Friday, 13 October 2017

Sheria ya Vyama vya Siasa Kufuta Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa Hadi Wakati wa Uchaguzi Pekee

Sheria ya Vyaamaa vya Siasa Kufuta Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa Hadi Wakati wa Uchaguzi Pekee
RASIMU ya Sheria ya Vyama vya Siasa inayotarajiwa kufanyiwa marekebisho kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, inapendekeza kufutwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa hadi wakati wa uchaguzi pekee.

Rasimu hiyo, ambayo imetumwa kwa vyama vya siasa kwa ajili ya kutoa maoni yao, pia inapendekeza ruzuku ilipwe mara moja na kwa vyama vyote kulingana na idadi ya kura za urais katika Uchaguzi Mkuu.

Iwapo mabadiliko hayo yatapelekwa bungeni, uwezekano wa kupitishwa kuwa sheria ni mkubwa kutokana na idadi kubwa ya wabunge kutoka chama tawala (CCM) kinachoongoza Serikali ambayo itawasilisha muswada wa mabadiliko hayo.

Rasimu hiyo imekuja wakati vyama vya upinzani vikipigia kelele kutoheshimiwa kwa Katiba na sheria na kuminywa kwa demokrasia iliyofanya vishindwe kupiga siasa kwa uhuru, hasa baada ya Serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano.
Serikali imeruhusu mikutano ya ndani ambayo pia imesababisha viongozi kadhaa kukamatwa au kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupanga mikakati ya uchochezi.

Na tayari vyama vya upinzani vimeshaingiwa na hofu dhidi ya mapendekezo hayo, vikisema yanalenga kufuta sheria ya mwaka 1992, kwa mujibu wa viongozi waliozungumza na Mwananchi jana na juzi.

Katika Rasimu ya Muswada wa Mabadiliko ya Sheria hiyo, Kifungu cha 45(2) kinaeleza kuwa mikutano ya vyama haitaruhusiwa katika kipindi ambacho hakuna uchaguzi, isipokuwa itakayoitishwa na wabunge, wawakilishi na madiwani katika maeneo yao.
Kuhusu ruzuku, rasimu ya muswada huo katika Kifungu cha 59 (1) inaeleza itatolewa mara moja katika mwaka wa fedha na waziri atazingatia hali ya kiuchumi na kifedha katika wakati husika.
“Sheria inayotungwa kwa kuangalia mtu au kundi la watu ni sheria mbaya,” alisema mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipoulizwa maoni yake kuhusu mapendekezo hayo.
“Kinachofanyika sasa kinaturudisha miaka 25 nyuma. Uhuru alioupigania Mwalimu (Julius)Nyerere upo wapi? Uhuru wa kukusanyika, uhuru wa mawazo?”
Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) alisema nchi inaendeshwa kwa matukio na kushauri kuwa maendeleo ya nchi ni lazima yawe shirikishi.
“Ajenda ya Malengo ya Milenia ya amani, haki na uimara wa taasisi unatoweka nchini,” alisema Mbatia, ambaye ni mbunge wa Vunjo.
“Zamani, mataifa ya nje yalikuwa yanakuja kujifunza siasa hapa kwetu, lakini kwa hali inavyoendelea sasa, watakuja kujifunza kitu gani? Tunapaswa kurejea katika mchakato wa Katiba ya Jaji Warioba, Katiba imara itatuondoa hapa tulipo na kwenda mbele zaidi.”
Serikali ilitangaza kupiga marufuku mikutano ya hadhara mwaka 2016, ikisema inataka watu wajikite kufanya kazi za maendeleo na kwamba yataruhusiwa mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Tamko hilo kwanza lilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, lakini alipoulizwa bungeni alisema ilihusu jimbo lake na baadaye likatolewa na Jeshi la Polisi wakati Chadema ilipotangaza mikutano ya hadhara ya kuishtaki Serikali, kabla ya Rais John Magufuli kuweka bayana wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma za polisi Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kwa wakati wote, vyama vya upinzani vimekuwa vikipinga marufuku hiyo kwa maelezo kuwa inapingana na Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotoa uhuru kwa watu kukusanyika na kuitishana kwa lengo la kujadili, kufanya mkutano au kupeleka ujumbe kwa jamii au Serikali kuhusu jambo lolote ilimradi wanafanya hivyo kwa amani.

“(Muswada huu) Umehalalisha makatazo ambayo hayakuwa kwa mujibu wa sheria na hasa tamko la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa sasa yanawekwa kwenye sheria,” alisema mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema.
“Kama chama tutakaa kupitia kifungu kwa kifungu na kutoa msimamo kuhusu rasimu ya muswada huu.

