Wednesday, 18 October 2017

Miss Tanzania Akabidhiwa Bendera Kwenda Kuwakilisha Mashindano ya Miss World

Miss Tanzania Akabidhiwa Bendera Kwenda Kuwakilisha Mashindano ya Miss World
Miss Tanzania aliyeteuliwa na kamati ya shindano hilo, Julitha Kabete amekabidhiwa bendera leo Jumatano kwenda kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World 2017.

Julitha ni mshindi wa nafasi ya tano ya Miss Tanzania 2016,

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya bendera ya Taifa kati ya mwakilishi huyo na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mkurugenzi wa Lino Agency Tanzania, Hasheem Lundenga amesema kutokana na kutofanyika kwa mashindano hayo mwaka huu, wamemteua Julitha kuwa mwakilishi wa Tanzania kwa mwaka huu.

"Rekodi yetu ya Miss Tanzania ni nzuri hivyo Miss World walivyohitaji tutume mwakilishi tuliwaambia kwa mwaka huu hatukufanya mashindano, walitusihi tutume mwakilishi kwa kuzingatia vigezo, hivyo tuliwaambia tunaye Julitha na wakakubali hivyo ataiwakilisha nchi kwa mwaka huu," amesema Lundenga.

Akizungumza na vyombo vya habari, Julitha amewashukuru Kamati ya Miss Tanzania kwa uteuzi na kuahidi kwamba hatawaangusha kwani amejiandaa vema na mashindano hayo ya urembo ya dunia.

"Nilikuwa mrembo na mshiriki wa Miss Dar City Center, Miss Ilala na hatimaye fainali za Miss Tanzania 2016 na nimeweza kujifunza mambo mengi katika tasnia hii ya urembo," amesema Julitha.

Mrembo huyo ambaye alishika nafasi ya tano ya Miss Tanzania 2016, Pia amewahi kushiriki mashindano ya urembo ya Afrika, Miss Africa yaliyofanyika nchini Nigeria mwaka 2016. 

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search