Friday, 13 October 2017

UJUMBE WA WATU 300 UNAOMWAKILISHA MFALME WA OMANI WAWASILI ZANZIBAR

Ujumbe wa watu zaidi ya 300 unaomwakilisha Mfalme wa Oman, Shekh Sultan Qabous Bin Said umewasili visiwani Zanzibar leo Alhamisi asubuhi kwa kutumia meli yenye jina la Fulk Al Salamah ambayo hutumiwa na mfalme huyo.


Ujumbe huo wa Serikali ya Oman umewasili katika Bandari Kuu ya Malindi mjini hapa majira ya saa tatu na nusu za asubuhi ikitokea nchini Oman.


Katika mapokezi ya ujumbe huo viongozi wa Serikali ya Zanzibar walihudhuria akiwamo Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Rashid Ali Juma, Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira, Salama Aboud Talib na Wazir wa Biashara na Masoko, Amina Salum Ali.


Kwa upande wa ujumbe huo wa mfalme uliongozwa na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Mohamed Al-ramh ambapo lengo kuu la kufika Zanzibar ni kusambaza amani na upendo ikiwa ni hatua ya kufikisha ulimwenguni kote.


Akizungumza katika mapokezi hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed amesema ni faraja kubwa kwa Zanzibar kupata ugeni huo wa heshima.


Amesema ugeni huo ni ishara njema ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ambazo zinaonekana kuwa na udugu wa kihistoria kwa miaka mingi.


‘’Ishara hii ni njema na tunaifurahia kwa moyo wote na kesho tutakuwa na mazungumzo rasmi na ugeni huo ambapo tunataraji mambo mbalimbali tutayajadili na baadaye kutoa taarifa rasmi ya mazungumzo yetu,” amesema Aboud.


Hata hivyo amesema ujumbe huo pia utapa nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria, ofisi za Serikali lengo ni kubadilishana mawazo juu ya ukuaji wa uchumi.


Waziri Aboud amewataka wananchi wa Zanzibar kuwapokea wageni hao katika maeneo tofauti ili kuonyesha ukarimu wao.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search