duniani kutoka 57 mwaka jana, nyuma ya majirani Kenya na Uganda katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika ripoti hiyo ya kila mwaka inayoandaliwa na asasi ya kiraia ya kimataifa kutoka Uingereza ya Charities Aid Foundation (CAF), inaonyesha Tanzania imeanguka katika vipengele viwili kati ya vitatu ambavyo hutumika kupima ukarimu wa watu wa nchi husika.

Mwaka jana, Tanzania ilifanya vyema katika utafiti huo katika vipengele vyote vya kumsaidia usiyemjua, kuchangia fedha na kujitolea muda kwa ajili ya kuwasaidia wale wenye uhitaji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya nane, ni rahisi kwa Mtanzania kukupatia fedha lakini si kupoteza muda wa kukusaidia au kukuhudumia iwapo hakufahamu.

Katika ripoti ya mwaka huu, Tanzania inashika nafasi ya 110 katika kipengele cha kujitolea muda kwa wenye uhitaji na nafasi ya 60 kati ya 138 zilizofanyiwa utafiti duniani katika kipengele cha kusaidia wageni wasiofahamika.

Ni kipengele kimoja tu cha kujitolea fedha ambacho Tanzania imepaa kwa nafasi 13 kutoka nafasi ya 49 mwaka jana hadi nafasi ya 36 mwaka huu ikiwa juu ya Uganda, Rwanda na Sudan Kusini.

Hii ni kinyume cha Kenya ambao wanashikilia nafasi ya pili duniani katika kipengele cha kujitolea muda kwa wenye uhitaji na nafasi ya nne kwa kumsaidia mgeni wasiyemjua. Kenya ni nchi ya tatu duniani kwa ukarimu.

Hata hivyo, ripoti ya utafiti huo uliofanywa mwaka jana inabainisha kuwa, licha ya ukarimu kushuka kwa jumla duniani mwaka jana, bado Afrika imefanya vyema baada ya wastani wa ukarimu kupanda kwa kila kipengele.

“Afrika mwaka huu imeenda kinyume cha mwenendo wa dunia na ndiyo Bara pekee lililoshuhudia kupanda kwa tabia ya kujitolea katika vipengele vyote vitatu itakapolinganishwa na wastani wa ukarimu kwa miaka mitano,” inaeleza ripoti hiyo.

Myanmar ndiyo nchi yenye ukarimu zaidi duniani kwa mwaka wa nne mfululizo ikifuatiwa na Indonesia na Kenya.

Utafiti huo ulifinyika katika nchi 138. Baadhi ya watu walioteuliwa kuwa sampuli waliulizwa ni mara ngapi huwasaidia watu wasiowajua, kuchangia fedha na kujitolea muda wao kwa wasiojiweza ili kupima kiwango cha ukarimu wao.

“Ili kuongeza tabia ya kujitolea miongoni mwa watu duniani, Serikali zote zinatakiwa kuhakikisha asasi za kiraia zinadhibitiwa kwa haki na kwa uwazi, zirahisishe mazingira ya watu kujitolea na kutoa motisha pale inapobidi,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti inaeleza, “Serikali pia, zihamasishe uwepo wa asasi za kiraia kama sauti huru za maisha ya watu na kuheshimu haki za taasisi zinazojiendesha pasipo kupata faida kuzungumzia masuala ya msingi ya kitaifa.”

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search