Wednesday, 18 October 2017

Sheikh Ponda afafanua kauli yake kwa wanahabari. Ni ile iliyodaiwa kuwa ya kichochezi

Image result for sheikh ponda
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda amesema alichozungumza hakikuwa uchochezi bali alitoa tahadhari kwa matukio yanayojitokeza na jinsi ya kuyakabili kwa mustakabali wa amani ya nchi.

Sheikh Ponda ametoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza tangu alipotiwa nguvuni na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akituhumiwa kutoa lugha ya uchochezi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano wiki iliyopita.

Katika mkutano huo, alizungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya utekaji, kuokotwa miili ya watu na mazungumzo aliyoyafanya kati yake na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya akiuguza majeraha baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu baada ya kutoka kuripoti Polisi, Sheikh Ponda amesema, “Nilizungumza kwa nia nzuri kwa masilahi ya Taifa na umma. Nilikuwa nakumbushia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwamba vina wajibu wa kusimamia amani na usalama.”

Amesema, “Kile nilichozungumza nimewaeleza nilikuwa sahihi na sikuwa na nia mbaya hata kidogo… leo saa tatu nimeripoti na nimeelezwa niondoke na watakaponihitaji muda wowote watanipigia simu.”

Kuhusu upekuzi uliofanyika nyumbani kwake Ubungo- Kibangu, Sheikh Ponda amesema, “Tulikwenda kukagua siku hiyo ya Ijumaa kama saa mbili usiku, walidai wanatafuta kama kuna nyaraka zozote za uchochezi lakini hawakuzikuta. Tuliporudi polisi dhamana ilishindikana kwa kuwa wakubwa hawakuwepo.”

Ponda alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi Ijumaa Oktoba 13 asubuhi kwa wito wa Jeshi la Polisi lililompa saa 72.

Baada ya kujisalimisha alishikiliwa kwa mahojiano na baadaye askari walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake na aliachiwa Jumamosi Oktoba 14 akitakiwa kuripoti leo.


CHANZO: Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search