Wednesday, 18 October 2017

Diwani wa Chadema Aliyerekodi Madiwani Wakishawishiwa Kujiuzulu Arusha Ajitokeza

Diwani aliyehusika kuwarekodi viongozi wa Halmashauri ya Meru wanaodaiwa kuwa walikuwa wakiwashawishi kwa ahadi ya fedha na mambo mengine Madiwani wa CHADEMA ili wajiuzulu, amejitokeza na kusema kuwa yeye alifanya hivyo kutokana na kuchukia rushwa.

Diwani wa Kata ya Mbuguni, Ahimidiwe Rico aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka katika ofisi za Taaisisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Arusha ambao alihojiwa kwa takribani saa tatu kuhusu tuhuma hizo za rushwa.

Rico aliwaambia waandishi wa habari kuwa alifanya hivyo kutokana na kuchukia rushwa na ni kwa manufaa ya maslahi mapana ya taifa na sio kwamba ni masuala ya kisiasa.

Akizungumzia kuhojiwa na TAKUKURU, Rico alisema kuwa alifika katika ofisi hizo baada ya kupokea wito uliomtaka kufanya hivyo, na alipofika alikutana na maafisa wa TAKUKURU kutoka Makao Makuu Dar es Salaam, ambapo walimhoji na yeye alitoa ushirikiano wote wakati wa mahojiano hayo.

Alisema kuwa alipoulizwa kuhusu vifaa vilivyotumika kurekodi, alisema kuwa ni mali ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari ambavyo alivitoa nchini Uingereza alipokuwa akisoma, na kwamba ushahidi huo walishirikiana kuukusanya.

Rico hakuweka wazi na masuala gani aliyoulizwa au aliyowaambia maafisa hao akisema kuwa, jambo hilo lipo chini ya uchunguzi hivyo ni vyema wakaachiwa TAKUKURU wenyewe wafanye kazi yao.

Mbali na Rico, maafisa hao waliwahoji kwa zaidi ya saa sita, madiwani waliojiuzulu Chadema wanaotuhumiwa na Mbunge Nassari kuwa walipewa rushwa na si kweli kwamba walijiuzulu kwa hiar yao kama ambavyo walidai kwa nyakati tofauti.

Wengine waliohojiwa ni  Catherine Mtui, aliyekuwa Diwani wa Viti Maalumu, Japhet Jackson, aliyekuwa Diwani wa Ambuleni na Bryson Isangya, aliyekuwa Diwani wa Maroroni.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search