Tuesday, 10 October 2017

UN Yapiga Marufuku Meli Nne Juu ya Korea Kaskazini

UN Yapiga Marufuku Meli Nne Juu ya Korea Kaskazini
Umoja wa Mataifa umepiga marufuku meli nne dhidi ya kufika kwenye bandari za kimataifa baada ya kubainika kwamba zilikiuka vikwazo vilivyowekewa Korea Kaskazini na umoja huo.
Hugh Griffiths, mkuu wa jopo la UN kuhusu vikwazo vya Korea Kaskazini, amesema meli hizo zimekuwa zikisafirisha "bidhaa zilizoharamishwa".
Amesema hatua ya kupiga marufuku meli hizo si ya kawaida.
Umoja wa Mataifa uliongeza vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini mwezi jana baada ya Pyongyang kufanya jaribio la silaha za nyuklia.
Bw Griffiths amesema ni "mara ya kwanza katika historia ya UN" kwa marufuku kama hiyo kutekelezwa.

"Kuna meli nne ambazo zimewekewa marufuku na kamati (ya UN). Hatua hii haina maana ya kuzuiwa kwa mali au marufuku ya usafiri. Ni marufuku ya kutotembelea bandari," alisema Jumatatu baada ya mkutano kuhusu utekelezwaji wa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.
Meli ambazo zimepigwa marufuku ni Petrel 8, Hao Fan 6, Tong San 2 na Jie Shun.
Kwa mujibu wa tovuti inayofuatilia safari za meli ya MarineTraffic Petrel 8 imesajiliwa Comoros, Hao Fan 6 visiwa vya Saint Kitts na Nevis, na Tong San 2 imesajiliwa Korea Kaskazini.
Haijabainika Jie Shun imesajiliwa katika taifa gani.

UN iliidhinisha vikwazo zaidi dhidi ya Korea Kaskazini mwezi Septemba
Korea Kaskazini imeshutumu hatua ya UN na Marekani kuiwekea vikwazo.
"Hatua hii ya kuwekea vikwazo na shinikizo kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea itawazindua tu watu wa Korea kuchukua hatua na kuimarisha nia yao ya kutaka kulipiza kisasi udhalimu wa Marekani na kufikisha mikomo uhasama wa miongo mingi," taarifa katika vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini ilisema Jumatatu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search