Saturday, 7 October 2017

LIPUMBA NA WENZAKE WAGONGA MWAMBA MAHAKAMANI WASHINDWA KESI

Mahakama Kuu imekataa pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria wa Serikali dhidi ya maombi ya kuizuia kufanya kazi Bodi ya Wadhamini wa CUF, kambi ya mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Uamuzi huo ulitolewa jana Alhamisi na Jaji Wilfred Dyansobera aliyetupilia mbali hoja za pingamizi zilizotolewa na wajibu maombi wakipinga maombi yaliyofunguliwa na Mbunge wa Malindi(CUF), Zanzibar, Ally Saleh.
Kutokana na uamuzi huo, Mahakama itaanza kusikiliza maombi ya mbunge huyo anayeomba zuio dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CUF ambayo wajumbe wake waliteuliwa na Profesa Lipumba.
Akizungumza na waandishi wa habari mmoja wa mawakili wa CUF, Juma Nassoro kwa upande wa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif alisema Jaji Dyansobera ameamuru usikilizwaji ufanyike kwa njia ya maandishi.
Nassoro amesema muombaji ametakiwa kuwasilisha hoja zake Oktoba 19 na wajibu maombi wametakiwa wawe wamezijibu ifikapo Oktoba 27.
Amesema Jaji Dyansobera ameelekeza iwapo muombaji atakuwa na hoja za nyongeza awe ameziwasilisha ifikapo Novemba 4 na shauri litatajwa Novemba 6.
Mbunge Saleh alifungua maombi hayo kutokana na kesi ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo akipinga uhalali wa wajumbe wa bodi walioteuliwa na Profesa Lipumba.
Anaiomba Mahakama itoe amri ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakala wao na watu wote wanaofanya kazi kwa maagizo yao kutokujihusisha kwa namna yoyote na masuala ya chama hicho mpaka uamuzi wa shauri lake la msingi utakapotolewa.
Wajibu maombi ni Ofisa Mtendaji wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita), aliyewakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wengine ni Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, mwenyekiti wa bodi hiyo, Peter Malebo na wajumbe wa bodi hiyo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search