Tuesday, 10 October 2017

MKUU WA SHULE YA SEKONDARI AJIUA

Mkuu wa Shule ya Sekondari Migukulama iliyopo Halmasahauri ya Buchosa wilayani Sengerema, Benerdicto Lweikiza (45) amejinyonga hadi kufa akiwa chumbani kwake.


Taarifa za kujinyonga kwa mwalimu huyo zilianza kusambaa wilayani Sengerema na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda.


“Ni kweli mwalimu huyo amejinyonga alikuwa mkuu wa Shule ya Sekondari Migukulama na amefikia uamuzi huo majira ya saa tisa mchana wa leo (jana) nyumbani kwake Mtaa wa Kilabela mjini Sengerema,” alisema Luanda.


Mmoja wa wanafamilia wa mwalimu huyo, Martin Kalemera alisema kuwa wao kama familia wanashangazwa na suala hilo na hawaamini kilichotokea ikiwa ni miaka mitano imepita tangu mke wake afariki dunia.


Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alithibitisha kupata taarifa ya kifo cha mwalimu huyo na kusema kuwa hajafahamu chanzo cha kufikia hatua ya kujinyonga na kamba chumbani kwake.


Alisema vyombo vya dola vinafuatilia kwa kina ili kubaini sababu.


Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya gari aina ya Toyota Hiace kutumbukia ndani ya Ziwa Victoria na kuua zaidi ya watu 12 katika eneo la Kivuko cha Kigogo wilayani Misungwi.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search