Thursday, 19 October 2017

Vigogo UVCCM Wasema Rushwa Bado ni Tatizo


Licha ya sifa nyingi anazomwagiwa Rais John Magufuli katika mapambano ya rushwa na ufisadi, Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) umesema bado lipo tatizo la rushwa nchini.

Kutokana na tatizo hilo, mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya na Songwe, Aman Kajuna amemtaka Rais Magufuli kutumia nguvu kubwa katika mapambano hayo kwa kuwa Taifa linaendelea kutafunwa kila uchwao.

Kajuna, ambaye aliongozana na mwenyekiti mwenzake wa Kagera, Yahaya Katema walikuwa wakizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM na walimsifu Rais kuwa amekuwa kiongozi wa mfano kwa kazi nyingi lakini wakatilia shaka maeneo matatu. Aliyataja maeneo hayo kuwa ni rushwa, kilimo na ukosefu wa maji aliosema bado wananchi wengi vijijini wanalia kukosa maji na kumtaka Rais kutupia macho katika maeneo hayo. “Ni kweli bado tuna changamoto kubwa kwa baadhi ya maeneo; kwanza rushwa bado inatutafuna naomba Rais aongeze nguvu, kilimo nacho kinaonekana kusahaulika lazima tuangalie na pia ilani yetu ilitaja upatikanaji wa maji, kweli bado ni tatizo kubwa,” alisema Kajuna.

Akizungumzia mchujo wa vijana waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika ndani ya umoja huo, alisema mchakato ulikwenda vizuri na kulikuwa na hoja zenye nguvu ambazo zilitolewa majibu bila ya kuwaathiri.

Mwenyekiti wa Kagera, Katema alisema kuna mambo mengi ambayo hayajatekelezwa, lakini akasisitiza kuwa ni mapema kutoa majibu kwa sasa kwa kuwa ilani inatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano.

Katema alimpongeza Rais kuwa anafanya kazi nzuri ambayo CCM ingetamani iwe na mtu wa aina hiyo hivyo ni vyema Watanzania wakawa wavumilivu kwa sasa ili wapatiwe maendeleo.

Pia, mwenyekiti huyo alimpongeza naibu katibu mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka kuwa amekuwa nguzo imara ndani ya umoja huo ikiwamo kujibu hoja za wapinzani kwa wakati na kusababisha utulivu mkubwa.

Umri kigezo muhimu

Shaka akizungumza na waandishi wa habari jana alisema asilimia 98 ya wagombea walijitokeza katika usaili ambao umechukua siku nne.

“Wengine walituma barua na dharura zao kwa nini hawakuja katika zoezi la usaili. Wengine pia wamejitoa, lakini wametuma barua za kujitoa,” alisema.

Kaimu katibu mkuu huyo alisema taarifa ya mchakato huo zitapelekwa kwenye Sekretarieti ya Kamati Kuu kwa ajili ya kuendelea na vikao vingine vya kuwajadili kabla ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho ndicho kikao cha mwisho kwa nafasi za uwakilishi wa chama.

Katika nafasi ya uenyekiti wa Taifa, wanachama 113 walijitokeza, makamu mwenyekiti 23 na nafasi tano za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia vijana wajitokeza 118.

Bila kueleza sababu za kujitoa, Shaka alisema mgombea mmoja wa nafasi ya uenyekiti aliandika barua ya kujitoa katika kinyang’anyiro cha kuomba nafasi hiyo inayoachwa wazi na mbunge wa Donge, Khamis Juma Sadifa.

“Msingi wa umoja wa vijana ndani ya kanuni ni umri, kwa hiyo tulijiridhisha kupitia kwa mamlaka, vyanzo vyetu sisi wenyewe kupitia mamlaka zinazohusika lakini kupitia kwa mhusika mwenyewe na vielelezo vyake,” alisema Shaka.

“Tutakwenda kusimamia haki baada ya kujiridhisha kuwa huyu ndiye mgombea mwenyewe na hivi ndivyo vielelezo vyake. Kwa sababu amepata nafasi ya kusalimia wajumbe (kamati ya utekelezaji) na tukapima capacity (uwezo) yake katika ku-face audience (kukabiliana na hadhara) lakini pia na kujenga hoja, kwa hiyo ni mafanikio kwetu tumeona uwezo wa wanachama wetu walionao,” alisema.

Shaka alisisitiza kuwa wagombea wa nafasi zote za jumuiya hiyo wanatakiwa hadi kumaliza muda wao wa kuongoza iwapo watachaguliwa wawe chini ya miaka 35.

Alisema usaili huo utawaweka katika nafasi nzuri ya kukishauri chama kwa kuwa miongoni mwao wapo watakaofanikiwa na wapo watakaosubiri.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search