Friday, 13 October 2017

Daraja la Kilombero kuzinduliwa

UZINDUZI wa Daraja la Mto Kilombero mkoani Morogoro, utafanyika wakati wowote kuanzia sasa baada ya ujenzi kukamilika kwa asilimia 100.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa aliliambia HabariLeo jana kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa Serikali ambao ama ni Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu, anatarajiwa kwenda kufanya uzinduzi huo.

Kwandikwa alisema daraja hilo lenye urefu wa mita 384 na viwango vya kisasa, litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya aina zote na lilivyosanifiwa linafanana na Daraja la Kigamboni.

“Natambua changamoto ya kivuko waliyokuwa nayo wananchi wa Ulanga, Malinyi na Kilimbero, naamini kukamilika kwa daraja hili itakuwa msaada mkubwa kwao. Serikali tumejipanga kuhakikisha wananchi wa wilaya hizo wanaunganishwa vyema na wananchi wa wilaya nyingine za mikoa ya kusini,” alieleza Kwandikwa.

Alisema kuwa baada ya kuaminiwa na Rais katika nafasi hiyo ya Unaibu Waziri, atahakikisha anamsaidia vyema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kwa kufanya ukaguzi kwenye miradi mbalimbali. Alisema atakwenda kufanya ukaguzi kwenye daraja Oktoba 23.

Moja ya changamoto inayoikabili Wilaya ya Ulanga ni kutounganishwa na wilaya nyingine kwa upande mikoa ya kusini, hali iliyofanya wilaya hiyo kuwa kama kisiwa, lakini pia kuna changamoto ya barabara kwa wilaya zote za Ulanga, Malinyi na Kilombero.

Naibu Waziri alisema kuwa changamoto hizo zitafanyiwa kazi haraka ili kuwasaidia wananchi. Wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi maarufu kwa kilimo cha mpunga na ufugaji, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia usafirishaji wa mazao ya mpunga, ufuta, mahindi na mazao yatokayo na mifugo.

Ikumbukwe kwamba mwaka jana mwezi Januari kivuko cha Mto Kilombero ‘MV Kilombero ll’ kilipinduka baada ya kusukumwa na upepo mkali ambapo watu 30 kati 31 waliokuwemo waliokolewa. Tukio hilo la kuzama kwa kivuko Mto Kilombero lilikuwa la pili baada ya mwaka 2003 pia kuzama na kuua watu kadhaa

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search