Monday, 9 October 2017

IGP SIRRO : NI AIBU KWA MWANASIASA KUTAKA KUMFUNDISHA KAZI ASKARI....SITAKI MALUMBANO

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amesema hataki malumbano na hana majibu kuhusu shinikizo linalotolewa na Chadema na familia ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kuruhusu vyombo vya nje kufanya uchunguzi wa tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi kwa mbunge huyo.


IGP Sirro amesema hayo jana Jumapili jijini hapa, akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alipojibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua kauli yake baada ya familia ya Lissu na viongozi wa Chadema kutamka kuwa hawana imani na Jeshi la Polisi kuhusu uchunguzi huo.


Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) alijeruhiwa kwa risasi Septemba 7 mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.


IGP Sirro alisema yeye na jeshi lake wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria kwa kuwatumikia Watanzania wote kuhakikisha wanakuwa salama pamoja na mali zao na si mtu mmoja.


Amewataka wanasiasa kuliacha jeshi hilo lifanye kazi yake.


"Ahsante kwa swali lakini kwa hili sina majibu kwa sababu sitaki malumbano. Sisi tupo kwa ajili ya Watanzania wote ndiyo maana nchi ipo shwari. Mimi ndiye mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na ninawajibika kuhakikisha raia na mali zao zinakuwa salama na kwa kweli ni salama. Kwa hiyo swali lako sina jibu,” alisema IGP Sirro.


Alisema ni aibu kwa mwanasiasa kutaka kumfundisha kazi askari anayetambua wajibu wake au askari kwenda kumfundisha siasa mwanasiasa, hivyo ametaka kuwe na mipaka ya utendaji kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na si vinginevyo.


Viongozi wa Chadema na familia ya Lissu imetoa msimamo ikitaka vyombo vya dola kuruhusu uchunguzi huru kwa kuhusisha vyombo kutoka nje ya nchi.


IGP Sirro yuko ziarani mkoani Mbeya ambako amekutana na askari na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search