“Muswada huu umeweka vifungu vingi ambavyo siasa sasa imefanywa kuwa kosa la jinai.”
Pamoja na vyama vya siasa, hasa vya upinzani kupinga mapendekezo hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameyatetea kuwa yametoka kwa wadau.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Jaji Mutungi alisema mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu hiyo yametoka kwa wadau, akisema ndio waliowezesha kupatikana kwa rasimu hiyo.
“Yeyote mwenye hoja afike ofisini kwangu,” alisema Jaji Mutungi.

Katika Kifungu cha 47 cha mapendekezo hayo, vyama vya siasa vinazuiwa kuajiri, kusambaza, kuunda vikundi vya ulinzi au kuwa na muundo sawa na wa Jeshi la Polisi au chombo chochote cha ulinzi na usalama cha Serikali.
Pia, vyama vinazuiwa kuratibu au kutoa mafunzo ya kijeshi na kutumia silaha.
Mapendekezo hayo pia yanalenga kuondoa utaratibu uliopo sasa wa vyama vya siasa kuwa na wanachama wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutokana na kifungu cha 32 kuzuia vyama kufanya shughuli za kisiasa kwenye maeneo ya kazi, shule au vyuo na majengo ya Serikali.
Mapendekezo hayo yanapendekeza adhabu ya Sh3 milioni au kifungo cha miezi sita jela au adhabu zote kwa pamoja kwa yeyote atakayekiuka kifungu hicho.

Mapendekezo hayo pia yanabadilisha utaratibu wa kuwasilisha ilani za uchaguzi. Kifungu cha 31(1)(c) kinapendekeza vyama kupeleka ilani hizo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa badala ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mrema, ambaye aliratibu kampeni za urais cha Chadema mwaka 2015, alisema mapendekezo hayo yanampa mamlaka makubwa Msajili kama ya kimahakama kwa kuwa anaweza kuagiza kupelekewa taarifa yoyote ya chama cha siasa, jambo alilosema ni la hatari.

Alikuwa akirejea Kifungu cha 36 cha rasimu hiyo kinachopendekeza kuwa kama chama cha siasa kitaitwa au kualikwa katika mafunzo ndani au nje ya nchi, ni lazima kitoe taarifa kwa Msajili siku saba kabla na kikikiuka kitakumbana na faini ya kati ya Sh1 milioni hadi Sh10 milioni au kifungo cha miezi sita gerezani au vyote kwa pamoja.
Sheria wanazotaka wao
Wakizungumza kuhusu rasimu hiyo, viongozi wa kisiasa walilaumu kuwa inalenga kuwabana.
“Tangu nchi hii ilipopata uhuru Desemba 9, 1961, sheria zinazotungwa ni zile wanazotaka wao na ndiyo maana zimekuwa na matatizo,” alisema mwenyekiti wa chama cha United Peoples’ Democratic (UPDP), Fahmi Dovutwa.

“Wao wamepanga na wanataka wanachotaka wao. Mimi nimepeleka mapendekezo, lakini sidhani kama yatafanyiwa kazi. Wanachokifanya si sawa. Huwezi kuweka sheria ngumu, huwezi kutubana tusifanye siasa.

“Sawa tutawasikiliza kwa kuwa wametaka wao. CCM wanaogopa kivuli chao na itakuja kuwagharimu siku moja. CCM isifikirie itapata kila siku na upinzani utakosa kila siku. Ipo siku CCM watang’oka na itawagharimu.”

Maoni kama hayo alikuwa nayo mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Costantine Akitanda ambaye alisema mapendekezo hayo yana lengo la kumaliza siasa na watu kama yeye wanaweza kujiondoa kutoka katika siasa.

“Sitaki kuamini kama kuna wabunge wanaojitambua hata wa CCM ambao watakubali kupitisha mapendekezo hayo,” alisema Akitanda. “Kwa nini tunashughulika na kuweka sheria kandamizi zinazokinzana na Katiba? Tunapaswa kutengeneza sheria zinazotekelezeka. Mimi nitakuwa miongoni mwa watakaoachana na siasa kwa sheria hizi na itafika wakati mzazi akimsikia mwanae anataka kuwa mwanasiasa atamzuia kwa sheria za aina hii.

“Ngoja tusubiri tukiitwa kuijadili na hata ikienda tutaitwa Kamati ya Bunge na tutaipinga.”

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search